22.5 C
Dar es Salaam
Saturday, May 11, 2024

Contact us: [email protected]

VIROBA VYA SH BILIONI 10 VYAKAMATWA DAR

Na ASHA BANI


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, amesema kikosi kazi  cha Serikali kimefanikiwa kukamata shehena ya pombe zinazofungwa kwenye vifungashio vya plastiki maarufu kama viroba katoni 99,171  yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 10.83.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana January alisema kuwa operesheni hiyo iliyodumu kwa siku tatu imefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Alisema mbali na kukamata idadi kubwa ya pombe hizo pia wamefanikiwa kuibua mambo mengi yakiwemo ya wahamiaji haramu, nyaraka feki za Serikali, makampuni yanayozalisha na kusafirisha pombe usiku na shehena  ya viroba iliyokutwa imefichwa kwenye handaki eneo la Kariakoo.

‘’Jumla   ya wakaguzi 58 kutoka katika taasisi mbalimbali ikiwemo jeshi la polisi walihusishwa na kugawanywa kwa timu tatu katika mikoa ya kikodi ya Mamlaka ya Mapato TRA, wamefanikisha kwa kiwango kikubwa zoezi hilo lakini tunaahidi kuendelea kufanya vyema zaidi ya hapo,’’ alisema January.

Alisema watahakikisha wanasimamia viwanda, maduka, maghala na baa zinazofanya biashara kinyume na sheria za udhibiti ikiwemo ya chakula, dawa na vipodozi  kupitia sheria ya viwango namba 2 ya 2009 pamoja na ile ya vileo ya mwaka 1968 na kufanyiwa marekebisho mwaka 2012.

Waziri January, alisema hadi sasa viwanda 16 vya kuzalisha pombe kali, maduka 18, maghala manne, baa tatu, kiwanda kimoja cha kuzalisha bidhaa za plastiki ikiwemo vifungashio tayari vimefanyiwa ukaguzi  ambapo viroba vya mililita 50,  katoni 69045 na mililita 100 katoni 29.344 za mililita 90 ni 782, chupa za ujazo mililita 100 ni 10,625.

Alizitaja pombe kali ambazo zinafungwashwa kwenye viroba kuwa ni Red Wine, Banjuka, Officer’s cane Sprit, Flash Ginna Dragon  ambazo hazikidhi viwango na hazijasajiliwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).

‘’Makampuni yote yaliyokamatwa hayana vyeti vya Tathmini ya athari kwa Mazingira (EIA) baadhi ya makampuni hayajalipa kodi na hayakuwa na cheti cha TFDA wala cheti cha TBS,’’ alisema January

Alisema shehena hiyo ya viroba iliyokamatwa imezuiliwa katika stoo za viwanda, maduka ya jumla, baa na maghala ya usambazaji na Idara ya Uhamiaji imeagizwa kushughulikia na kuchukua hatua kwa raia wa kigeni wasio na vibali vya kuishi nchini ambao walikutwa kwenye baadhi ya viwanda.

Pia ameagiza oparesheni hiyo kuendelea nchi nzima kwa kasi zaidi kwa kuhusisha kamati za ulinzi na usalama na serikali za mitaa.

Alisema hatua mbalimbali zitakachukuliwa ikiwa ni pamoja na kufungua kesi mahakamani dhidi ya wafanyabiashara waliokiuka na adhabu kali zitolewe.

Waziri huyo alitangaza bingo katika mkutano huo ambapo alisema itatolewa zawadi ya Sh 500,000 kwa atakayefanikisha kutoa taarifa dhidi ya mtu anayeingiza pombe za viroba zilizopigwa marufuku.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles