31.2 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

Walioua albino mwaka 2009 wahukumiwa kunyongwa

NA JUDITH NYANGE, MWANZA
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Mwanza imewahukumu kunyongwa washtakiwa watatu wa kesi ya mauaji ya Jesca Charles (25) mwenye albino, mkazi wa Igoma Kishiri wilayani Nyamagana, Mkoa wa Mwanza.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Jaji Agnes Bukuku baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na pande zote mbili.
Washtakiwa hao ni Melikiadi Christopher (33) mkazi wa Igoma Kishiri, Yohana Kabadi (52) maarufu kama Mwanamalundi mkazi wa Igoma na Regina Mashauri (43) kutoka Mwisenya Igoma wilayani Nyamagana.
Jaji Bukuku alisema washtakiwa walifanya mauaji hayo Juni 21, 2009 eneo la Igoma Kishiri wilayani Nyamagana mkoani Mwanza.
“Mimi ninaamini binadamu wote tuna haki ya kuishi na wote tunaamini kuwa tutakufa, lakini siyo kwa kuua albino,” alisema Jaji Bakuku.
Alisema vitendo hivyo ni vya kinyama, hivyo ni lazima vikomeshwe kwa kutolewa kwa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wote.
Awali Jaji Bukuku aliieleza mahakama hiyo kuwa kuna baadhi ya watu wanaowatumia vijana kutekeleza vitendo vya uhalifu kwa kuwaahidi dau kubwa la fedha.
“Vijana hawa waliahidiwa dau la Sh milioni 800 ingawa hawakuwahi kukutana wala kuona mtu anayenunua viungo hivyo,” alisema.
Jaji Bukuku alimtaja mshtakiwa Regina kuwa ndiye alikuwa akitafuta masoko kwa ajili ya kuuza viungo hivyo na kukitaja kitendo hicho cha kujipatia utajiri kwa kutumia viungo vya albino kuwa cha kinyama na kinapaswa kukumewa vikali.
Kesi hiyo ilisimamiwa na Wakili Mkuu, Pendo Makondo kwa kushirikiana na mawakili wa Serikali waandamizi, Paschal Mrungu na Castus Ndamgoba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles