24.6 C
Dar es Salaam
Saturday, September 7, 2024

Contact us: [email protected]

Wazazi wanawasaidiaje watoto kielimu?

image-20150406-26496-uo448iMOJA ya jambo linalozungumzwa na walimu na AZISE (asasi zisizo za kiserikali), na hasa zile zinazoshughulikia masuala ya elimu, ni kuhusika kwa wazazi katika elimu ya watoto wao. Wao wanaona kuwa ili mtoto aweze kufanya vizuri shuleni, lazima kuwe na namna fulani ya ushirikishwaji wa wazazi.

Nafahamu kuwa katika baadhi ya nchi, au hata shule hapa nchini, walimu hutoa majukumu kwa wazazi wa watoto wanaosoma shule za kutwa…. Moja ya majukumu ni mzazi kupitia madaftari ya mtoto wake, kusahihisha mazoezi na kutia saini kuwa aliona kazi za mwanawe. Usipofanya hivyo mtoto anarudishwa nyumbani.

Hapa kwetu utaratibu duni sana wa kuwashirikisha wazazi na walezi ni kuwapatia taarifa za muhula za maendeleo ya masomo kwa watoto wao. Wazazi wanaona tu alama alizozipata mtoto lakini hakuna maelezo ya ziada ya kitu gani kilimfikisha mtoto hapo alipo. Nitalizungumzia kidogo kwa siku ya leo hilo la kuwashirikisha wazazi katika elimu na mafunzo ya watoto wao.

Wakati shule zinapofungwa na zinapofunguliwa ni wakati mwafaka wa kuwaambia wazazi ni jukumu lao katika maendeleo ya elimu ya watoto wao wenyewe. Kuna namna mbalimbali ya kulifanya hilo.  Kwanza, ili mzazi aweze kujishirikisha kikamilifu katika elimu ya mwanawe ni lazima aambiwe kuwa kuna jukumu hilo na hilo atalifanya kama mwalimu atamwita mzazi shuleni, wakaongea juu ya hilo na kuweza kufanya tathmini ya uwezo wa wazazi/ walezi katika kutekeleza jambo hilo.

Katika jamii yetu wazazi wengi si watu wanaoweza kulifanya jambo hilo kutokana na wao wenyewe kuwa na elimu duni, na pengine kukosa fursa ya wakati wa kutosha kwa sababu umasikini na kutumia muda mwingi kukimbiza shilingi. Lakini walimu wanaweza kupanga utaratibu wa kumtumia ndugu wa mwanafunzi, kama yupo, ambaye ana elimu na ufahamu wa kutosha na anaonekana atafanya jukumu hilo.

Lakini njia nyingine pia ni mwalimu kama anaweza kupanga siku moja kwa mwezi ambapo wazazi wanaitwa kukutana na walimu na wanafunzi kuzungumzia elimu ya watoto. Kwa sasa hivi wazazi wanaitwa siku ambayo mtoto amekuwa mtovu wa nidhamu, basi mtoto anashitakiwa kwa wazazi wake.

Lakini siku mtoto amefanya vizuri katika masomo, wazazi hawaitwi kuja kusikia mafanikio ya mtoto wao. Mtoto anaposifiwa na mwalimu mbele ya wazazi linaweza kumjenga kiakili, kisaikolojia na hivyo kuwa mtu anayehangaika kuhakikisha kuwa anafanikiwa zaidi na zaidi.

Njia nyingine ya kuwashirikisha wazazi ni kutayarisha maonyesho ya kielimu shuleni. Kama mfumo wa ufundishaji – pedagogia – unakuwa ni ule wa ushirikishi na unaohamasisha watoto kwa wabunifu, wagunduzi na wanaofanya elimu kwa vitendo, ni rahisi mno kwa watoto kuonyesha kile walichovuna katika elimu yao.

Walimu wanatakiwa kuhakikisha kuwa kwa vile watoto watataka kuonyesha walichokielewa shuleni, basi mfumo wa ufundishaji uwe na namna ya kuwawezesha watoto katika hilo. Kwanza, watoto waambiwe kuwa katika hatua fulani, watatakiwa kuonyesha wazazi na wageni wengine kile wanaochokivuna shuleni.

Hali ya kuwa wazazi watakuja kujionea wenyewe inaweza kuwaamsha na kuwajengea hamasa kubwa. Kila mmoja atataka kuonyesha alivyo bora. Aidha, wazazi wakiambiwa nao wanaweza kuwa wa msaada mkubwa kwa kuwapatia ushauri (kwa wazazi wenye elimu ya kutosha) au msaada wa fedha, au vifaa vya kufanyia maonyesho, ili mradi, nasisitiza; wazazi wawe wameambiwa mapema juu ya maonyesho hayo, faida yake na kuwa wanaweza kuombwa msaada wa hali na mali kuyafanikisha.

Maonyesho yasiwe ya gharama kubwa, la msingi ni kutaka kuimarisha ubunifu kwa watoto na namna ambayo wanaweza kuwaonyesha wazazi kuwa wanaweza na wanaelewa wanachokisoma. Mtoto anajisikia vizuri kama ataweza kuwaeleza wazazi na watu wazima wengine kile anachojifunza na litamwongezea kujiamini, na mapenzi kwa walimu, pia kuimarisha ushirikiano miongoni mwao.

Baada ya maonyesho, walimu wanaweza kukaa na wazazi ili kufanya tathmini ya namna ya kuboresha tendo hilo na wazazi kuahidi msaada zaidi kufanikisha elimu ya watoto wao. Hilo linaweza kufanyika mara moja kwa muhula. Kwa hiyo, maoneysho mawili kwa mwaka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles