24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Wafanyabiashara wanaoficha mafuta washushiwa rungu

Andrew Msechu

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imevifutia leseni za uuzaji wa mafuta mafuta vituo vitano, kwa makosa ya kuficha, kutouza na kuuza mafuta juu ya bei elekezi huku ikotoa onyo kali kwa wauzaji wa nishati hiyo wanaojaribu kufanya hujuma na kukiuka maagizo ya Serikali.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa Ewura, Titus Kaguo, alisema uamuzi huo umechukuliwa baada ya tathmini ya kina iliyowawezesha kubaini kuwa kuna sababu za makusudi kwa wauzaji hao kuhujumu uuzaji wa mafuta.

Alisema katika uchunguzi wa awali uliofanywa na Ewura, kuna dalili za wauzaji wa mafuta kufanya hujuma kwa kuwanyima wananchi mafuta kwa makusudi na kutoa onyo kwa waauzaji wote kutofanya hujuma ambazo zitawaingiza katika uhujumu uchumi.

“Katika uchunguzi tumeona kuna viashiria vya hujuma ambazo bado hatujajua hasa kiini chake, ila tunatoa onyo kali kwa wauzaji wote wa mafuta kutojihusisha na aina yoyote ya hujuma inayoweza kuwaingiza kwenye uhujumu uchumi kwa kujaribu kukwamisha juhudi za Serikali kuleta maisha bora kw awatu wake,” alisema.

Alisema miongoni mwa waliofungiwa ni wauzaji wawili wa jumla, ambao ni Olympic Petroleum na Mansoor Oil Industries Ltd (Moil) baada ya kutakiwa kutoa maelezo na kutoa maelezo ambayo hayakujitosheleza.

“Ewura imeamua kuchukua hatua kali kwa wauzaji hao wakubwa baada ya kufuata taratibu zote ikiwemo kuwapa muda wa kutoa maelezo na kushindwa kutoa maelezo yanayojitosheleza juu ya kwa nini hawakuwa wanauza mafuta kama leseni zao zinavyoelekeza.

“Kwa hiyo utaratibu utakaofuata ni wa kutekeleza matakwa ya kisheria ambayo yanataka kuwatangaza, hivyo tutatekeleza utaratibu huo na kuwafungia rasmi ndani ya muda mfupi ujao,” alisema Kaguo.

Alisema Ewura pia imechukua uamuzi wa kuvifungia vituo vitatu vinayouza mafuta ya rejareja kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kutouza mafuta kwa mujibu wa maelekezo ya leseni na kuuza mafuta juu ya bei elekezi.

Alisema vituo hivyo ni vya B.O. Petrol Station kilichopo Bagamoyo kwa kutouza mafuta bila sababu ya msingi, kituo cha mafuta cha Mexon Energy Ltd kilichopo Makambako na kituo cha Mexon Energy Ltd kilichopo Njombe kwa kuuza mafuta juu ya bei elekezi.

Alisema kituo cha mafuta cha Mtweve oil huko Chunya pia kimefungiwa baada ya kubainika kuuza mafuta juu ya bei elekezi kwa kuuza kwa Sh 1985 badala ya Sh 1637 iliyotolewa na Serikali hata baada ya kuonywa mara kadhaa.

“Kwa hiyo kituo hicho pia kimefungiwa na kwa kuwa kimekutwa kikiuza kwa bei hiyo mara mbili, kitalipa faini ya kisheria ya Sh milioni tatu mara mbili, ambayo itakuwa Sh milioni sita. Pamoja na adhabu hiyo watakabidhuwa kwa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) ili kubaini kama wamekwepa kodi au la kwa kuwa hawakuwa wakitumia mashine za EFD,” alisema.

Alisema kampuni ya wauzaji wa mafuta wa jumla wa Oryx wamepewa onyo na karipio baada ya kutoa maelezo ya kina kuhusu sababu za kutokuwa na mafuta kwa kipindi ilipokaguliwa na Ewura huku kampuni ya Mogas ikisamehewa baada ya kutoa maelezo kuwa ilikuwa haifanyi biashara kwa kuwa ilikuwa imefungiwa na Wakala wa Mizani na Vipimo (WIMA) lakini ilipewa onyo kwa kushindwa kutoa taarifa hiyo kwa Ewura.

“Kampuni hii ya Mogas ilikuwa na sababu ya msingi kabisa, kwamba haikuweza kufanya biashara kwa kuwa ilikuwa imefungiwa na Wakala wa Mizani na Vipimo. Lakini kosa lake ni kwamba baada ya kufungiwa ikaacha kuuza mafuta bila kuiarifu Ewura. Katika hili imesamehewa lakini imepewa onyo pia,” alisema.

Kaguo alisema kampuni nyingine ya Mansoor Oil Tanzania Ltd wa mafuta ambayo ilikuwa ikifuatiliwa baada ya kulalamikiwa ilieleza kuwa tatizo ni watumiaji wake kushindwa kutumia mfumo wa kielektroniki uliofungwa na kampuni hiyo.

Alisema uongozi wa kampuni hiyo ulieleza kuwa wanaolalamika hawajajua namna ya kutumia mfumo huo hivyo Ewura bado inafutilia kwa karibu kuhusu utetezi huo kabla ya kutoa uamuzi.

Kaguo alisema kwa upande wa kampuni ya mafuta ya Oilcom ambayo pia ililalamikiwa badaa aya baadhi ya vituo vyake kutouza mafuta, ilijieleza kuwa ina matatizo yanayohusiana na mifumo yake ya kibiashara ambapo wadaiwake wamezuia mali zao, hivyo imepona kuadhibiwa.

HALI YA MAFUTA

Akizungumzia hali ya mafuta nchini, Kaguo aliwataka wananchi kutotaharuki na kuendelea kununua mafuta bila wasiwasi kwa kua yapo ya kutosha kwa muda mrefu ujao.

Alisema Ewura imepata taarifa kuwa kuna baadhi ya maeneo nchini wananchi wameanza kununua mafuta tofauti na mahitaji yao kwa hofu kwamba huenda yakaadimika siku za karibuni, suala ambalo si sahihi.

“Niwaambie Watanzania kwamba hakuna haja ya kuwa na taharuki, mafuta yapo ya kutosha na ya muda mrefu kwa hiyo waendelee kununua kwa kadiri ya mahitaji yao ya wakati kama kawaida,” alisema.

Alisema Ewura ilipata taarifa kuwa kulikuwa na uhaba wa mafuta Ifakara mkoani Morogoro ivyo tayari imeshaiagiza kampuni ya Oryx kupeleka mafuta ya petroli na dizeli kwenye vituo vya mafuta vya Ester Oil katika eneo hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles