26.9 C
Dar es Salaam
Friday, December 9, 2022

Contact us: [email protected]

Shibuda agoma kupiga kura

Derick Milton/ Samwel Mwanga -Simiyu

MGOMBEA urais wa kupitia Chama cha ADA-Tadea, John Shibuda amegoma kwenda kupiga kura hadi pale mawakala wake katika majimbo ya Maswa Mashariki na Magharibi mkoani Simiyu watakaporuhusiwa kuingia katika vituo vya kupiga kura.

Shibuda alisema kuwa hawezi kwenda kupiga kura endapo mawakala wake hawataruhusiwa kuingia katika vyumba hivyo baada ya kuzuiliwa kwa kile kilichoelezwa kuwa hawana barua za utambuzi.

Akiongea kwa njia ya simu na MTANZANIA kutoka Wilayani Maswa ambako ndiko alitegemea kupigia kura, Shibuda alisema kuwa amehangaika tokea asubuhi kuwatafuta wahusika wa kuweza kutatua jambo hilo, lakini imeshindikana.

Alisema mawakala wake wote katika vituo vya kupigia kura kwenye majimbo ya wilaya hiyo, wamekataliwa kuingia kwenye vyumba vya kupigia kura kutokana na kukosa barua za utambuzi kutoka msimamizi wa uchaguzi wa jimbo.

“Mpaka asubuhi hii (jana) hakuna barua ya wakala wa chama changu ambaye amepatiwa barua, wote wamekataliwa kuingia ndani ya vituo, namtafuta msimaizi wa uchaguzi hapokei simu yangu, nimewaeleza viongozi wa mkoa na wilaya, lakini bado hakuna usaidizi.

“Nimeamua kutokwenda kupiga kura mpaka pale mawakala wangu watakapopatiwa barua hizo, nimejiuliza kwanini msimamizi amechelewesha barua hizo na hakuna sababu za msingi,” alieleza Shibuda.

Alisema kuwa hawezi kuwasaliti watu wake kwa kwenda kupiga kura katika mazingira ambayo hana uhakika kama kura zake zitakuwa salama kutokana na kutokuwepo kwa mawakala wake.

MTANZANIA ilimtafuta msimamizi wa uchaguzi katika majimbo hayo, Dk. Fredrick Segamiko, ambaye alisema kuwa hawezi kuzungumzia malalamiko hayo kutokana na kutokuwa na mamlaka ya kumwongelea mgombea urais.

“Mgombea urais mamlaka ya kumwongelea ipo Tume ya Uchaguzi, mimi siwezi kuongelea chochote juu yake, malalamiko hayo tume ndiyo wenye mamlaka ya kuongelea, mimi naweza kuongelea malalamiko ya wabunge au madiwani,” alisema Dk. Segamiko.

Hata hivyo licha ya kusena hana mamlaka ya kumwongelea mgombea urais, ameeleza malalamiko hayo hayana ukweli kwani wagombea wote wa ubunge na udiwani wakiwemo wa chama hicho hakuna aliyeleta malalamiko hayo kwake.

Alisema kuwa mawakala wote wa vyama ambao aliwaapisha, barua za utambuzi zilianza kupelekwa juzi na nyingine zimepelekwa jana asubuhi na zimewafikia wote.

“Hakuna malalamiko kutoka kwa wagombea udiwani, ubunge, wakiwemo wa ADA-Tadea, lakini hakuna malalamiko ambayo nimeyapokea kutoka kwa mawakala wenyewe kama wamekosa barua au vyama vyao,” alisema Dk. Segamiko.

Alisema kuwa kama msimamizi ametekeleza wajibu wake wa kupeleka barua hizo kwa wahusika, ambapo alieleza labda shida kama itakuwa kwenye vyama husika kushindwa kuelewana na mawakala wao.

Hata hivyo, baadaye Shibuda alipiga kura katika kituo cha Sayusayu Shule ya Msingi Na 1 wilayani Maswa.

Shibuda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini aliwasili katika kituo cha kupigia kura majira ya saa 9.58 jioni na kuwa mpiga kura wa mwisho katika kituo hicho.

Mara baada ya kupiga kura Shibuda aliipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kazi nzuri waliyofanya ya kuandaa vituo vingi vya kupigia kura bila usumbufu na kufuata sheria na taratibu za upigaji kura huku akisisitiza kuwa hata uhesabuji kura na kutangaza matokeo ufanyike kwa uweledi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,735FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles