23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

WAFUNGWA MIAKA 30 KWA KULIMA BANGI

Na ELIUD NGONDO-SONGWE


MAHAKAMA ya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, imewahukumu watu wawili kifungo cha miaka 30 jela baada ya kuwakuta na hatia ya kulima bangi katika mashamba yao yenye ukubwa wa hekari tano na robo kinyume cha sheria.

Mwendesha Mashtaka Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Saada Abdul, alisema washtakiwa hao walikamatwa kwa nyakati tofauti kwa makusudi walikutwa wamelima bangi wakiwa wamechanganya kwenye mashamba ya mahindi kinyume cha sheria, huku wakijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Alimtaja mshtakiwa wa kwanza kuwa ni Joel Mwangambaku (41), mkazi wa Kijiji cha Shaji katika Kata ya Mlangali, Wilaya ya Mbozi mkoani hapa, ambaye alikamatwa Februari 22, mwaka huu saa 12 jioni ambapo alikutwa amelima bangi kwenye shamba lenye ukubwa wa hekari tano, huku akiwa amechanganya na zao la mahindi.

Abdul alimtaja mshtakiwa wa pili katika kesi nyingine namba 29/2017 kuwa ni Yohana Rashid (24), mkazi wa Kijiji cha Nyimbili wilayani hapa, ambapo Februari 27, mwaka huu muda wa saa 12 jioni, alikutwa amelima bangi kwenye shamba lenye ukubwa wa robo hekari lililopo nyumbani kwake huku akijua kufanya hivyo ni kosa.

Hata hivyo, washtakiwa hao walikiri kutenda kosa hilo mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya, Nemes Chami ambapo alitoa nafasi kwa washtakiwa hao kujitetea, huku mshtakiwa wa kwanza aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu kwani ana watoto saba wanaomtegemea na ambao mama yao alifariki.

Kwa upande wa mshtakiwa wa pili katika utetezi wake, alisema alilima bangi hiyo kwa ajili ya matumizi yake ya nyumbani hivyo aliiomba mahakama imsamehe na kumpunguzia adhabu.

Aidha, kabla ya kutoa hukumu Mwendesha Mashtaka wa polisi, Saada Abdul, aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa washtakiwa ili iwe fundisho kwa wengine kwani kosa walilotenda washtakiwa lina madhara makubwa kwa vijana wengi ambao ni nguvu kazi ya Taifa.

Hakimu wa mahakama hiyo, Nemes Chami, akisoma hukumu alitupilia mbali utetezi uliotolewa na washtakiwa wote, ambapo alimhukumu kifungo cha miaka 30 gerezani mshtakiwa wa kwanza, Joel Mwangambaku na kifungo cha miaka 15 mshtakiwa wa pili, Yohana Rashid.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles