MANNY PACQUIAO AKUBALI KIPIGO

0
485

BRISBANE, AUSTRALIA

BINGWA wa ngumi uzito wa juu duniani, Manny Pacquiao, raia wa Ufilipino, amekubali kichapo kutoka kwa mpinzani wake, Jeff Horn wa nchini Australia, kwenye ukumbi wa Suncorp Stadium, mjini Brisbane jana.

Katika pambano hilo, Pacquiao alikuwa anatetea ubingwa wa WBO, likiwa la raundi 12, lakini bingwa huyo alishindwa kuonesha uwezo wake na kuwapa mashabiki wasiwasi kwa kipindi kijacho.

Mashabiki wengi kutoka nchini Ufilipino walijitokeza kwa wingi, huku wakiamini bingwa wao anaweza kufanya maajabu mbele ya watazamaji 50,000 ambao walijitokeza kushuhudia pambano hilo.

Ushindani ulikuwa wa hali ya juu, ambapo kila mmoja alikuwa anafanya shambulizi la kushtukiza kwa mpinzani wake na hatimaye Pacquiao akikubali kupoteza mchezo huo kwa pointi 117-111, 115-113, 115-113.

Katika pambano hilo, kila mmoja aliweza kumtoa damu mwenzake, kutokana na kushambuliana. Jeff Horn, mwenye umri wa miaka 29, aliweza kuonesha kuwa na damu changa dhidi ya Pacquiao, mwenye umri wa miaka 38.

“Katika maisha yangu sikuwahi kufikiria kama nitakuja kupigana na bingwa kama Pacquiao na nikaweza kushinda, lakini tayari nimeweka historia mpya na kutwaa ubingwa wa WBO mbele ya bingwa huyo.

“Ninayo furaha kubwa kuwa bingwa, ninaamini historia hii inaweza kunisaidia kwenye mapambano yangu yajayo,” alisema Horn.

Kipigo hicho cha Pacquiao kinaweza kumfanya bingwa huyo kuwa ni mwisho wake wa ngumi, kwa kuwa uwezo wake unazidi kupungua siku hadi siku, kwa mujibu wa mwalimu wake, Freddie Roach.

“Pambano lilikuwa gumu sana, wala sikutegemea kama ningeweza kukutana na ushindani wa aina hiyo, lakini natakiwa kukubaliana na matokeo, kwa kuwa ni sehemu ya pambano na hayo yalikuwa matokeo kutoka kwa majaji, natakiwa kuheshimu na kukubaliana nao.

“Nampongeza mpinzani wangu kwa kuibuka na ushindi, nadhani alikuwa na maandalizi mazuri na ndiyo maana amefanikiwa kushinda,” alisema Pacquiao.

Uwezo wa Pacquiao ulionekana kushuka tangu alipochezea kichapo dhidi ya bingwa Floyd Mayweather, Mei mwaka 2015, hata hivyo, mabondia hao walitangaza kustaafu mchezo huo, huku Paquiao akidai kuwa, anataka kutumikia jamii katika mambo ya kisiasa, wakati huo Mayweather akidai muda wake umefika.

Hata hivyo, Mayweather alirudi tena ulingoni na Agosti 26 mwaka huu anatarajia kurudi tena uwanjani dhidi ya mpinzani wake, Conor McGregor, pambano ambalo linadaiwa kuwa la kihistoria.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here