26.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 26, 2023

Contact us: [email protected]

Wananchi wa Maswa watakiwa kutunza vyanzo vya maji

Na Samwel Mwanga, Maswa

WANANCHI wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu wanaoishi kandokando ya vyanzo vya maji likiwemo Bwawa la New Sola lililoko katika kijiji cha Zanzui wametakiwa kuvitunza na kuviendeleza vyanzo hivyo vya maji vilivyopo katika maeneo yao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa,Mhandisi Nandi Mathias(aliyenyoosha mkono)akimweleza Balozi wa Maji Nchini,Msanii Mrisho Mpoto(mwenye kofia nyeusi)jinsi chujio la maji linavyochuja maji kabla ya kusambazwa kwa wananchi wa mji wa Maswa na vijiji 12 vinavyohudumiwa na Bwawa la New Sola.(Picha Na Samwel Mwanga).

Balozi wa Maji nchini, Msanii Mrisho Mpoto ametoa wito huo Julai 23, mwaka huu kwa wananchi wa Vijiji vya Kata ya Zanzui, Ng’wigwa na Nguliguli wilayani humo ambao ndiyo wanazunguka bwawa hilo ambacho ndicho chanzo pekee cha maji katika mji wa Maswa na vijiji 12.

Akizungumza na wananchi hao katika eneo la bwawa hilo kwenye kijiji cha Zanzui, Balozi Mpoto amesema kuwa anafanya ziara ya kujionea uhifadhi wa vyanzo mbalimbali vya maji hapa nchini.

Amesema kuwa vyanzo vya maji vilivyopo katika maeneo yetu ni muhimu sana, kwani vimekuwepo tangu miaka mingi na kutunzwa na watu mbalimbali hadi kufikia hapa, hivyo hakuna budi kwa kila mwananchi kuendelea kuvitunza na kuvilinda, ili viweze kuisadia jamii na watanzania wote kiujumla, na hasa kizazi kijicho.

Balozi Mpoto amesema kuwa si jambo rahisi kwa wafugaji kutunza chanzo cha maji lakini amestaajabu kuona wafugaji wanaozunguka bwawa hilo wameweza kulitunza na kulilnda jambo ambalo wanastahili kupatiwa pongezi sambamba na zawadi.

“Kutunza chanzo cha maji kama hili bwawa lenu si jambo rahisi tena kwa wafugaji ambao wamekuwa wakudaiwa kuwa ndiyo waharibifu wakubwa wa vyanzo vya maji kwa ninyi kuna jambo la kujifunza kwani mmeweza mnastahili pongezi na kupewa zawadi.

“Wananchi wa maeneo haya mkishirikiana na Bonde la Ziwa Victoria pamoja na Mamlaka ya Maji ma usafi wa Mazingira Maswa(MAUWASA) bila kuusahau uongozi wa serikali wa  wilaya ya Maswa kwa kweli mmefanya kazi kubwa ya uhifadhi wa bwawa hili na ndiyo maana hadi sasa lina hali mzuri na linawahudumia maji wananchi kwa kupata maji safi na salama,”amesema.

Amesema ni vizuri wakaendeleza kulilinda bwawa hilo kwa kuendelea kupiga marufuku kufanyika shughuli za kibinadamu kwenye bwawa hilo kama vile kilimo na ufugaji kwani athari zake ni kubwa sana ambazo ni pamoja ma kuchafua maji sambamba na kusababisha bwawa kukauka kutokana na uharibifu wa mazingira.

 Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Victoria, Dk. Renatus Shinhu amesema kuwa wao ndiyo wanajukumu la kuhifadhi chanzo hicho cha maji hivyo wameshirikiana na wananchi wa maeneo wanaozunguka bwawa hilo kutambua maeneo ya mipaka ya bwawa na kuweka vigingi.

“Niwaombe wananchi tuendelee kushirikiana kukitunza chanzo hiki kwani kwa pamoja tumeweka mipaka ya bwawa hili na tuendelee kuiheshimu maana wanufaika wakubwa wa bwawa hili ni sisi wenyewe na vizazi vyetu vijavyo,”amesema Dk. Shinhu.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa, Mhandisi Nandi Mathias ambao ndiyo wamiliki wa bwawa hilo amesema kuwa mwaka 2017 bwawa la New Sola lilikauka baada ya wananchi kufanya shughuli za kibinadamu kama vile kilimo, ufugaji na uharibifu wa mazingira lakini baadaye waliweza kushirikiana na Bonde la Ziwa Victoria,Uongozi wa serikali wa wilaya ya Maswa na kuweza kuondoa hali hiyo na kuweza kufanikiwa kwenye uhifadhi hali ambayo wanaendelea nayo kwa sasa.

“Kwa kweli sina budi kuipongeza Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Victoria pamoja na Uongozi wa serikali wa wilaya ya Maswa kwa kuweza kusimamia uhifadhi katika bwawa hili anbacho ndicho chanzo pekee cha maji katika mji wetu wa Maswa na vijiji 12 na linategemewa na watu wapatao  111,074,” amesema Mhandisi Mathias.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,726FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles