24.4 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wengine sita wahojiwaTakukuru kashfa ya Lugola

Ramadhan Hassan – Dodoma

WAFANYAKAZI sita wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji  waliokuwa kwenye kamati ya utekelezaji wa makubaliano  na Kampuni ya Rom Solutions Co. Ltd ya nchini Romania, jana walihojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani hapa.

Wajumbe hao wanahojiwa kutokana na kashfa ya watendaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ya zabuni ya kununua vifaa vya zimamoto vyenye thamani ya Euro milioni 408 (Sh trilioni moja).

Inadaiwa walipoenda kwenye mazungumzo, walipewa  kompyuta mpakato (Laptop) na walilipwa Dola za Marekani 800 kwa kila kikao walichohudhuria na Kampuni ya Rom Solution.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Takukuru waliohojiwa jana ni Kamishna wa Zimamoto, Mbaraka Semwanza, Naibu Kamishna wa Zimamoto, Fikiri Salala, Naibu Kamishna wa Zamamoto, Lusekela Chaula, Naibu Kamishna wa Zimamoto, Ully Mburuko, Ofisa Ugavi Mkuu wa Zimamoto, Boniface Kipomela na Mchumi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Felis Mshana.

Wakiwa na nyuso za huzuni, wafanyakazi hao walifika majira ya saa nne asubuhi kwa pamoja katika Ofisi za Makao Makuu ya Takukuru jirani na Uwanja wa Jamhuri jijini hapa.

Waliingia kila mmoja akiwa na Laptop ambazo walipewa na kampuni hiyo ya Rom Solution ambapo walianza kuingia mmoja mmoja kwenda mapokezi na kisha baadae kuingia ndani kuhojiwa.

Wiki iliyopita Takukuru waliwahoji watendaji wa juu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi akiwamo Naibu Katibu Mkuu, Ramadhan Kailima na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni.

Wengine waliohojiwa ni aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu na aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye.

Baada ya kuhoji watendaji hao, Takukuru inakuwa imekamilisha kazi ya kuwahoji watendaji 11 wa wizara hiyo kufuatia agizo la Rais Dk. John Magufuli kuhusiana na mkataba ulioingiwa na wizara hiyo wa Sh trilioni 1 kununua vifaa vya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kupitia Kampuni ya Rom Solutions Co. Ltd.

“Watu wamekosa uadilifu, hivi karibuni kulikuwa na mkataba mmoja wa ajabu unaotengenezwa Wizara ya Mambo ya Ndani wenye thamani ya zaidi ya Sh trilioni 1. Mradi huo umesainiwa na Kamishna Jenerali wa Zimamoto,” alinukuliwa Rais Magufuli katika sehemu ya hotuba yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles