27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

TWAWEZA: ASILIMIA 80 YA WATANZANIA WANATAKA BUNGE LIONYESHWE ‘LIVE’

Na LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM


 

aidan-eyakuzeUTAFITI wa taasisi ya Twaweza, unaonyesha asilimia 65 ya wananchi wanapenda vyombo vya habari vitoe taarifa za mambo maovu yanayofanywa na watumishi wa Serikali vikiwamo vitendo vya rushwa.

Hata hivyo,  asilimia 31 wamesema utoaji wa taarifa hizo utaliathiri Taifa.

Twaweza imefanya utafiti huo kwa ushirikiano na Shirika la Afrobarometer   kutathimini utawala wa demokrasia,uhuru wa upatikanaji wa habari na kusimamishwa   matangazo ya moja kwa moja ya Bunge.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mtendaji Mkuu wa Twaweza, Aidan Eyakuze alisema wananchi wanane kati ya 10   (asimilia 75), walisema vyombo vya habari vinafanya kazi nzuri ya kufichua maovu na rushwa huku wananchi wawili kati ya 10 (asilimia 18), wakisema havifanyi kazi nzuri.

“Kwa upande wa uhuru wa kutangaza habari, asilimia 53 wanasema vyombo vya habari viwe huru kutangaza habari yoyote huku asilimia 44 wakisema Serikali iwe na mamlaka ya kufungia magazeti.

“Asilimia 65 wanasema vyombo vya habari havijawahi au kama vimewahi, ni mara chache vimekuwa vikitumia vibaya uhuru wake kwa kutangaza vitu ambavyo si vya kweli,” alisema Eyakuze.

Alisema wananchi wanaunga mkono kwa kiasi kikubwa uhuru wa kutoa maoni na kupata taarifa ambako asilimia 95 ya wananchi waliohojiwa walisema wanapenda wananchi wawe huru kuikosoa Serikali  inapokosea.

“Wananchi pia wanaunga mkono demokrasia.Takwimu za sauti za wananchi za hivi karibuni zinaonyesha asilimia 69 walichagua demokrasia kuliko aina nyingine ya serikali.

“Uungaji mkono huu wa demokrasia pia unadhihirika kupitia takwimu za Afrobarometer (2014), zinazoonyesha asilimia 79 ya wananchi walisema Serikari inayoongoza kwa demokrasia ndiyo aina ya serikali wanayoipenda zaidi na asilimia 81 wakisema ni vema wachague viongozi wao kupitia uchaguzi huru wa demokrasia,” alisema.

Utafiti huo pia unaonyesha asilimia 77 ya wananchi wanataka wawe na uwezo wa kupata taarifa zinazoshikiliwa na mamlaka za umma, huku asilimia 23 wakisema ni wale tu wanaofanya kazi kwenye mamlaka za umma ndiyo waruhusiwe kupata taarifa hizo.

Kuhusu Bunge kuonyesha ‘live’, asilimia 92 ya wananchi waliohusika walitaka vipindi vya Bunge kurushwa moja kwa moja kupitia luninga na redio na asilimia 79 wanapinga uamuzi wa Serikali ya kusimamisha matangazo hayo.

“Asilimia 88 wanasema Bunge lirushwe moja kwa moja bila kujali gharama. Asilimia 12 wanasema wanadhani suala la kubana matumizi ni sababu nzuri ya kutokurusha vipindi ya Bunge moja kwa moja,” alisema Mkurugenzi huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles