23.8 C
Dar es Salaam
Monday, September 25, 2023

Contact us: [email protected]

Wakala Serikali Mtandao : ERMS mfumo shirikishi kuunganishwa na mingine

RAMADHAN HASSAN

WAKALA wa Serikali Mtandao (eGA) imetengeneza mfumo shirikishi wa kusimamia shughuli na Rasilimali za Taasisi(ERMS) ambao utaunganisha shughuli mbalimbali za Taasisi kuwa katika mfumo mmoja ambao utawezesha usimamizi na kufuatilia kwa ufanisi shughuli zote za taasisi.

Taarifa  hizo zinaweza kuwa za fedha,vifungu vya bajeti na bakaa ya fedha, hali ya matumizi ya fedha, taarifa zinazosaidia katika  upimaji na utendaji kazi wa watumishi  na hivyo kusaidia katika maamuzi sahihi.

Jambo hili ni zuri kwani Taasisi zote shughuli zake  zitakuwa katika Mfumo mmoja na hivyo kuisaidia Serikali katika kuziendesha na katika ukusanyaji wa mapato.

Mtendaji Mkuu wa Wakala huo, Dk.Jabir Bakari akizungumza na Waandishi wa Habari hivi karibuni anasema mfumo huo unaunganisha shughuli mbalimbali za taasisi kuwa katika mfumo mmoja unaowezesha usimamizi, ufuatiliaji, ukaguzi na tathmini ya utekelezaji wa shughuli zote za taasisi kwa ufanisi.

“Tumeamua kutumia utajiri wa utaalamu wetu  wa kidigitali kutengeneza mfumo wa ERMS ambao ni dirisha moja linalounganisha shughuli zote ndani ya taasisi ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na utoaji wa huduma bora kwa umma,”anasema  Dk.Bakari.

Mtendaji Mkuu huyo anasema mfumo huo una moduli 18 zitakazounganisha shughuli mbalimbali za utendaji kazi zitakazotegemeana kuwezesha na kubadilisha taarifa miongoni mwa idara  na kusimamia rasilimali  kama vile watu, fedha na vitendea kazi.

“Mfumo huu pia unawezesha ushughulikiaji  wa miamala kutoka idara moja hadi nyingine kama vile ankara za bidhaa na huduma, mapato  na matumizi, ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi, utekelezaji wa shughuli za ununuzi na utayarishaji wa taarifa mbalimbali za utendaji,”anasema Mtendaji huyo.

Anasema  mfumo huo unawezesha Maafisa Masuuli na watumiaji wengine kupata taarifa mbalimbali  kulingana na mahitaji yao.

Anasema taarifa hizo zinaweza kuwa za fedha, vifungu vya bajeti na bakaa ya fedha, hali ya matumizi ya fedha, taarifa zinazosaidia katika  upimaji na utendaji kazi wa watumishi  na hivyo kusaidia katika maamuzi sahihi.

“ERMS pia inaweza kuunganishwa na kubadilishana taarifa na mifumo mingine mikuu ya Serikali  kama vile mfumo Mkuu wa Uhasibu, mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Rasilimali watu (HCMIS),    mfumo wa malipo ya Serikali Kielektron (GePG), Mfumo wa Barua Pepe Serikalini (GMS) pamoja na mfumo wa Ofisi Mtandao,”anasema.

Anasema Moduli za Mfumo huo zinaweza kuongezwa au kupunguzwa bila kuathiri utendaji kazi  wa Moduli nyingine  au mfumo kwa ujumla.

Dk.Bakari anaielezea mifumo mingine inayotengenezwa na Wakala katika utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao nchini ni pamoja na kuhuishwa kwa iliyokuwa Tovuti ya Serikali  na kuwa Tovuti kuu ya Serikali, www.tanzania.go.tz inayosimamiwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Anaitaja mifumo mingine kuwa ni Tovuti kuu ya ajira,unaosimamiwa na sekretarieti ya ajira, Mfumo wa Barua Pepe Serikalini, unaotumiwa na Taasisi za umma 402 zikiwemo Ofisi za Ubalozi nje ya Nchi kwa ajili ya kubadilishana taarifa Serikalini.

Mtendaji huyo aliitaja Mifumo mingine kuwa ni pamoja na Ofisi Mtandao, ambao unawezesha na kurahisisha shughuli za utawala za kila siku hususani mzunguko wa majalada na nyaraka za ndani ambapo  Taasisi za Umma  52 zinatumia mfumo huo mpaka sasa.

“Mfumo wa Huduma za Serikali kupitia Simu za Mkononi (mGov) ambao ni dirisha moja la huduma Serikali kupitia simu za mkononi,” anasema Dk.Bakari.

Anasema mGov imeunganishwa na watoa huduma wote wakubwa wa simu za mkononi  na unatumiwa na Taasisi za umma 147 mpaka sasa.

Anasema Mfumo mwingine ambao umetengenezwa kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango ni wa Malipo ya Serikali Kielektroni (GePG).

Anasema Mfumo huo unalenga kuongeza udhibiti katika usimamizi wa ukusanyaji mapato Serikalini.

Mtendaji huyo anasema Mfumo huo unatumiwa Taasisi za umma 385, watoa huduma za malipo 17, ambao ni Benki kubwa 12, mifumo ya fedha ya simu za mkononi 5 mpaka sasa.

Pia anasema Mfumo wa e-Vibali unatumiwa na Taasisi 389 katika kuomba na kupata vibali vya kusafiria nje ya Nchi, kwa safari za kikazi na binafsi kwa watumishi wa umma.

Anasema kuna Mfumo wa Ukusanyaji wa Taarifa za Miradi ya Tehama Serikalini(GIP) ambao unatumiwa na Taasisi takribani 77.

“Taasisi 315 zinatumia Mfumo huu na jumla ya matatizo 5,187 yanayohusu Tehama yameshughulikiwa,”anasema.

Mtendaji huyo Mkuu anasema pia kuna Mfumo wa Usimamizi wa Tiketi na Mizigo kielektroni (e tiket and Cargo System) unaotumiwa na Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) na Shirika la Reli Tanzania (TRC).

Dk.Bakari anazishauri  Taasisi za umma kuendelea kutumia Tehama  katika kuboresha utendaji kazi Serikalini na utoaji huduma kwa umma kwa kuzingatia  miongozo na viwango vya serikali.

“Kinachohitajika ni ujuzi stahiki na kujiamini ili kupata matokeo  bora na ya haraka.Wakala utaendelea kutoa ushauri na msaada wa kiufundi katika utekelezaji wa Serikali Mtandao kwa Taasisi za umma,”anasema Dk.Bakari.

Kuhusiana na malalamiko sehemu ambazo zimekuwa zikitumia matumizi ya Tehama kwamba mtandao upo chini, Dk.Bakari anasema changamoto hizo bado zipo lakini Wakala wa Serikali mtandao wanaendelea kuzitatua.

“Tatizo hilo limekuwa likijitokeza lakini tumekuwa tukilitatua mtandao huwa unakuwa chini na ukiwa chini huwezi kufanya jambo lolote, lakini huwa tunajitahidi baada ya muda huduma zinarudi katika ubora wake,”anasema Dk.Bakari.

Nahitimisha kwa kuwataka Wakala wa Huduma Mtandao kusimamia mifumo hii ili iweze kuleta tija hasa katika suala la ukusanyaji wa mapato.

Maana lazima tukubali kutengeneza ni jambo moja na kuisimamia ni jambo lingine angalieni sana hasa hili suala la kutokuwepo kwa Mtandao, huduma nyingine  zimekuwa hazifanyiki kwa kigezo kwamba hakuna mtandao.

Jambo hili limekuwa likiikosesha Serikali mapato wakati kila mmoja anajua kwamba Serikali hii imejikita kuhakikisha inakusanya mapato kwa  njia ya Kieletroniki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,718FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles