KULWA MZEE-DAR ES SALAAM
WAKAZI wawili wa Chanika Kwa Zoo, Dar es Salaam, wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kukutwa na vipande 47 vya meno ya tembo vyenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni moja.
Washtakiwa hao, Abdallah Hamis (30) na Adam Kawà mbwa (35), walipanda kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi, Augustino Rwezile.
Wakili wa Serikali, Candid Nasua alidai washtakiwa walitenda makosa hayo Februari 11, mwaka huu eneo la Chanika Kwa Zoo, Ilala Dar es Salaam.
Alidai kuwa katika shtaka la kwanza, washtakiwa hao walikutwa wakimiliki vipande 47 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh 1,081,357,500 mali ya Serikali bila kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyama Pori nchini.
Ilidaiwa kwamba katika shtaka la pili washtakiwa walitakatisha fedha hizo wakati wakijua zimetokana na kosa la ujangili.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa hawakutakiwa kujibu lolote kwakuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
Wakili Nasua alidai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na kesi iliahirishwa hadi Machi 25, mwaka huu itakapotajwa.