23.6 C
Dar es Salaam
Thursday, May 9, 2024

Contact us: [email protected]

Viongozi wataka uamuzi mgumu uchukuliwe kusimamia rasilimali

NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

VIONGOZI wa Afrika wametakiwa kuchukua uamuzi mgumu katika kusimamia rasilimali za asili kuliepusha bara hilo na uharibifu wa mazingira.

 Suala hilo ni miongoni mwa maazimio yaliyofikiwa jana wakati wa mkutano wa sita wa Jukwaa la Uongozi Afrika lililoandaliwa na Taasisi ya Uongozi na kukutanisha marais wastaafu na viongozi waandamizi kutoka ndani na nje ya Tanzania.

 Jukwaa hilo lilijadili kwa kina kuhusu rasilimali za Afrika hasa zilizoko juu ya ardhi yaani misitu, maji, wanyama na nyingine kwa lengo la kuhakikisha kunakuwa na usimamizi mzuri kwa ajili ya mabadiliko ya kiuchumi barani Afrika.

 Akisoma maazimio hayo jana, Profesa Andrew Temu, alisema wamekubaliana kwamba lazima kuunganisha nguvu pamoja kwa viongozi wa Afrika ili kufanikisha jitihada za kulinda rasilimali hizo.

 “Tukae kwa pamoja na kuona namna ya kusimamia vizuri maji na rasilimali nyingine na tutumie sheria zilizopo kupambana na rushwa, tuwe na hasira chanya kuhakikisha viongozi wanasimamia rasilimali zetu,”alisema Profesa Temu.

Pia alisema pamoja na kwamba matatizo ya mazingira na mabadiliko ya tabia nchi yanatokea kiulimwengu, lakini bado nchi mojamoja zinatakiwa kuyashughulikia kwani yanaathiri uchumi na nchi haziwezi kusonga mbele bila kukabiliana nayo.

 “Tutambue kwamba sisi Waafrika ndio tunamiliki rasilimali hizi na hapo ndipo tutakapoweza kupanga mikakati ya matumizi bora badala ya kuwaachia wenzetu wa nje.

“Wanyama milioni moja wako mbioni kupotea, tuungane pamoja kulinda rasilimali zetu kupunguza majanga na tutumie nishati mbadala badala ya kuni na mkaa,”alisema.

Maazimio mengine ni kuhamasisha uelewa katika kusimamia rasilimali kwa kuhakikisha wananchi na viongozi wanalielewa tatizo kwa undani ili watawale kwa manufaa ya kizazi cha sasa na cha baadaye.

 Azimio lingine ni kuboreshwa kwa mitaala ya elimu ili misingi ya utawala bora na usimamizi wa rasilimali iwe ni sehemu ya masomo yanayotolewa shuleni kujenga kizazi kitakachokuwa na utawala bora wa rasilimali hizo.

MKAPA

 Akifunga mkutano huo Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, alihimiza elimu iendelee kutolewa na kupeana taarifa sahihi juu ya usimamizi wa rasilimali ili kuziepusha nchi za Afrika na uharibifu wa mazingira.

 “Naamini tunaweza kwa pamoja kulinda rasilimali zetu katika bara hili kwa kutoa elimu na kupeana taarifa sahihi, tuanze na watu wa chini na hawa wanaweza kusaidiwa na watu wa juu wakaweza kufanya vizuri zaidi,”alisema Mkapa.

Kwa upande wake Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, alisema kunatakiwa kuwe na urali kati ya matumizi na uendelezaji wa rasilimali jadidifu.

 Marais wengine wastaafu waliohudhuria jukwaa hilo ni Thabo Mbeki (Afrika Kusini), Olusegun Obasanjo (Nigeria), Henry Rajaonarimampianina (Madagascar).

 Viongozi hao kwa pamoja walisema Bara la Afrika lina rasilimali za kutosha lakini changamoto inayolikabili ni namna ya kushughulikia matatizo yatokanayo na uharibifu wa mazingira. 

Hivyo walipendekeza jitihada za serikali za kusimamia rasilimali zijielekeze katika malengo ya muda mfupi na mrefu, serikali ziwekeze katika tafiti na kuangalia namna bora ya kuhimiza matumizi ya nishati mbadala kuepuka ukataji wa miti.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles