25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wagombea wanaodhalilisha wanawake waonywa

NA ASHA BANI-DAR ES SALAAM

WANAMTANDAO wa Katiba, Uchaguzi na Uongozi ambao ni watetezi wa haki za wanawake na wasichana, wamekemea lugha za matusi kwa wanawake zinazotolewa na baadhi ya wagombea tangu kuanza kwa kampeni za Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 28.

Akisoma tamko hilo, Mwenyekiti wa Mtandao wa Jinsia nchini (TGNP), Asseny Muro alisema wamekuwa wakifuatilia kampeni za uchaguzi tangu zilipoanza ambapo matukio ambayo tayari yameshajitokeza bi pamoja na utumiaji wa lugha za matusi na kauli za udhalilishaji dhidi ya wanawake wanaogombea na wafuasi wa vyama kwa ujumla. 

“Ni vyema tutambue kwamba kasumba hii mbali na kwamba ni kinyume na haki za binadamu na ni kosa kisheria, inarudisha nyuma jitihada za Serikali katika kufikia usawa wa kijinsia na kurudisha nyuma ari ya wanawake wengi kugombea nafasi za uongozi kwa sababu ya kuogopa kudhalilishwa.

“Pia inanyamazisha sauti za wanawake ambao ni zaidi ya nusu ya Watanzania wote ambao ni wapigakura wakuu na ambao wana haki ya ushiriki salama katika masuala ya kisiasa, suala ambalo halina tija kwa taifa letu,” alisema Asseny. 

Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo wameona kuna umuhimu wa vyombo na mamlaka zinazohusika kuwawajibisha kwa mujibu wa sheria, kanuni na maadili ya uchaguzi kwa wote wanaotumia matusi na lugha za kudhalilisha wanawake. 

“Sisi wanamtandao watetezi wa haki za wanawake nchini, tunachukulia matukio haya kama kuvunjwa kwa Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977), inayokataza ubaguzi wa aina yoyote, na tunaikumbusha jamii  kwamba kanuni ya makosa ya adhabu, sura ya 16, kifungu cha 89 kinataja kutumia lugha chafu dhidi ya mtu mwingine kuwa ni kosa la jinai. 

 “Tunaomba umma wa Watanzania na vyombo mbalimbali vinavyosimamia uchaguzi wa taifa hili kutambua kwamba ushiriki wa wanawake katika michakato ya uchaguzi ni haki yao ya kikatiba, na zimebainishwa katika sheria mbalimbali za nchi, ” alieleza Asseny. 

Alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi huweka wazi kanuni mbalimbali za uchaguzi na maadili ya vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi kwa  lengo la kuweka mazingira wezeshi kwa Watanzania wote, wa kike na wa kiume, kushiriki katika mchakato huu wa uchaguzi na kutoa mchango wao, kwa uhuru, uwazi na amani. 

Pia alisema Sheria ya Vyama vya Siasa iliyorekebishwa mwaka 2018, katika kifungu chake cha 9, inakataza viongozi na wanachama kutamka au kutumia lugha za matusi, maneno ya kudhalilisha, uchochezi, au alama ambazo zinaweza kusababisha au kuhatarisha amani na ukosefu wa umoja wa kitaifa. 

Asseny aliongeza kuwa kwa kuzingatia makatazo yanayotolewa na tume kuhusu udhalilishaji kwa wanawake, wamezitaka  mamlaka zinazohusika kuwachukulia hatua kali wagombea pamoja na wapambe wao wanaotoa lugha za kudhalilisha na kutukana wanawake kwenye kampeni au mahali popote wakati huu wa uchaguzi.

Pia viongozi wa taasisi mbalimbali zikiwemo za dini, na hasa vyama vya siasa, asasi za kiaraia na jamii yote kwa ujumla ya Tanzania kukemea vikali tabia hizi za kudhalilisha wanawake, hasa kipindi hiki cha uchaguzi. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles