NA NORA DAMIAN, DAR ES SALAAM
CHAMA cha Walimu Tanzania CWT) kimesema madai ya walimu yasiyokuwa ya mishahara ambayo hadi sasa bado hayajalipwa ni zaidi ya Sh bilioni 10.
Wiki iliyopita, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, wakati akizungumza katika kipindi cha Tunatekeleza kinachorushwa na Kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC1), alieleza kuwa katika madai yasiyokuwa ya mishahara hakuna mtumishi ambaye hajalipwa.
Alisema madeni ya walimu yamegawanyika katika sehemu mbili ambazo ni madai yanayotokana na mishahara na yasiyokuwa ya mishahara ambayo yamekuwa yakilipwa na Serikali kupitia wizara yake huku madai ya mishahara yakishughulikiwa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Katibu Mkuu wa CWT, Ezekiah Oluoch alisema walimu waliolipwa madai yasiyokuwa ya mishahara ni wachache na kwamba mengine bado yanaendelea kukusanywa.
“Hatuwezi kwenda namna hii, matamko kama haya, mawaziri wawe wanajiridhisha kwanza. Kama walimu waliosimamia mtihani wa kidato cha nne mwaka jana hadi leo hawajalipwa na waziri anajua yote haya,” alisema Oluoch.
Alisema walimu waliosimamia mtihani huo mwaka jana wanadai zaidi ya Sh bilioni nne.
Chama hicho kimepanga kukutana na timu iliyoundwa kushughulikia madeni ya walimu kufanya tathmini kujua madeni yaliyolipwa na yale ambayo bado walimu wanadai.
Alisema mara ya mwisho walikutana Aprili 19, mwaka huu, ambako Serikali iliomba kupewa muda wa miezi minne na walipanga kukutana tena mwezi uliopita lakini hadi sasa hawajakutana.
“Tunasubiri ni lini tutakutana nao watupe majibu kuhusu madeni ya walimu. Mwezi huu tuna kikao cha baraza na mojawapo kati ya taarifa tunayotakiwa kuiwasilisha ni hii ya madeni…kazi yetu ni kupeleka kwenye vikao vya chama ndivyo vitakavyotupa mwongozo,” alisema.
Wakati huohuo, CWT kimesema wiki iliyopita kiliwasilisha Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) madeni ya walimu 988 wa Mkoa wa Songwe ambayo ni karibu Sh bilioni moja.
Wilaya za mkoa huo na madeni ya walimu katika mabano ni Ileje (Sh milioni 400), Mbozi ( Sh milioni 400) na Momba (Sh milioni 140).