29.7 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

WABUNGE WAMKAANGA WAZIRI WA UVUVI

NA GABRIEL MUSHI- DODOMA


WABUNGE wamemuonya Waziri wa Mifugo na Uvivu, Luhaga Mpina na kumweleza kwamba operesheni inayoendelea ya kudhibiti uvuvi haramu, inaweza kugeuka kuwa kaa la moto kama ilivyokuwa Tokomeza Ujangili na kudai inakiuka haki za binadamu.

Pamoja na hali hiyo, pia walimtaka Waziri huyo kutaja majina ya baadhi ya wabunge kama alivyoeleza kuwa nao wanajihusisha na uvuvi haramu.

Hayo waliyasema jana Dodoma wakati wakichangia mjadala katika semina elekezi kuhusu uvuvi haramu iliyotolewa na wizara hiyo.

Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Kuteuliwa, Alhaj Abdallah Bulembo (CCM), alisema anao ushahidi wa kutosha kuwa watendaji wa wizara hiyo wanamwangusha Waziri husika kwa kuendekeza vitendo vya rushwa.

“Mwenyekiti mimi ni mfano halisi, niliomba leseni ya kuingiza samaki sato nchini, lakini nikazungushwa zaidi ya mwaka mmoja na miezi mitatu na mwishowe sikupewa, si mimi tu asilimia kubwa ya Watanzania hawapewi leseni, kuna urasimu mkubwa kwani wanaopewa leseni ni Wahindi na Wazungu.

“Hili ni jambo ambalo limenitokea na nina uhakika na ninachokiongea, hivyo nakuonya Waziri angalia hawa watendaji wako watakuangusha,” alisema Bulembo.

Naye Mbunge wa Kiteto, Emmanueli Papian (CCM), alimtaka Waziri Mpina kuwataja wabunge na madiwani wanaojihusisha na biashara hiyo haramu.

“Kule Uganda wameweka sheria kali ambazo zimetokomeza kabisa suala hili la uvuvi haramu, sasa tunamtaka Waziri ataje hao vigogo ili kutokomeza suala hili,” alisema.

Kwa upande wake Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya (Chadema), alisema operesheni tokomeza uvuvi haramu inawaumiza zaidi akinamama kwa sababu wanakamatwa na samaki ambao tayari wameshawanunua kwa matumizi yao ya nyumbani au ya kibiashara.

“Hii operesheni tusipoangalia itakuwa kama ile ya ujangili kwa sababu vitendo wanavyofanyiwa kinamama ni ukiukwaji wa haki za binadamu, mama kabeba samaki wake kwenye boxi ndani ya daladala, anakamatwa anapigwa faini Sh 600,000 na mwenye daladala anapigwa faini mamilioni ya shilingi, hii si sawa kabisa,” alisema.

Hoja ya Bulaya iliungwa mkono na Mbunge wa Mlimba, Suzani Kiwanga (Chadema) ambaye alisema baadhi ya wavuvi katika Mto Kilombero wakikamatwa wanamezeshwa samaki mzima mzima, jambo ambalo ni kinyume na haki za binadamu.

Mbunge wa Geita Mjini, Costantine Kanyasu (CCM), alisema wabunge hawapingi operesheni hiyo ya uvuvi haramu ila tatizo ni taratibu zinazotumika katika kutekeleza operesheni hiyo.

Alisema baadhi ya wavuvi wamefariki kwa kupata mshtuko kutokana na zana zao kama vile mitumbwi na injini kuchomwa moto, baada ya kukamatwa na samaki au nyavu zisizokubaliwa kisheria.

Akijibu baadhi ya hoja za wabunge hao, Waziri Mpina alikiri kuwa wapo baadhi ya watendaji wanaojihusisha na vitendo vya rushwa hivyo atawashughulikia.

Aidha, alimtaka Bulembo kuendelea na utaratibu wa kupata leseni ya kuingiza sato nchini kwa kuwa jambo hilo amelisikia na atalichukulia hatua.

Pamoja na mambo mengine, alisema sheria inaruhusu hata kutaifisha zana za uvuvi haramu ikiwamo magari, lakini kwa ubinadamu ameagiza kutotaifishwa kwa zana hizo wala kuchoma moto pindi zinapokamatwa.

“Kama kuna mvuvi ambaye mitumbwi au injini pamoja na pikipiki au magari yamechomwa moto, aje aniambie niwachukulie hatua kwa sababu tayari nimeagiza kuwa zitozwe faini na si kuchoma moto,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji, Mahmoud Mgimwa, alimwagiza Waziri Mpina kuleta kwa maandishi hoja na maswali yaliyoulizwa na wabunge hao.

Alisema wabunge hawapingi operesheni ya uvuvi haramu ila kinachotakiwa ni kufuata taratibu na kutokiuka haki za binadamu.

Awali wakiwasilisha mada kuhusu operesheni tatu zinazoendelea kufanywa, Mpina alisema hadi sasa Serikali imekusanya zaidi ya Sh bilioni saba kutokana na faini zinazokusanywa na vikosi vya operesheni hizo.

Operesheni hizo ni zile zinazotokana na uvivu wa kutumia mabomu na kemikali (NMATT); Operesheni Sangara na Operesheni Jodari.

Mkurugenzi wa wizara hiyo, Magese Bulai, alisema zaidi ya Sh bilioni 1.6 zimetumika katika operesheni hiyo iliyoanza Januari mosi mwaka huu.

Aidha, alisema kulingana na takwimu zilizopo, Ziwa Victoria lina wavuvi zaidi ya 190,000 ambao wanaweza kuvua samaki wenye thamani zaidi ya Sh trilioni 1.1 kwa mwaka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles