23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

WANANCHI LINDI WALALAMIKIA NOTISI YA TANROADS

Hadija Omary, Lindi                   |

Wananchi wa Kata ya Milola na Rutamba, Halmashauri ya wilaya ya Lindi mkoani hapa, wamelalamikia utaratibu uliotumiwa kuwaondoa na Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Lindi wa kuwapatia notisi ya siku 14 kuwataka wabomoe nyumba zao zilizopo kwenye hifadhi ya barabara.

Hayo yameibuka kwenye kikao rasmi kilichokutanisha wananchi wa Vijiji vinavyounda tarafa hiyo vya Rutamba ya Zamani, Rutamba ya sasa, Kinyope Milola A, Milola B na Mkangaulani.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kinyope, Omary Limbendela baadhi ya wananchi wa kijiji chake walipokea notisi ya kuwataka wahame kwenye makazi yao sanjari na kubomoa nyumba zao.

“Wananchi hawa hawalalamikii kuhama au kubomoa nyumba zao kwa kuwa tayari zilishawekea alama ya ‘X’ miaka 10 iliyopita, ila wanacholalamikia ni muda wa siku 14 uliotolewa na Idara ya Ujenzi kwani hautoshi kuwapa nafasi wananchi hao kufanya maandalizi ya makazi mapya.

“Kama ukiwa mpangaji wa nyumba ya mtu binafsi unapewa notisi ya siku 90 ya kutafuta makazi mapya na ukizembea unaweza kupewa barua nyingine, iweje serikali kwa mara ya kwanza tu iwape notsi ya siku 14,” amesema.

Amesema suala hilo linaweza kuwafanya wananchi wakose imani kwa serikali yao kwa uzembe wa watu kutofuata sheria, kwani waliweka alama kuwaonyesha hawatakiwi kuendeleza nyumba zao na ikumbukwe kuweka alama ni jambo moja na kubomoa ni jambo jingine.

Kutokana na hali hiyo, amehoji ni kwanini wasipewe muda wa kutosha wananchi hawa wakafanya maandalizi.

Naye Omary Nangumbi, mkazi wa Kijiji cha Kinyope ambaye ni mmoja wa waathirika, amewaomba watendaji wa serikali kuzingatia sheria na taratibu pale ambapo kuna shughuli za maendeleo zinazotarajia kufanyika na kuingia katika makazi ya wananchi.

“Hii nchi inaongozwa kisheria na taratibu na hiki kijiji kipo kwa mujibu wa sheria na kimesajiliwa hata wananchi wake pia wapo kwa mujibu wa sheria, kama hivyo kunapotokea shuguli ya maendeleo inakuja na inawakuta watu kwenye maeneo ni vyema taratibu za sheria zitumike sisi wananchi ni waelewa tutaupisha lakini kwa mfumo uliokuja si wa kisheria na uko tafauti na nchi yetu inavyoendeshwa,” amesema

Akizungumza kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Mchinga, Hamidu Bobali Katibu wa Mbunge huyo, Hussen Kimbyoko amesema licha ya wananchi hawa kulalamikia muda uliotolewa kuwa hautoshi  pia utaratibu na sheria zilizotumika kuwaondoa wananchi hao hazikuwa rafiki.

“Ukiangalia historia ya vijiji hivyo vilianza mwaka 1974, wakati wa operesheni vijiji ambapo wananchi kutoka maeneo tofauti walikusanywa na kupelekwa kwenye maeneo hayo ambapo kwa wakati huo  bara bara hizo zilikuwa zikijulikana barabara za wilaya.

“Wakati wananchi hawa wanahamia barabara hizi zilikuwa za wilaya ila baada ya  kijiji cha jirani cha Ruangwa kupandishwa hadhi na kuwa wilaya ndipo mwaka 2018  barabara hii ikapandishwa hadhi kuwa ya mkoa, ni wazi kuwa imewafuata wananchi na kulipwa ni haki yao ya msingi, ni ajabu kwa wananchi hawa kutakiwa kuhama bila ya kulipwa chochote ni barabara za wilaya,” amesema.

Kwa upande wake Meneja wa Tanroads Mkoa wa Lindi, Isack Mwanawima amethibitisha wananchi hao kupewa notisi na kuongeza kuwa kuwa zoezi la ubomoaji wa nyumba hizo hauhusiani na kupisha ujenzi wa barabara kama malalamiko ya wananchi yanavyodaiwa bali zoezi hilo ni la kuwaondoa wananchi waliovamia barabara.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles