24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

WALIOTUHUMIWA KUKUSANYA MATOKEO YA UCHAGUZI MKUU WAACHIWA HURU

Na Kulwa Mzee-Dar es Salaam


pg-1

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaachia huru wafuasi watano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliokuwa wakituhumiwa  kukusanya na kusambaza matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa urais, ubunge na udiwani mwaka jana.

Wafuasi hao waliachiwa huru jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicious Mwijage baada ya upande wa Jamhuri kuomba kufanya hivyo.

Wakili wa Serikali, Elia Athanas alidai   kwamba kesi ilikuwa kwa ajili ya kuanza kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka lakini badala yake Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) aliwasilisha hati kuonyesha kwamba hana haja ya kuendelea na kesi hiyo hivyo aliomba iondolewe.

Alidai DPP aliomba kesi hiyo iondolewe kwa mujibu wa kifungu cha sheria namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Mahakama iliridhia maombi hayo na kuwaachia huru washtakiwa.

Washtakiwa hao ni pamoja na Mashinda Mtei, Julius Fredrick. Eddie Fussi, Meshack Mlawa na Anisa Rulanyaga.

Mbali na wanachama hao wa Chadema, washtakiwa wengine waliopandishwa kizimbani hapo kwa mashtaka hayo ni Julius Matei (raia wa Kenya), Jose Mavinga Nimi ambaye kwa sasa ni marehemu (raia wa Angola) na Kim Hyunwook (raia wa Korea).

Kwa pamoja wanadaiwa kutenda makosa hayo kinyume cha kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Uhalifu wa Mtandao namba 14 ya mwaka 2015.

Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza  Oktoba  27, 2015  na kusomewa mashtaka ya makosa ya uhalifu wa kimtandao, wakidaiwa kukusanya na kusambaza matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa urais, ubunge na udiwani, uliofanyika Jumapili  ya Oktoba 25, 2015.

Kwa pamoja wanadaiwa kati ya Oktoba 25 na 26, 2015 kwenye  maeneo tofauti   Dar es Salaam, walichapisha matokeo ya uchaguzi wa urais wa mwaka 2015 yasiyo sahihi na ambayo hayakudhibitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Ilidaiwa lengo lilikuwa ni kuipotosha jamii kuhusu matokeo ya uchaguzi yaliyokuwa yanaendelea kutolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Walidaiwa kuwa siku hiyo ya tukio, walichapisha na kusambaza matokeo hayo kupitia Mfumo wa Uratibu wa Uchaguzi uitwao M4C Election Results Management na kupitia mitandao mingine ya  jamii kama vile Facebook na Twitter.

Washtakiwa Matei, Mavinga  na  Hyunwook walidaiwa kujihusisha na ajira nchini bila ya  kuwa na kibali, kinyume cha Sheria ya Uhamiaji.  Wanadaiwa kuwa Oktoba 26, 2015 katika Hoteli ya King D  wilayani Kinondoni,  Dar es Salaam, washtakiwa hao ambao ni wageni, walijihusisha katika ajira ya kukusanya na kusambaza matokeo ya uchaguzi wa urais nchini, kwa Chadema, bila kibali.

Pia wageni hao walidaiwa kujihusisha na shughuli za biashara nchini kwa  niaba ya Wanama Saccos, bila  ya kuwa na kibali,  kinyume cha Sheria ya Uhamiaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles