WAFANYAKAZI 7 WA VYETI FEKI WARUDISHWA KAZINI MUHIMBILI

0
656

MWANAIDI MZIRAY (TSJ) NA TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM


WATUMISHI saba kati ya 134 wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ambao waliondolewa kazini baada ya kubainika na vyeti vya kughushi, wamerudishwa kazini.

Hatua hiyo imefikiwa  siku chache baada ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Laurean Ndumbalo kusema watumishi 450 wameshinda rufaa zao.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Uhusiano wa MNH, Neema Mwangomo alisema watumishi hao tayari wameandikiwa barua za kurudi kazini.

Alisema watumishi sita vyeti vyao vilikuwa na utata baada ya majina yao kuonekana katika vituo vya kazi viwili tofauti.

“Watumishi hao walihamia hapa na katika uhakiki wa vyeti majina yao yalionekana katika vituo viwili.

“Hivyo walitakiwa kupeleka vyeti halisi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuhakikiwa ambako  wamejiridhisha na kuwarejesha kazini,” alisema Neema.

Msemaji huyo wa MNH alisema watumishi watano walikata rufaa na mmoja kati yao alishinda hivyo naye  amerudishwa kazini.

Hospitali ya Muhimbili ilikumbwa na sekeseke hilo baada ya tangazo lililosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji, Profesa Lawrence Museru kutaja majina na idara za watumishi ambao walibainika kuwa na vyeti vya kughushi.

Tangazo hilo lilisitiza kuwa watumishi walioorodheshwa katika orodha hiyo walitakiwa kujiondoa wenyewe kazini kabla ya Mei 15, mwaka huu.

Profesa Maseru alisema iwapo watumishi hao hawakuridhishwa na uamuzi huo wakate rufaa kwa Katibu Mkuu  Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kabla ya tarehe hiyo na barua hiyo ni lazima ipitie kwake.

Idara   zilizoongoza kuwa na watumishi waliobainika kuwa na vyeti vya kughushi ni Kurugenzi ya Uuguzi (70), ikifuatiwa na Kurugenzi ya Tiba watumishi 20.

Nyingine ni Kurugenzi ya Tiba Shirikishi (14), Tehama (11), Upasuaji (4) na Raslimali (2)

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here