23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Wachache wajitokeza kupiga kura Dodoma

MWANDISHI WETU -DODOMA

KATIKA Jimbo la Dodoma Mjini, watu wachache wamejitokeza kupiga kura katika vituo mbalimbali huku baadhi ya wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wakiwa wamekaa tu wakisubiria watu.

MTANZANIA ilizunguka katika baadhi ya vituo mara baada ya upigaji kura kumalizika saa 10 jioni na ilijionea idadi ya watu wachache waliojitokeza kupiga kura tofauti na waliojiandikisha.

Katika kituo cha Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Viwandani namba mbili, waliojiandikisha kupiga kura ni 310, lakini waliojitokeza kupiga kura ni 81.

Kituo cha Ofisi ya Mtendaji namba moja katika Kata hiyo hiyo, waliojiandikisha katika daftari la kudumu la kupigia kura ni 310 huku waliopiga kura wakiwa ni 59 na kura tatu ziliharibika.

Katika kituo cha Samora namba moja, Kata ya Viwandani waliojiandikisha ni 435 ambapo waliopiga kura ni 94, na kituo cha Moku Securty Guard namba mbili walioandikishwa ni 479 waliopiga kura ni 103.

Katika kituo cha Jumba la Maendeleo namba moja, Kata ya Madukani waliojiandikisha ni 408, waliojitokeza kupiga kura ni 118, huku Jumba la Maendeleo namba mbili waliojiandikisha ni 408 waliopiga kura ni 114.

Kituo cha WEO kipande namba moja waliojiandikisha ni 354 na waliopiga kura ni 84, huku kituo cha WEO kipande  namba mbili waliojiandikisha ni 354 waliopiga kura ni 95 na WEO namba tatu waliojiandikisha 352 waliopiga kura ni 88.

 Vituo vya Shule ya Msingi  Kizota, Nkuhungu, Maghorofani, Msalato, Nzuguni A, Kikuyu na Four ways watu wachache walijitokeza  kupiga kura hadi majira ya saa tano asubuhi.

Hata hivyo katika Kata ya Chang’ombe, kituo cha Chang’ombe Juu, idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura ilikuwa kubwa ambapo wananchi walifika katika kituo hicho majira ya saa 12 asubuhi.

Ilipofika majira ya saa moja asubuhi upigaji kura ulianza huku wananchi walianza kulalamika kwamba wasimamizi wa kituo hicho wapo taratibu sana na idadi ya watu ni wengi.

Katika kituo cha Mambo Poa kilichopo Kata ya Uhuru katikati ya Jiji la Dodoma pia idadi ya watu ilikuwa kubwa ambapo kulikuwa na jumla ya vituo nane vya kupigia kura.

Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jimbo la Dodoma Mjini lina jumla ya vituo 911 vya kupigia kura ambapo watu zaidi ya 300,000 walitarajiwa kupiga kura.

MAVUNDE

Mgombea ubunge Jimbo la Dodoma Mjini kwa tiketi ya CCM, Anthony Mavunde aliyepiga kura katika kituo cha Chadulu, alizungumza na waandishi wa habari ambapo aliishukuru NEC kwa kuweka vituo vingi vya kupigia kura, hivyo kutokuwepo kwa msongamano wa wananchi.

Alipoulizwa atayapokeaje matokeo Mavunde alisema wananchi ndio wenye mamlaka ya nani awatumikie.

MAJINA KUKOSEKANA

Changamoto kubwa iliyojitokeza jana ni baadhi ya wapigakura kulalamika kutokuyaona majina yao katika baadhi ya vituo vikiwamo NHC, Chadulu, Udom na Nzuguni.

Akizungumza na MTANZANIA, mpigakura Ramadhan Saibaba alisema alifika mapema katika kituo cha NHC na kutokuona jina lake hali iliyompa wakati mgumu ambapo baada ya kufuatilia baadae alipewa majibu kwamba majina ya kituo hicho yamehamishiwa katika kituo kingine cha LAPF ya zamani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles