25.2 C
Dar es Salaam
Monday, May 6, 2024

Contact us: [email protected]

Waliovamia na kujenga kuzunguka Airport Mwanza waondoke mara moja-Silaa

Na Clara Matimo, Mwanza

Waziri wa Ardhi, Nyumba  na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa amesema wakazi wote waliovamia, kujenga nyumba na kuishi maeneo yasiyoruhusiwa kuzunguka uwanja wa ndege wa Mwanza waondoke mara moja na kwamba Serikali haitawapa fidia kwani baadhi ya watu hao walivamia wakiwa wanajua eneo hilo haliruhusiwi kwa makazi.

Baadhi ya watumishi wa sekta ya ardhi wakimsikiliza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa( hayupo pichani).

Waziri Silaa ametoa maagizo hayo leo Desema 12, 2023 wakati akizungumza na watumishi kutoka sekta ya ardhi na taasisi zilizo chini ya wizara yake kwenye ziara ya kikazi ya siku moja jijini Mwanza.

Amesema serikali inampango wa kupandisha hadhi uwanja huo wa ndege wa Mwanza uliopo wilayani Ilemela uwe wa kimataifa na tayari mkandarasi wa kujenga jengo la abiria pamoja na kuongeza urefu wa njia ya kutua na kuruka ndege amekwishapatikana kwa hiyo watu hao wanapaswa kuondoka kupisha uendelezaji huo.

“Maeneo mengi ambayo watu wanavamia, wanavamia wakijua wanavamia na hawana haki nayo, ukienda eneo la uvamizi aina ya nyumba ama maimarisho (uendelezaji) yanayofanyika pale ukiangalia unapata picha kabisa kwamba wanaelewa eneo hilo wamevamia.

“Kwenye baadhi ya halmashauri yapo maeneo wananchi walivamia baadhi ya maeneo ya hifadhi na maeneo mengine, serikali imeelekeza wananchi wale wamegewe maeneo na wafanyiwe mpango wa matumizi bora ya ardhi  lakini kwa uwanja wa ndege wa Mwanza hilo halitawezekana,” amesisitiza Waziri Silaa na kuongeza;

“Mambo ya ardhi huwa yanahadithi  nyingi sana zinatengenezwa ambazo ukizisikiliza kwa masikio mawili unaweza kuamini kwamba mtu yuko pale kwa mujibu wa sheria na ana haki lakini ukisikiliza kwa masikio ya serikali ambayo inamasikio 20 utabaini kwamba watu hao wako pale wakijua wazi kwamba wamevamia eneo lile,” ameeleza.

Amesema serikali haiwezi kuendesha taifa kwa kusikiliza taarifa za mtu ambaye anaamini zinafaa bali wanafuata taratibu, sheria, kanuni na miongozo ya nchi kupitia katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Nimesema na narudia tena kusema hapa kwamba Watanzania wote wanapaswa kufuata sheria za ardhi wanapofanya jambo lolote la kuendesha shughuli  za kiuchumi na kijamii  kwenye  ardhi,” amesisitiza.

Hata hivyo, amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, CPA Amos Makalla, viongozi na watendaji wa sekta ya ardhi mkoani humo kwa kuwapa  wananchi elimu  ya sheria ya ardhi.

Aidha, Waziri Silaa amewataka watumishi wa sekta ya ardhi kuhakikisha wanasimamia  sheria za ardhi  na wahakikishe wanatenga muda wa kutoa elimu kwa viongozi wa ngazi za kata. Vijiji, vitongoji na mitaa ili nao wawe na  uelewa kuhusu sekta hiyo  waweze kuwafikishia  elimu hiyo wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles