30 C
Dar es Salaam
Saturday, December 4, 2021

Wananchi Mtwara washauriwa kujiepusha na magendo

Oliver Njunwa, Mtwara

Wananchi wanaoishi katika vijiji vilivyo pembezoni mwa Bahari ya Hindi mkoani Mtwara, wametakiwa kuwa walinzi wa mipaka ya nchi kwa kutoa taarifa za watu wanaofanya biashara za magendo katika maeneo yao ili kuepukana na athari zinazotokana na biashara na matumizi ya bidhaa hizo.

Wito huo umetolewa jana na Ofisa Mkuu Usimamizi wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Valentina Bartazar wakati akitoa elimu ya uzuiaji wa bidhaa za magendo kwa wananchi wa mkoani Mtwara katika vijiji mbalimbali.

Amesema biashara za magendo zina athari za kiafya, kijamii, kiuchumi pamoja na usalama kwa wananchi wa maeneo husika na taifa kwa ujumla.

“Tumetembelea vjijiji vya Msangamkuu, Msimbati, Kivava, Kitaya na Dindwa wilaya ya Mtwara, Mihambwe, Chikongo Wilaya ya Tandahimba na Chikunya Wilaya ya Newala mkoani Mtwara ili kuwapa elimu ya madhara ya biashara ya magendo wananchi wa maeneo hayo na kuwataka kutoa taarifa za watu hao ambao si wazalendo kwa taifa lao,” amesema Bartazar.

Amesema bidhaa za magendo ni hatari kwa afya za wananchi kutokana na kuwa zinapoingizwa nchini hazifuati utaratibu wa kuthibitishwa ubora na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Kwa upande wake Ofisa Forodha wa TRA, Mkoa wa Mtwara,  Salvatory Chami amesema baadhi ya bidhaa zinazoingizwa nchini kwa njia ya magendo kutoka nchi jirani ya Msumbiji hazistahili kulipiwa kodi kutokana nchi hizo kuwa na makubaliano ya kibiashara.

“Ofisi za TRA ziko wazi kwa ajili ya kuwashauri wananchi ambao wanataka kufanya biashara ya kuingiza bidhaa ndani ya nchi hivyo wananchi mnashauriwa kutembelea ofisi hizo kupata ushauri kabla ya kufanya bashara ili muweze kufahamu bidhaa zinazostahili kulipiwa ushuru na ambazo hazistahili kulipiwa ushuru.

“Pia mfahamu bidhaa zinazostahili kuingizwa nchini na viwango vya kodi vinavyostahili kutozwa kwa bidhaa hizo,” amesema Chami.

Naye Ahmad Juma mkazi wa Kijiji cha Chikunya Wilaya ya Newala amesema wanaomba serikali ihalalishe vituo vya forodha vilivyo jirani na vijiji hivyo ili waweze kufanya biashara halali na kulipa kodi stahiki.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Msangamkuu kilichopo Wilaya ya Mtwara, Hamdani Mohammed amesema elimu hiyo inahitajika mara kwa mara ili kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kulinda mipaka yao kwa kuzuia vitendo vya biashara ya magendo.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,968FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles