WALIOKOPA KCBL WATAKIWA KULIPA MADENI YAO

0
812

Na UPENDO MOSHA-MOSHI

SERIKALI mkoani Kilimanjaro imesema itahakikisha watu wote waliokopeshwa fedha zaidi ya Sh bilioni 4 katika Benki ya Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro (KCBL) na kushindwa kuzilipa, wanachukuliwa hatua.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, alipokuwa akizungumza katika mkutano mkuu maalumu wa benki hiyo, uliofanyika mjini Moshi.

Kwa mujibu wa Mghwira, madeni yote ya Benki ya KCBL ya zaidi ya Sh bilioni 4 yatafuatiliwa ili wakopaji waweze kuyalipa kwa haraka.

“Katika suala hilo, Serikali haitasita kuwachukulia hatua za kisheria wadaiwa wote wanaodaiwa na benki hiyo na tutahakikisha madeni hayo yanalipwa kwa haraka ili fedha zitakazolipwa ziingizwe kwenye mtaji wa KCBL moja kwa moja.

“Najua kuna zaidi ya shilingi bilioni nne zipo katika mikono ya watu, sasa nasema Serikali itawafuatilia wadaiwa wote waliokopa fedha hizo na kushindwa kuzirejesha kwa wakati na wakishindwa basi sheria ipo wazi tutafanya maamuzi mengine.

“Kutokana na ubadhirifu wa mali za ushirika uliokuwa umefanyika huko nyuma, kuna fedha zilizofuatiliwa na Serikali zilirudishwa.

“Kwa hiyo, ninaiomba Bodi ya KNCU kuangalia uwezekano wa kuwekeza sehemu ya fedha hizo kuwa sehemu ya mtaji kwenye benki ya KCBL,” alifafanua.

Aidha, Mghwira aliwaomba wafanyabiashara na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya mkoa huo kujitokeza kwa wingi ili kuja kununua hisa za KCBL kwa kuwa sasa benki hiyo inajiendesha kwa muundo mpya.

Awali, akizungumza wakati akitoa taarifa ya benki hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya KCBL, Reginald Hoseah, alisema hadi Julai 31, mwaka huu, mtaji wa benki hiyo ulivuka lengo lililowekwa la Sh bilioni 5 hadi kufikia jumla ya Sh bilioni 5.2.

Wakati huo huo, wajumbe wa Benki ya KCBL waliridhia kubadilishwa kwa muundo wa uendeshaji wa benki hiyo kutoka chama kikuu cha ushirika na kuwa kampuni.

Mwisho.

Msukuma aahidi kuwapelekea wananchi umeme

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here