22.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Wamekuja kufanya mapinduzi Ligi ya England

makocha England

BADI MCHOMOLO NA MITANDAO,

AGOSTI 13, mwaka huu michuano ya Ligi Kuu nchini England,itaanza kutimua vumbi kwenye viwanja mbalimbali, huku tukitarajia kuyaona makubwa kwenye michuano hiyo.

Kama msimu huu ambao umemalizika hivi karibuni ambapo Leicester City wakawa mabingwa wapya, hivyo tunatarajia kuyaona mambo mapya kutokana na maandalizi yanayoendelea na klabu hizo ambazo zinashiriki ligi hiyo.

Kwa sasa kuna ushindani katika usajili ambao unaendelea kwa ajili ya msimu huo, wakati huo tayari klabu zimeanza mazoezi ya pamoja na michezo ya kirafiki kwa ajili ya kijiweka sawa.

MTANZANIA Spoti Kiki, leo hii imekuandalia uchambuzi juu ya makocha wapya na wa kutazamwa kwenye msimu mpya wa Ligi Kuu nchini England kutokana na uwezo wao na uzoefu.

Jose Mourinho (Manchester United)

Huyu ni kocha mpya wa klabu ya Manchester United ambaye anaanza kazi msimu huu wa ligi, lakini awali alikuwa anaitumikia klabu ya Chelsea ambayo aliipa ubingwa wa Ligi Kuu msimu wa 2014-2015.

Lakini alishindwa kutetea ubingwa msimu uliopita, hivyo uongozi wa Chelsea uliamua kuachana nayo pamoja na matatizo yake mengine, lakini United wanaelewa uwezo wa kocha huyo, hivyo wakampa nafasi.

Mbinu zake

Mourinho anajulikana kwa uwezo wa kutengeneza safu ya ulinzi iliyo bora, alifanikiwa kutwaa Ligi ya Mabingwa akiwa na klabu ya Inter Milan, katika ubingwa huo Mourinho alionekana kuwa na kikosi bora cha ulinzi.

United ikiwa chini ya kocha Louis van Gaal, ilikuwa inajaribu kucheza soka la kufurahisha mashabiki, lakini hayo yote Mourinho anayaweza pamoja na kuondoka na mataji, hivyo mashabiki wanatarajia kuona mbinu za kupaki basi, za ushindi.

Usajili

Mourinho wakati anajiunga na Chelsea kwa mara ya kwanza alifanya usajili wa Didier Drogba, Ricardo Carvalho na Michael Essien. Kwa mara ya pili kabla ya kufukuzwa alifanya usajili wa Baba Rahman, Pedro, Papy Djilobodji na Radamel Falcao.

Lakini tangu amejiunga na United tayari amefanya usajili wa beki Eric Bailly kutoka Villarreal, Zlatan Ibrahimovic na sasa anamuangalia Paul Pogba.

Uhusiano na mashabiki

Mashabiki wa Chelsea walifurahishwa na uwepo wake kwa vipindi viwili tofauti akiwa Stamford Bridge, sawa na kipindi yupo Real Madrid, mashabiki walikuwa na furaha kubwa.

Hali hiyo inatarajiwa kutua kwa mashabiki wa United, huku wakiwa wanatarajia kuona soka safi la kuvutia pamoja na mataji mbalimbali.

Pep Guardiola (Manchester City)

Ni kocha mpya wa Manchester City ambaye amejiunga na klabu hiyo mara baada ya kumalizika kwa Ligi msimu uliopita. City wanatarajia makubwa kutoka kwake kutokana na uwezo wake ambao aliuonesha akiwa Barcelona pamoja na Bayern Munich.

Mbinu zake

Mashabiki wa City wanatarajia kuona timu yake ikicheza soka kama la Barcelona au Bayern Munich, lile la kufurahisha hasa katika kipiga pasi nyingi na kumiliki mpira, Guardiola anatumia mbinu ya tiki-taka. Muda mwingi timu yake inakuwa inashambulia.

Usajili

Mipango ya Guardiola haiko tofauti sana na Mourinho, tangu akiwa Barcelona na Bayern Munich, lakini baada ya kujiunga na City alianza na usajili wa Ilkay Gundogan, pamoja na Nolito, na hivi sasa wanatarajia kufanya usajili wa wachezaji wawili kabla ya Ligi kuanza.

Uhusiano na mashabiki

Mashabiki wa Barcelona walikuwa na huzuni baada ya kocha huyo kutangaza kuondoka mwaka 2012 na kujiunga na Bayern Munich, hata hivyo baada ya kujiunga na timu hiyo ya Ujerumani alifanya makubwa na kuwafurahisha mashabiki.

Hivyo mashabiki wa Manchester City wanatarajia kuwa na furaha kubwa wakati wote huku wakiamini kuwa wanaweza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na hata Klabu Bingwa Ulaya.

Antonio Conte (Chelsea)

Ni kocha mpya wa Chelsea ambaye amechukua nafasi ya Jose Mourinho ambaye amejiunga na Manchester United. Conte ametokea timu ya taifa ya Italia.

Mbinu zake

Siku zote kocha huyo amekuwa akipenda kutumia mfumo wa 3-5-2, ambapo mfumo huo amekuwa akiutumia sana tangu alivyokuwa klabu ya Juventus na timu ya Taifa ya Italia.

Mfumo huo uliwafanya Italia waonekane tishio kwenye michuano ya Euro 2016, hasa pale walipokutana na Ujerumani kwenye hatua ya robo fainali.

Mashabiki wa Chelsea wanatarajia kuona klabu yao ikiwa na safu imara ya ulinzi, pamoja na kushambulia kwa kupiga mipira ya mbali (counter-attack).

Usajili

Wakati yupo Juventus alifanya usajili wa Paul Pogba kutoka Manchester United, pamoja na Arturo Vidal.

Tangu amejiunga na Chelsea, kocha huyo tayari amefanya usajili wa mshambuliaji Michy Batshuayi kutoka klabu ya Marseille kwa kitita cha pauni milioni 3, na sasa anafanya mazungumzo na kiungo wa Leicester City N’Golo Kante na Radja Nainggolan.

Uhusiano na mashabiki

Mipango ya kocha huyo siku zote inawafanya mashabiki kuwa na furaha tangu akiwa na timu ya Taifa ya Italia na klabu ya Juventus, kwenye michuano ya Euro 2016 mashabiki wa Italia walikuwa na furaha kubwa kutokana na kile ambacho alikuwa anakifanya japokuwa walitolewa.

Hata hivyo, mashabiki wa Chelsea wameanza kumzungumzia kocha huyo wakidai kwamba amekuja kubadilisha soka na kuwapatia mataji, hivyo kila shabiki ana imani na kocha huyo.

Jurgen Klopp (Liverpool) 

Alijiunga na Liverpool mwishoni mwa msimu wa Ligi Kuu, lakini aliweza kufanya mabadiliko ambayo aliyaacha kocha Brendan Rodgers, na sasa Liverpool wanatarajia kuyaona makubwa.

Mbinu zake

Mbinu zake za kushambulia kwa kasi ziliweza kuinufaisha klabu ya Borussia Dortmund wakati anaitumikia timu hiyo kabla ya kujiunga na Liverpool.

Hata hivyo, aliweza kufanya hivyo tangu alipoichukua Liverpool na kuwafanya wafanikiwe kucheza fainali ya Europa. Liverpool wanaamini hali hiyo itaendelea kwenye msimu mpya wa Ligi Kuu.

Usajili

Dortmund waliwahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Ujerumani mara mbili na kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa 2013 kutokana na wachezaji ambao aliwasajili kama vile Mats Hummels na Robert Lewandowski.

Katika kipindi hiki cha usajili kocha huyo ameweza kuwasajili Sadio Mane, Loris Karius na Joel Matip kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi akiwa na Liverpool.

Uhusiano na mashabiki

Amekuwa na uhusiano mzuri na mashabiki wa Liverpool tangu alipowasili hapo, hivyo wanaamini kutokana na maandalizi yanayoendelea lazima wataweza kufanya makubwa msimu mpya wa Ligi Kuu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles