23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

WALIMU WATAKIWA KUZINGATIA ADHABU YA VIBOKO

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


WALIMU na bodi za shule wametakiwa kuzingatia taratibu na kanuni katika kutekeleza adhabu ya uchapaji viboko shuleni ili kuepuka kuwasababishia madhara watoto.

Waraka wa Elimu wa mwaka 2002 unaozungumzia utoaji adhabu ya viboko shuleni, unaonesha makosa ambayo yanafaa viboko na unafafanua kuwa mkuu wa shule ndiye anayetakiwa kutoa adhabu hiyo au kwa kuchagua mwalimu.

Akizungumza juzi wakati wa mahafali ya 10 ya Taasisi ya Elimu ya Ebonite, Ofisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Hamis Lissu, alisema waraka huo ni mgumu kuutekeleza, hivyo aliwataka walimu kuusoma kwa makini na kuuzingatia.

“Viboko havijapigwa marufuku bali vimewekewa utaratibu maalumu na msipozingatia mtoto akipata matatizo, mwalimu utaadhibiwa kwa ule waraka. Hivyo, angalieni msije mkaanza kazi leo halafu kesho mnafukuzwa kwa kutouzingatia,” alisema Lissu.

Kwa mujibu wa ofisa huyo, mwanafunzi husika kabla hajaadhibiwa ni lazima apimwe afya na kwa wasichana wanatakiwa wachapwe mikononi na wavulana kwenye makalio na viboko visizidi vinne.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi hiyo, Thadeus Njuu, aliwataka wahitimu hao kuwapenda wanafunzi wa jinsia zote bila ubaguzi na kuondoa ujinga walio nao kwa kuwapa ujuzi na maarifa wanayohitaji.

“Watoto wanastahili kupendwa, tusipowapenda ukatili tutakaowafanyia watadhani kuwa huo ndio mtindo wa maisha na tutajenga Taifa la watu wakatili,” alisema Njuu.

Awali Mkuu wa Chuo cha Ualimu cha Ebonite, Mwinjuma Mirambo, aliiomba Serikali kuangalia upya sifa za kujiunga na vyuo vya ualimu, kwani ziko juu na kusababisha vyuo binafsi kukosa wanafunzi.

“Tunapendekeza sifa za kujiunga na vyuo vya ualimu zianzie daraja la kwanza hadi la nne lenye alama 27, kwa sababu hizi za sasa zimesababisha tushindwe kujiendesha na vyuo vingine vimefungwa,” alisema Mirambo.

Alisema mipango yao ya baadaye ni kuanzisha shule ya sekondari, kituo cha lugha za Kiswahili, Kiingereza na Kichina na kutengeneza chumba maalumu cha zana za kufundishia na kujifunzia.

Katika mahafali hayo, wahitimu 28 walitunukiwa vyeti vya Daraja la 111 A na wahitimu 86 walitunukiwa vyeti vya elimu ya awali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles