30 C
Dar es Salaam
Monday, September 27, 2021

Wakili aeleza watuhumiwa dawa za kulevya walivyokamaywa kimafia

NA KULWA MZEE -DAR ES SALAAM

KESI ya kusafirisha dawa za kulevya inayomkabili Abdul Nsembo na Mkewe Shamim Mwasha, iko mbioni kuhamia Mahakama Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi baada ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya mashahidi.

Washtakiwa walisomewa maelezo ya mashahidi jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Godfrey Isaya ili kesi yao iweze kuhamishiwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kusomwa maelezo ya mashahidi na alidai upande wa Jamhuri una mashahidi 12.

Kabla ya kuanza kusoma maelezo ya mashahidi Wankyo alisoma kwanza vielelezo vilivyomo katika taarifa hiyo ya maelezo ya mashahidi.

Vielelezo hivyo vilikuwa ni maelezo ya onyo kwa watuhumiwa wote wawili, hati ya ukamataji, ripoti ya uchunguzi wa maabara ya Serikali, fomu ya kuwasilisha sampuli maabara, taarifa ya usajili wa gari kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na bahasha zilizokuwa na dawa za kulevya.

Akisoma maelezo ya shahidi wa kwanza Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Paschal Daudi, ambaye ndiye alikuwa kiongozi wa upekuzi siku washtakiwa walipokaguliwa na kukamatwa, alidai Mei mosi 2019, alipewa kazi ya kuongoza ukaguzi katika nyumba ya mfanyabiashara Abdul Nsembo iliyopo Mbezi Beach Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Alidai kwa mujibu wa maelezo ya Daudi walifika eneo la tukio saa 2 usiku na kugonga geti ambalo lilifunguliwa na mlinzi aliyejitambulisha kwa jina la Bakari Senkokwa na baada ya kujitambulisha na kumueleza kilichowapeleka Senkokwa aliwaeleza wasubiri amuite mwenye nyumba ambaye ndiye mwenye ufunguo.

Kwa mujibu wa maelezo hayo baada ya muda mfupi alitoka mama ambaye alijitambulisha kwa jina la Shamim Mwasha ambaye alikiri kuwa ndiye mama mwenye nyumba na mke wa Nsembo.

Inadaiwa Shamim alipoulizwa kuhusu mume wake alisema hakuwa anajua aliko kwani walikuwa na ugonvi wa kifamilia na hajui angerudi muda gani lakini wao walimuomba awaruhusu wafanye ukaguzi naye akawaruhusu.

Kabla ya ukaguzi walimruhusu Shamim awakague ambapo alifanya hivyo na kujiridhisha kwamba hawakuwa wamebeba kitu chochote hatarishi kwake.

Walipotakiwa ukaguzi katika maeneo kadhaa hawakufanikiwa kupata chochote wala kumuona yeyote hadi walipoingia katika moja ya chumba na kukuta vipande vya Gypsum vikiwa vimeanguka na alama ya mguu ikionesha kuwa kuna mtu alipanda darini muda mfupi uliopita.

Alidai alimwagiza mmoja wa askari alioongozana nao aliyemtambulisha kwa jina la Brown apande darini kuangalia kama kuna mtu lakini hakuona mtu, baada ya kurudi mara ya pili aligundua kulikuwa na mfuniko unaotokea upande wa nje kwa kupitia kwenye paa hivyo aliufunua na kutoka nje kwenye kibaraza cha kuwekea tanki la maji ambalo Nsembo alikuwa amejificha nyuma yake.

Simon alisema maelezo hayo yaliendelea kudai kuwa Brown alimshusha Nsembo chini na kuendelea na upekuzi ambapo walifanikiwa kukamata vitu kadhaa ikiwemo pasi ya kusafiria, cheti cha kuzaliwa cha Nsembo, vifaa vya mawasiliano kama simu, kifaa cha kuhifadhia picha za CCTV, na kifaa cha kuhifadhia nyaraka za kompyuta (external backup).

Mbali na vifaa hivyo walikuta pia vikopo vinne vyenye unga ambao baadaye ulibainika kuwa ni dawa za kulevya na waliendelea na upekuzi katika magari ambapo katika gari moja aina ya Landrover Discovery lenye namba T 817 BQN nyuma ya kiti walikuta mfuko wa kitambaa uliowekwa kwenye mfuko laini wenye unga ambao baadaye ulibainika kuwa ni dawa za kulevya.

Alidai waliweka kumbukumbu ya vielelezo vyote na katika fomu maalumu na kuwekalwa saini na wahusika wote wakiwemo washtakiwa.

Maelezo hayo pia yalithibitishwa na maelezo ya mashahidi wegine 11 waliobaki ambao maelezo yao yalishabihiana na maelezo ya Paschal.

Baada ya kusikiliza maelezo hayo hakimu Issaya alisema wataandaa taarifa kwa ajili ya kupeleka kesi Mahakama Kuu na itaangwa tarehe ya kusikilizwa kesi hiyo katika Mahakama Kuu.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,348FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles