WAKULIMA WATAKIWA KULIMA KIBIASHARA

0
989

Na LILIAN JUSTICE-KILOSA

WAKULIMA ametakiwa kulima kilimo cha kibiashara ili waweze kupata mafanikio zaidi.

Ushauri huo umetolewa juzi na Ofisa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro, Furahia Mark, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wakulima.

“Wakulima wanatakiwa kwenda na wakati kwa kupanga mkakati wa kilimo wa muda mrefu na mfupi wenye malengo ya kujipatia mazao bora yenye kuleta tija kwa Taifa.

“Kwa hiyo, nawashauri wakulima waondokane na utamaduni wa kulima kienyeji, kwani wakilima kibiashara watanufaika zaidi kupitia kilimo hicho.

“Sisi kama wataalamu wa kilimo, lengo letu ni kuongeza uzalishaji katika eneo analolima mkulima,” alisema Mark.

Naye Mkuu wa Shirika la ICRAF Tanzania, Dk. Anthony Kimaro, alisema mpaka sasa mradi huo umeweza kuwafikia wakulima mbalimbali katika wilaya kumi.

Pia, alisema malengo ya mradi huo ni kueneza kilimo bora kwa kuwaelimisha wakulima mbinu bora za kilimo, uhifadhi wa nafaka, lishe na kurutubisha udongo.

“Sisi kama ICRAF Tanzania tumeweza kufanikisha mradi huo kutokana na ushirikiano uliopo baina ya mashirika rafiki yanayotaka kuwaendeleza wakulima,” alisema.

Kwa upande wake, Mratibu wa Shirika la ICRAF Tanzania, Elvis Jonas, alisema tangu kuanza kwa mradi huo miaka minne iliyopita, wakulima wamenufaika na mazao yao kutokana na kutumia mbegu bora na mbolea za viwandani ambazo zimekuwa chachu ya mafanikio yao katika kilimo.

Wakati hao wakisema hayo, Ofisa Kilimo, Kata ya Kimamba A, Elisha Kingu, alisema mara kwa mara amekuwa akiwaeleza wakulima namna ya upandaji wa mazao ili waongeze uzalishaji.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here