Wafanyakazi Udart watishia kugoma

PIC+SUMATRANA KOKU DAVID, DAR ES SALAAM

WAFANYAKAZI katika mabasi yaendayo haraka (Udart) wametishia kugoma na kuzuia mabasi hayo leo yasifanye kazi hadi watakapolipwa mishahara yao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, walidai kuwa tangu waanze kazi Mei 2 hadi leo, hawajawahi kulipwa mishahara yao na kwamba kila wakiuliza uongozi kuhusu haki zao wamekuwa wakipewa ahadi zisizotekelezeka.

Erick John, mmoja kati ya wafanyakazi hao, alisema walichukuliwa na Kampuni ya Udart kutoa huduma kwa abiria ndani ya mabasi na wengine katika vituo kwa makubaliano ya kulipwa  Sh 300,000 kwa mwezi na posho ya Sh 10,000 iwapo muda wa kazi utapita.

Alisema tangu wameanza kazi hiyo, wamekuwa wakipewa posho mara moja moja bila ya kulipwa mshahara kama walivyokubaliana, huku wakiendelea kusubiri taratibu za kupewa mikataba zikamilike.

“Sisi leo (jana) kama tusipopewa fedha zetu humu ndani hatutoki, tutalala humu humu na kesho tutafunga mageti hakuna gari hata moja litakalotoka nje kufanya kazi,” alisema Nassoro Selemani.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Udart, David Mgwassa, alipoulizwa alisema hawawatambui hao wafanyakazi.

Alisema anachokijua ni kuwa watumishi hao ni wa Kampuni ya SGA iliyoingia mkataba wa kazi na Udart.

Mgwassa alisema Udart haitarajii kumpa mtu yeyote mkataba na badala yake inatarajia kuvunja mkataba na kampuni ya SGA kutokana na utendaji wake wa kazi kutokuwa mzuri.

“Fedha wanazodai kwa ujumla ni kama Sh milioni 11, hivyo mimi nimeamua wahesabiwe fedha zao wapewe halafu waondoke ili wasitufanyie fujo.

“Kuhusu ulinzi wa vituo, sisi tunatumia Kampuni ya China Tanzania Security na si wao kama wanavyodai,” alisema Mgwassa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here