24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

JPM AAGIZA SERIKALI, TAASISI ZAKE KUITUMIA NMB

Na Mwandishi Wetu-MTWARA


RAIS Dk. John Magufuli, amewaagiza viongozi wa Serikali wakiwemo wa wakuu wa wilaya nchini kuhakikisha wanafanyabishara na Benki ya NMB kwani Serikali ina hisa kwenye benki hiyo na inapata faida.

Kauli hiyo aliitoa juzi mjini Mtwara, alipokuwa akizindua Kituo cha Kibiashara cha NMB kinachojulikana kama ‘Mtwara Business Centre’ ambapo pia amezitaka benki zote nchini kuangalia uwezekano wa kushusha riba ili ziweze kuwahudumia wananchi wengi zaidi.

“Nikuombe Waziri (Dk. Mpango), toa maelekezo kwa sababu wewe ndiyo unasimamia pesa, pesa ya serikali ipitie NMB ili ipate gawio kubwa zaidi, wale wengine wanaofanya biashara bila kuifaidisha Serikali na kugawana gawio wao kwa wao huku Serikali haipati faida yoyote, hatutafanya biashara nao,” alisema Rais Dk. Magufuli

Pamoja na hali hiyo aliiomba NMB kushiriki katika kuunga mkono ajenda ya Serikali ya kuifanya Tanzania kuwa ya viwanda.

“Naomba NMB mshiriki katika kukopesha viwanda hasa viwanda vidogo vidogo na hivyo kuunga Mkono juhudi za serikali katika kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda,” alisema

Kutokana na hali hiyo alizitaka benki nchini kupunguza riba ili kuwahamasisha zaidi Watanzania wengi waweze kukopa kwa manufaa  kama njia ya kuchangia maendeleo ya nchi.

“Naomba mabenki waanze kufikiria kupunguza riba, mkirekebisha riba zenu Watanzania wengi zaidi watahamasika kukopa na nyinyi kupata faida zaidi.

 “Kwenye mabenki haya ni vizuri kuwa na benki hata tatu tu zinazofanya kazi vizuri kuliko kuwa na msururu wa mabenki ambayo mengine ni kufanya utapeli tu, suala si kuwa na mabenki mengi.

“Suala ni kuwa na benki ambazo zinafuata sheria za nchi, zenye kutoa riba ndogo, zenye kufuata mazingira na masharti ya nchi na ambazo zinakuwa karibu na wananchi wa maisha ya chini siyo benki zinazowabagua wananchi wa chini,” alisema mkuu huyo wa nchi.

Awali akimkaribisha Rais Magufuli, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango,  alisema Serikali haina mpango wa kuuza hisa zake zilizopo NMB kutokana na mwenendo mzuri wa benki hiyo hivyo kuwa kielelezo cha ubinafsishaji bora ambao serikali iliufanya katika sekta ya kibenki.

Alisema Serikali inamiliki asilimia 32 ya hisa ndani ya NMB zenye thamani ya Sh bilioni 430 ambapo thamani ya uwekezaji huo ni mara 10 zaidi ya thamani ilivyokuwa mwaka 2005 wakati benki hiyo ina binafsishwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NMB, Profesa Joseph Semboja,  alisema NMB imefanya maboresho makubwa na hivyo kuwa na uwezo mkubwa wa kutoa huduma za kifedha kwa kila kada ya watanzania na serikali kwa ujumla.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa NMB, Ineke Bussemaker alisema nia ya benki ni kuendelea kukua zaidi huku ikitoa suluhu ya vipaumbele vya serikali na kujikita katika ukusanyaji wa mapato ya serikali kwa njia za kielektroniki.

“Kwa kutumia teknolojia mbalimbali, NMB tumewekeza zaidi kwenye kutatua changamoto mbalimbali za wateja wetu na hivyo kutoa fursa za kutumia zaidi njia za benki kuliko kutumia njia za malipo kwa kutumia fedha taslim,” alisema Ineke.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles