24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Hili ni funzo kwa Yanga fainali mwakani

PLUIJM (2)

NA ZAINAB IDDY,

WAWAKILISHI Tanzania katika michuano ya kimataifa, Yanga wameendelea kupoteza mwelekeo katika harakati za kutinga nusu fainali za michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Ndoto ya Yanga kutinga hatua hiyo ilianza kuyumba baada ya kupokea kipigo cha bao 1-0 wakiwa ugenini nchini Algeria walipocheza na Mo Bejaia, kabla ya kuja kufungwa nyumbani idadi kama hiyo hivyo na TP Mazembe ambao ni mabingwa wa mwaka jana katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika.

Kilio cha Wanajangwani na Watanzania kwa ujumla ni kuona Yanga inawatoa kimasomaso kwa kuingia fainali kama ilivyokuwa kwa watani zao, Simba mwaka 1993. Lakini juzi Yanga walijikuta wakilazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya Medeama ya Ghana.

Kwa matokeo ya michezo mitatu iliyocheza Yanga, imeambulia pointi moja, ikiwa inaburuza mkia katika kundi lake A, iliyopo sambamba na Medeama walio nafasi ya tatu, Bejaia walioshika namba mbili na Mazembe walioongoza kundi kabla ya mchezo wao wa jana na Bejaia.

Ni wazi matokeo hayo yanaifanya Yanga kupoteza matumaini ya kutinga nusu fainali licha ya kocha wake mkuu, Hans van de Pluijm, kusema kuwa wana nafasi ya kuingia nusu fainali jambo ambalo linaonekana ni sawa na ndoto za mchana kulingana na pointi walizonazo wapinzani wake pamoja na mechi zilizobaki kwa Wanajangwani hao.

Iwapo kama tutatumia usemi wa Kiswahili unaosema yaliyopita  yamepita tugange yajayo, basi ni wazi Yanga inawalazimu kuchukulia mashindano hayo kama sehemu ya kujifunza kwa ajili ya mashindano ya mwakani ambayo tayari wameshakata tiketi ya kushiriki.

Kwa hivi sasa ni wazi hatua iliyofikia Yanga ni somo kwao hivyo wanapaswa kulitumia kujiandaa na mwakani, lakini pia wakitakiwa kutambua kuwa kuna vitu lazima wavifanyie kazi, ili kutimiza nia yao iliyoelekea kuwashinda mwaka huu, miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na:-

Ushindi wa nyumbani

Kosa kubwa ambalo mwaka huu Yanga wamelifanya katika michezo yake kimataifa ya klabu ingwa kisha kombe la shirikisho baada ya kuangukia pua, ni kuruhusu kupoteza mechi za nyumbani.

Licha ya rekodi kuonyesha Wanajangwani mara nyingi wamekuwa na matokeo mazuri ugenini, lakini mara nyingi ushindi wa nyumbani unaibeba timu.

Ni wakati wa kocha Hans van de Pluijm na msaidizi wake, Juma Mwambusi, kutafuta plani B ambayo itawawezesha kuwa na matokeo mazuri nyumbani.

Usajili wa kiungo mshambuliaji

Tatazo la kiungo mshambuliaji linaendelea kuiandama Yanga, kwani hivi sasa wanamtumia Thaban Kamusoko ambaye hana uwezo mzuri wa kupandisha na kushusha mpira uwanjani.

Awali, alikuwa akiimudu nafasi hiyo Salumu Telela, lakini baada ya Yanga kuamua kuachana naye kumekuwa na tatizo kubwa kwenye kiungo mshambuliaji.

Ni wakati wa benchi la ufundi kuangalia namna wanavyoweza kulimaliza tatizo la kiungo mshambuliaji ambaye atakuwa na sifa stahiki, ili kuisaidia katika mechi za kimataifa mwakani.

Semina elekezi ya CAF

Ni kawaida kabla ya kuanza mashindano yoyote lazima kutolewe semina elekezi itakayotoa mwongozo wa jinsi gani timu zitashiriki michuano hiyo.

Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), kama ilivyokuwa katika mashindano lilitoa waraka kwa timu zilizokuwa zinacheza kuwania kuingia hatua ya makundi (Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho) kupeleka majina ya maofisa watakaohudhuria semina ya namna ya kuratibu mechi hizo kuelekea fainali lakini pia walitakiwa kupeleka vivuli (photocopies) vya hati zao za kusafiria.

Maofisa waliohitajika ni meneja wa timu, daktari wa timu na ofisa habari wa timu, TFF iliwafikishia ujumbe Yanga kabla ya kucheza na Esperanca ya Angola kwa kuwataka kutuma nyaraka hizo kati ya Aprili 26 na Aprili 28, 2016.

Cha ajabu Yanga wanaojiita wa kimataifa, walishindwa kutekeleza maagizo hayo licha ya taarifa hizi na hata ukumbusho (reminders) zilipelekwa kwa barua pepe, simu na hata kuonana ana kwa ana kwa Katibu Mkuu wa Yanga, ofisa habari na viongozi wengine wa klabu.

Madhara ya kutoshiriki semina hiyo yaliweza kuonekana katika mchezo wa kwanza wa Yanga dhidi ya Mo Bejaia pale walipozuiliwa kutumia baadhi ya vitu vyao ikiwemo maji na jezi zenye nembo ya wadhamini Kilimanjaro.

Siku moja kabla ya washiriki kuanza kuwasili Cairo, Misri, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga alituma nyaraka kama zilivyotakiwa na wakatumiwa tiketi tatu (3) na CAF. Pamoja na tiketi kuletwa Yanga bado watu hao hawakusafiri wakidai klabu haijatoa ruhusa.

Umri wa wachezaji

Tatizo kubwa lililopo sasa ndani ya timu ya Yanga ni kuwa na wachezaji wenye umri mkubwa jambo ambalo linasababisha kutoendana na kasi iwapo watakutana na wachezaji wanaokimbia na mpira.

Wachezaji kama Kamusoko, Kelvin Yondani, Nadir Harub ‘Cannavaro’, Mbuyu Twite na wengineo, licha ya kucheza kandanda safi lakini mara nyingi hawawezi kuendana na kasi ya kimchezo wanapokutana na wanandinga damu zao zinazochemka.

Ifike wakati Yanga isiangalie kiwango cha mchezaji pekee  bali izingatie umri wa mwanandinga, kwani kusajili mchezaji mkubwa kiumri kunasababisha kuitumikia timu kwa muda mfupi kuliko thamani ya fedha alizosajiliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles