25.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 1, 2024

Contact us: [email protected]

Wakili azibana kampuni za simu vifurushi muda wa maongezi, bando

FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM

WAKILI wa kujitegemea, Bashir Yakub, ambaye amechapisha barua ya wazi mtandaoni aliyoiita, ‘mashtaka kwa kampuni nne za simu’, akipinga kuisha kwa muda wa vifurushi vya muda wa maongezi na bando vinavyowekwa kwenye simu ameliambia gazeti hili kuwa mapambano bado ni makubwa katika kufanikisha azma yake hiyo.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi jana Dar es Salaam, Yakub, alisema ameamua kufanya hivyo baada ya kudai kuona haki za Watanzania kwenye nyanja ya mawasiliano zinasiginwa bila kujua.

Katika andiko lake hilo lenye hoja tano alisema kuwa anataka kuzishtaki kampuni  hizo za mawasiliano ya simu za mkononi kwa kuwanyang’anya wateja kitu ambacho wamekilipia.

Alisema tayari ameziandikia barua kampuni nne za mawasiliano ambazo ni, Tigo, Airtel, Vodacom na Halotel akizitaka kufanya mabadiliko juu ya utaratibu huo wa kuisha kwa vifurushi na kwamba anangoja majibu ndani ya simu 30 vinginevyo atakwenda mahakamani.

“Sheria inavyotaka, inaelekeza kuziandikia kampuni husika, na kuwapa siku 30, huku ukitaka kufanyika kwa mabadiliko juu ya jambo husika, na iwapo muda huo utapita bila mafanikio, basi lazima uende ngazi husika.

“Licha ya kwamba nina wiki moja tangu nimeandika, lakini bado sioni mwanga kwa kampuni hizo kufanya hivyo kwa kuwa eneo hilo ndilo linalotumiwa kuvuna fedha kwa wateja, hivyo muda huo ukipita bila mafanikio nitaenda ngazi nyingine ambayo ni kamati za TCRA, japo ikumbukwe kuwa kitendo cha kuanza kuandika barua kwa kampuni husika tayari unakuwa umeanza mchakato wa kesi,” alisema.

Alifafanua kuwa nchi nyingi tayari zimeachana na mfumo huo badala yake mteja ana haki ya kutumia kifurushi chake hadi pale kitakapoisha bila kusitishwa na kampuni.

“Hizi ni haki ambazo wananchi wa nchi nyingi wameanza kuzipata kwa muda mrefu, mfano Afrika Kusini kupitia mamlaka yao ya mawasiliano walitunga kanuni ya kuhakikisha kuwa vifurushi haviishi muda wake hadi pale mtu atakapotumia huduma yake na kuisha, jambo ambalo liliungwa mkono na Ghana kupitia mamlaka yao ya mawasiliano.

“Lakini pia Kenya nao baada ya kuona hivyo waliiga, lakini baada ya mamlaka yao ya mawasiliano kukataa, raia wakaenda mahakamani hadi sasa kesi hiyo ipo mahakamani, lakini hapa kwetu tumesubiri muda mrefu kuona labda Baraza la Ushauri la Watumiaji Huduma za Mawasiliano (TCRA-CCC) labda na sisi tutakuja na kitu kama hiki bila mafanikio, hivyo nikaona njia rahisi na bora ya kuweza kuwasukuma watu hawa kwenda kwenye vyombo vya sheria ambako ndiko haki iliko.

“Nimebaini kuwa watanzania wengi walikuwa wamechoka lakini hawakuwa na sehemu ya kusemea…naamini tutapata ushindi, nimejiandaa kwa muda mrefu kwani najua vita haitakuwa nyepesi,” alisema Yakub.

Mambo yanayombwa

Katika mashitaka yake wakili  huyo anaomba mambo matano la kwanza, vifurushi vyote havipaswi kuisha muda, kitu pekee ambacho kinapaswa kumaliza kifurushi inatakiwa iwe ni mteja  kuongea hadi dakika zako ziishe.

“Kwani, siyo haki kukata kifurushi cha mtu ambaye dakika zake za kuongea, za data, au Sms bado zipo kwa kigezo cha kuisha muda wake wa siku, wiki au mwezi.

Alisema mitandao hiyo inapaswa kuiga mfano kama ilivyo kwa Shirika la Umeme nchini Tanesco kwenye manunuzi ya  LUKU.

“Tanesco akishakuuzia umeme/units ukamlipa basi hatma ya units zako ni utumie mpaka umalize, hawezi kuikata na kujirudishia kwasababu anajua alikuuzia bidhaa na wewe ukamlipa na hivyo una haki ya kutumia bidhaa yako mpaka umalize, hii ndiyo haki. 

“Kinachofanywa na kampuni za simu ni sawa ununue mkate dukani na mwenye duka umlipe hela yake yote, halafu mwenye duka huyohuyo akwambie kwamba usipokula mkate huo kufikia saa 12 za jioni au ndani wiki au mwezi nitakuja tena kuuchukua nyumbani kwako, na aje kweli auchukue iwe mali yake tena kwa mara ya pili,” alisema.

Mbali na hilo, mambo mengine anayoyalalamikia ni haki ya kutochanganyiwa kifurushi na muda wa kawaida wa maongezi bila ridhaa.

“Nitatoa mfano, unakuta mtu ameweka shilingi 1,000 kwenye simu ambapo anajiunga 500 na 500 inabaki kama muda wa maongezi wa kawaida. Wakati anapokuwa akizungumza au akitumia data kupitia ule muda aliojiunga na ukaisha basi simu haikatiki bali inaunganisha moja kwa moja na ile 500 ya muda wa maongezi wa kawaida ambayo alikuwa hajajiunga, hii siyo sawa hata kidogo.

Jambo la tatu ni haki ya kujua matumizi ya kifurushi, alisema malalamiko ya vifurushi vya watu kuliwa isivyo kawaida ni mengi mno. 

“Mfano, unanunua dakika 20 unaongea 10 unaambiwa kifurushi kimeisha, unabaki kushangaa, ni lazima waweke mfumo wenye kutoa taarifa sahihi na za wazi, ili kumwezesha mtumiaji kumonita matumizi ya kifurushi chake,” alisema.

Jambo lingine ni haki ya kuhamisha kifurushi, kwa kile alichosema kuwa kifurushi ni mali ya mteja hivyo anao uhuru wa kukihamisha.

 “Lakini jambo la tano ni, haki ya kupewa tahadhari kuhusu kifurushi au muda wa hewani unapokaribia kuisha, kuna kampuni wana huduma hii lakini wanaitoa kwa hiari sana na wengine wameacha kabisa,  wengine wanatoa tahadhari muda unapoisha na sio unapokaribia.,” alisema.

SHERIA 

Alisema mambo hayo kwa ujumla wake ni kinyume na Katiba ya nchi Ibara ya 18(c) inayotaka uwepo wa mawasiliano bila kuingiliwa.

“Lakini pia yanakiuka kanuni za kielektroniki na mawasilano ya Posta kuhusu viwango vya Tozo GN. No 22/2018 hasa Kanuni ya 4 ( 1 na 2) inayotaka viwango vyote vya tozo za simu kuwa vya haki na kadri.

“Yanakiuka Kanuni ya 4 ya Kanuni za Kielektroniki na Mawasiliano ya Posta GN No.61/2018 kuhusu kumlinda mlaji inayotaka mlaji kupewa taarifa kwa usahihi ya matumizi ya huduma muda wote, yanakiuka Sheria ya Ushindani namba 8/2003 inayotaka mtoa huduma kutoa huduma kwa kuzingatia zaidi maslahi ya watu wa hali ya chini, na sheria nyingine nyingi zimekiukwa,” alisema Yakob.

Kampuni za Simu

Akizungumzia suala hilo, Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania,Jackson Mbando alisema kuwa hana  maoni.

 “Sina ‘comment’ kwa sasa,” alisema Mbando kwa kifupi na kisha akakata simu.

Naye, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Halotel, Mhina Semwenda, alisema kuwa anaomba atafutwe baadae ili aweze kulizungumzia.

“Kwenye hilo hebu naomba unitafute baada ya dakika 30,” alisema Semwenda, ambaye hata hivyo alipotafutwa baadaye simu yake ilikuwa ikiita tu bila kupokelewa.

Kwa upande wake, Meneja Mahusiano wa kampuni ya Vodacom Tanzania, Alex Bitekeye, alisema kuwa atumiwe barua pepe akiahidi kuijibu jana hiyo hiyo, ambayo hata hivyo haikujibiwa.

TCRA,  CCC

Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina gazetini, mmoja wa wafanyakazi wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano, alisema kuwa ujumbe huo hata yeye ameuona na kwamba una hoja za msingi.

“Jambo hilo ni kweli ni la msingi kwani, suala lolote linalohu maslahi ya watumiaji huwa tunalifikisha kwa wahusika ambao ni TCRA, hivyo wazo lake hilo ni zuri na linapaswa kufanyiwa kazi, hivyo kazi yetu ni kuwasilisha mapendekezo kwa TCRA kwa lengo la kuwasaidia wananchi ambao ndiyo wanufaika.

TCRA

MTANZANIA Jumamosi liliwasiliana na TCRAambao walilielekeza gazeti hili kuandika barua kwa Mkurugeni Mkuu wa Mamlaka hiyo, Mhandisi James Kilaba.

Haki ya Mteja wa Mawasiliano

Kwa mujibu wa TCRA haki za Mteja wa Mawasiliano ni pamoja na  kupata huduma bora, kupewa taarifa kuhusu huduma au bidhaa, kutobaguliwa na kulalamika.

Haki nyingine ni, kutatuliwa malalamiko yake, kuhakikishiwa usalama wa bidhaa au huduma, kuwa na faragha na usiri katika matumizi yake, kuelimishwa, kupewa taarifa kabla ya kusimamisha au kikatisha huduma pia kukata rufaa endapo haridhishwi na maamuzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles