Arodia Peter, Dodoma
Somo la haki za binadamu litakuwa sehemu ya lazima na muhimu kwa vyombo vyote vya usalama nchini.
Hayo yamesemwa bungeni leo Mei 14, na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Augustine Mahiga wakati akijibu maswali mbalimbali yanayohusu haki za binadamu.
Amesema suala la haki za binadamu linazingatiwa na Serikali iko mbioni kujenga chuo kitakachokuwa kinatoa mitaala na kufundisha masuala yote ya haki za binadamu.
Dk Mahiga amesema wafadhili wa kujenga chuo hicho wako tayari na wanasubiri uamuzi wa Serikali ya Tanzania.
Katika swali lake la msingi, Mbunge wa Viti Maalum, Dk Sware Samisi pamoja na mambo mengine alitaka kujua katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2015 ni kesi ngapi zilifunguliwa mahakamani kuhusu madhira yanayofanywa na vyombo vya dola dhidi ya raia, na huchukua muda gani kutolewa hukumu, na serikali inafanya kazi gani kuhakikisha wananchi wake pamoja na vyombo vya usalama wanapata elimu ya uraia.