30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Hukumu ya Zitto Mei 29, Mahaka yatoa hati akamatwe

NA KULWA MZEE -DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, inatarajia kusoma hukumu ya Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe Mei 29 mwaka huu huku ikitoa hati ya kumkamata kwa kutohudhuria kwenye shauri lake bila taarifa.

Amri hiyo ya kumkamata Zitto ambaye anakabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi, ilitolewa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Hukumu ilipangwa kusomwa MEI 29 mwaka huu, baada ya upande wa mashtaka na utetezi kufunga ushahidi na kuwasilisha majumuisho ya mwisho kwa kuirahisishia mahakama kufikia uamuzi.

 Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka, alidai shauri lilitajwa kwa ajili ya kupanga tarehe ya hukumu ambapo mshtakiwa hakuwepo na hakuna taarifa kuhusu kushindwa kufika kwake mahakamani.

” Mheshimiwa Hakimu mshitakiwa hayupo na muda wa mahakama unafahamika ni saa tatu asubuhi na hakuna taarifa yoyote ingawa mshtakiwa hana tabia ya kushindwa kufika mahakamani,” alidai.

Baada ya kudai hayo, Hakimu Shaidi alisema hati ya kukamatwa itolewa, kesi iliahirishwa hadi Mei 29, mwaka huu kwa ajili ya hukumu.

Katika kesi hiyo upande wa mashitaka uliwasilisha mashahidi 15 na utetezi ulikuwa na mashaidi nane.

Katika kesi hiyo inadaiwa Oktoba 28 mwaka juzi, Zitto  aliitisha mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika ofisi za Makao Makuu ya ACT Wazalendo, akiwa na lengo la kuleta chuki kwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinyume na sheria na kwamba alitoa maneno ya uchochezi dhidi ya Jeshi la Polisi.

Mshtakiwa anadaiwa alitamka kuwa ‘’ watu ambao walikuwa ni majeruhi katika tukio la mapambano baina ya wananchi na polisi wakiwa wamekwenda hospitali kupata matibabu katika kituo cha afya Nguruka, Polisi wakapata taarifa kuwa kuna watu wanne wamekwenda hospitali kituo cha afya Nguruka kupata matibabu wakawafuata kule wakawaua’’

Katika mashtaka ya pili ilidaiwa Oktoba 28, mwaka juzi maeneo ya Kijitonyama katika makao makuu ya chama hicho, jijini Dar es Salaam, alitoa maneno ya uchochezi dhidi ya Jeshi la Polisi akisema ‘’ lakini tumefuatilia kwa kina jambo hili, taarifa ambazo tumezipata kutoka kijijini Mpeta-Nguruka, Uvinza ni mbaya.

“Taarifa ambazo zinaonyesha wananchi wengi sana wameuawa na jeshi la Polisi pamoja na kwamba afande Sirro amekwenda kule, haijatoa taarifa yoyote kuhusu wananchi…kama hawa wanyantuzu walivamia eneo la Ranchi kuna taratibu za kiheria za kuchukua na sio kuwauwa, wananchi wengi sana wamekufa.’’

Ilidaiwa katika tarehe hiyo hiyo, Zitto alitoa maneno ya uchochezi dhidi ya Jeshi la Polisi akisema ‘’tumekuwa tukifuatilia kwa kia yanayojiri yote huko Uvinza tunasikitika kusema kuwa taarifa tunazozipata kutoka Uvinza zinaogofya mno, kwani tunaambiwa kuwa wananchi zaidi ya 100 wa kabila la Wanyantuzu wamepoteza maisha kwa kupigwa risasi na polisi, wengine wakisema kuuawa hata wakiwa kwenye matibabu hospitalini baada ya kujeruhiwa kwenye purukushani na jeshi la polisi…’’

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles