27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

Wanafunzi UDSM kuanza kunolewa kujiajiri

NA LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM

WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wanatarajiwa kuanza kupewa mafunzo ya ujasiriamali, ili kuwawezesha kujiajiri na kuachana na dhana ya kutegemea kuajiriwa pekee.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa utilianaji saini makubaliano na Kampuni ya Empower yatakayowezesha kutoa mafunzo ya ubunifu na ujasiriamali kwa wanafunzi jana, Naibu Makamu Mkuu wa Utafiti, Profesa Bernadeta Killian, alisema kwa miaka mitano ijayo makubaliano hayo yatahusisha wanafunzi wa mwaka wa mwisho wa kozi mbalimbali.

Profesa Bernadeta alisema katika mwaka wa kwanza wa makubaliano hayo, wanafunzi 250 wa kozi mbalimbali wanatarajiwa kunufaika baada ya kuanza mwaka mpya wa masomo 2020/2021 unaotarajiwa kuanza Novemba.

Alisema kuwa ushirikiano wao na kampuni hiyo unaendeleza dhamira ya chuo hicho ya kuleta maendeleo ya kijamii, kuichumi na kisiasa.

Profesa Bernadeta alisema makubaliano hayo ni mwanzo mzuri kwa kuzingatia kuwa chuo hicho ni miongoni mwa taasisi za elimu zinazoingiza idadi kubwa ya wahitimu katika soko la ajira ambapo kwa mwaka hutoa zaidi ya wahitimu 7,000 huku kikiwa na zaidi ya wanafunzi 35,000 wanaoendelea na masomo na kozi zaidi ya 350.

“Hata kabla ya makubaliano haya, katika kitengo chetu cha ubunifu na ujasiriamali tumekuwa na shughuli mbalimbali za kuwajengea ujuzi wanafunzi wetu, sasa makubaliano haya yataanza na wanafunzi ambao wako mwaka wa pili wanaotarajia kuanza mwaka wa tatu.

“Kumekuwa na taarifa kuwa wahitimu katika taasisi nyingi za elimu ya juu nchini hawaajiriki kwa kutokidhi vigezo vya mahitaji ya soko la ajira, sisi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tunataka kupunguza hilo ‘gap’ (pengo) kwa kusogeza karibu wadau ikiwamo sekta binafsi ambao ndiyo waajiri,” alisema Profesa Bernadeta.

Alisema ili kuhakikisha wahitimu wa chuo hicho wanakuwa na ujuzi unaowawezesha kujiajiri, tayari chuo hicho kitaanza kutoa masomo ya ujasiriamali kwa kozi zote zinazotolewa tofauti na sasa ambapo hutolewa kwa baadhi ya kozi tu.

“Mabadiliko haya yatakwenda pamoja na maboresho ya mitaala inayolenga kuongeza ubunifu kwa wahitimu wetu,” alisema Profesa Bernadeta.

Naye Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Empower, Miranda Naiman, alisema taasisi hiyo inafahamu kuwa wanafunzi wanahitaji ujuzi utakaowawezesha kujiajiri ndiyo maana wameamua kutoa mafunzo hayo na kwamba wanajivunia kuwa na ushirikiano na chuo hicho.

Miranda alisema kama programu hiyo itaonyesha mafanikio, watapanua wigo wa mafunzo hayo kwa vyuo na taasisi nyingine za elimu ya juu nchini.

Aidha, alizitaka taasisi ikiwamo sekta binafsi kujitokeza kusaidia utoaji wa mafunzo ya aina hiyo ili kuwezesha vijana wengi wanaohitimu masomo kujiajiri badala ya kutegemea kuajiriwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles