24.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 8, 2021

Wafanyabiashara soko la Mabibo walia ubovu wa miundombinu

BATROMAYO JAMES (DSJ) – DAR ES SALAAM

WAFANYABIASHARA wa soko la Mabibo, Dar es Salaam wamelalamikia ubovu wa miundombinu katika soko hilo, hasa nyakati za mvua, wakisema mitaro ya kupitisha maji huwa inaziba na kusababisha tope.

Wakizungumza na MTANZANIA jana, wafanyabiashara hao walidai adha hiyo ni kubwa na inasababisha wapate ugumu wa kufanya biashara, kwani soko zima linatapakaa matope.

Meneja wa soko hilo aliyejitambulisha kwa jina la Ashim Ramadhani maarufu ‘Kachala boy’, alisema yeye kama meneja wa soko kwa upande wa matunda, amelilalamikia suala hilo kwa muda mrefu sana bila ya mafanikio.

Ramadhani alisema wao wanalipa ushuru wa soko kila siku bila kugoma na kumwomba Rais Joseph Magufuli, akiwa kama mtetezi wa wanyonge kuliona suala hilo na kuwasaidia na ikiwezekana afike na kuwatatulia kero yao hiyo ambayo imekuwa ni ya muda mrefu.

“Tumekuwa tukilalamika sana juu ya hili, lakini halitatuliwi, kila siku tunapewa ahadi kuwa linafanyiwa kazi na kazi yenyewe hatuoni, hivyo tunaomba kama baba yetu, Rais wetu mpendwa Magufuli akiliona hili atutatulie shida yetu ikiwezekana afike sokoni kutusalimia na kuona hali halisi ya soko,” alisema Ramadhani.

Alisema soko la Mabibo ni kubwa na linaingizia taifa mapato makubwa, lakini haliboreshwi, ukiangalia soko la Buguruni lilikuwa bovu kuliko soko la Mabibo, lakini Rais Magufuli alipofika pale akaagiza liboreshwe na kweli lilitekelezwa agizo lake.

Naye Meneja wa soko hilo kwa upande wa Manispaa ya Ubungo, Moses Olomi, alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo na ameomba wafanyabiashara hao kuwa watulivu, kwani suala hilo lipo kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo na wanalifanyia kazi.

Ulomi alisema mvua zilinazonyesha hivi sasa ambazo sio za msimu zimeharibu miundombinu na kusababisha mazao kutofika sokoni, huku kuna uhitaji mkubwa wa baadhi ya mazao, hivyo unaleta mfumuko mkubwa wa bei na kushuka kwa ukusanyaji wa mapato ndani ya soko hilo.

“Ninawasihi wafanyabiashara wawe watulivu kidogo, kwani suala hili lipo kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo na tunalifanyia kazi, tayari tumeanza ukarabati wa vibanda na muda wowote mvua zikitulia tutamwaga kifusi ndani ya soko lote,” alisema Ulomi.

Ulomi aliendelea kusema changamoto kubwa ya soko la Mabibo ni la asili, kwani eneo lile lilikuwa mashamba ya mpunga, hivyo kifusi kikimwagwa huzama chini na hali hiyo kurejea tena.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,538FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles