Wabunge watatekeleza azma yao kumuondoa Spika?

0
1314
Spika wa Bunge la Taifa Kenya, Justin Muturi

BUNGE la Kenya linaanza vikao vyake leo baada ya mapumziko ya mwezi mmoja huku Wakenya wakiwa na shauku ya kuona kama wabunge watatekeleza walichoahidi kukifanya kabla ya Bunge kuahirishwa.

Spika Justin Muturi aliitisha kikao cha dharura mwishoni mwa mwezi uliopita wakati wabunge wakiwa likizo ili kujadili na kupitisha mapendekezo ya Rais Uhuru Kenyatta ya kupunguza ushuru kwa asilimia nane ya bidhaa zote zinazotokana na mafuta.

Ni mjadala ambao ulishuhudia Rais Uhuru akiitisha kikao cha wabunge wote wa chama cha Jubilee huku kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, naye akifanya vivyo hivyo kwa wabunge wanaounda Muungano wa NASA wote wakiwa na lengo moja la kuwashawishi kupitisha mapendekezo ya kupunguza ushuru wa mafuta kutoka asilimia 16 hadi nane.

Wakenya wengi walikuwa na imani wabunge watapiga kura kukataa mapendekezo ya Rais kwa sababu yangefanya gharama za maisha kupanda na hivyo basi kumuumiza Mkenya wa kawaida.

Lakini kilichoshuhudiwa bungeni  kilikuwa sarakasi tupu kwani sauti za wabunge waliokataa mapendekezo ya Rais ndiyo yaliyosikika zaidi ila Spika Muturi akaamua vinginevyo na baadaye Rais Uhuru akatia saini Muswada wa Fedha 2018 ambayo sasa ni sheria.

Wabunge waliapa ‘kumshughulikia’ Spika Muturi pindi vikao vya Bunge vitakaporejea mapema mwezi huu wakisisitiza wao wanawawakilisha wananchi ambao waliwachagua na lengo lao bungeni ni kuona wananchi wanapata maisha bora.

Je, zile sauti zilizosikika za ‘Muturi must go!’ (Muturi lazima aondoke) kutoka kwa wabunge walioonekana kughadhabishwa na uongozi wa Spika hususani baada ya kusema Bunge limepitisha mapendekezo ya Rais, yataleta mageuzi bungeni? Je, watapiga kura ya kutokuwa na imani na Spika?

“Kama mbunge kutoka Jubilee, msimamo wangu umekuwa ushuru wa mafuta kubaki asilimia sifuri. Uongozi wa Bunge hili umetuangusha licha ya wingi wetu kuukata ushuru mpya uliopendekezwa na rais. Namheshimu Muturi lakini kwa suala hili tunatofautiana,” alisema Catherine Waruguru ambaye ni Mwakilishi wa Wanawake kutoka Kaunti ya Laikipia.

Naye Mbunge wa Turkana Kusini, James Lomenen, alimshutumu Muturi, Kiongozi wa walio wengi bungeni Aden Duale, kiongozi wa walio wachache bungeni John Mbadi na Kiranja wa walio wachache Junet Mohammed kwa kutumia nafasi zao kulazimisha mapendekezo ya Uhuru kupitishwa.

“Wakenya lazima wajue Duale, Muturi, Mbadi, Junet na wenyeviti wa kamati mbalimbali bungeni ndiyo chanzo cha muswada huo kupita kwa nguvu,” alisema.

Njia bora kwa mujibu wa Mbunge wa Dagoretti Kaskazini, Simba Arati, kudhibiti utawala wa kimabavu bungeni ni kuanza mchakato wa kura ya kutokuwa na imani na Muturi licha ya Duale kusema alitumia mbinu na nafasi aliyonayo bungeni kuhakikisha msimamo wa serikali unapita Bunge likiamua kupiga kura.

Ili kumuondoa Spika ofisini, pendekezo linalowasilishwa bungeni linahitajika kuungwa mkono  si chini ya asilimia 75 ya wabunge. Baada ya hapo, notisi ya nia ya kumuondoa Spika inawasilishwa kimaandishi kwa Katibu wa Bunge ikiwa na sahihi ya takribani thuluthi moja ya wajumbe ikiainisha sababu za msingi za kumuondoa Spika.

Kwa mujibu wa Ibara 178 (2) (b) ya Katiba ya Kenya, mbunge yeyote aliyechaguliwa anakaimu nafasi ya Spika na kuendesha mjadala wa pendekezo la kumuondoa Spika ikiwamo Spika mhusika kupewa nafasi ya kujibu shutuma kabla hawajapiga kura. Vivyo ndivyo ilivyo na mabadiliko muhimu kama kuna hoja ya kumuondoa Naibu Spika.

Ni dhahiri pendekezo la kumuondoa Spika Muturi litapata wakati mgumu hususani baada ya Duale kuonesha imani yake kwamba jaribio hilo halitafaulu.

Hata hivyo, wabunge pia wanataka Duale na Mbadi kuachia nafasi zao nyeti bungeni na kinachosubiriwa wakati vikao vya Bunge vinaporejea ni namna wabunge wa Jubilee na NASA watakaposhirikiana kutimiza azma yao hiyo.

“Uamuzi wa kuwaondoa wanaoshikilia nafasi za chama haifanywi barabarani, lazima ipate baraka kutoka kwa viongozi wa chama. Tupo chini ya maelekezo maalumu kuhakikisha hoja za serikali zinapata ushindani na hicho ndicho kilichotokea siku hiyo,” alisema Duale.

Tayari Mbunge wa Kilifi Kaskazini, Owen Baya ambaye pia ni katibu mipango msaidizi wa Chama cha ODM, ameshamuandikia barua kiongozi wa ODM, Raila akitaka Mbadi aondolewe katika nafasi yake ya Kiongozi wa Wachache bungeni kwa madai ameshindwa kusoma na kuwashawishi nini ambacho kambi ya wachache bungeni wanahitaji.

Lakini Mbadi ambaye pia ni Mbunge wa Suba Kusini amesema yupo tayari kwa lolote na kusisitiza ataunga mkono mapendekezo ya serikali endapo anaona inayo manufaa kwa mwananchi wa kawaida.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here