24.8 C
Dar es Salaam
Friday, September 29, 2023

Contact us: [email protected]

Wakili adai Kabendera Kapooza akiwa gerezani

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

WAKILI anayemtetea Mwandishi wa habari za uchunguzi, Erick Kabendera (39), Jebra Kambole, ameieleza mahakama kwamba afya ya mteja wake imetetereka, aliumwa ghafla gerezani akapooza miguu na kushindwa kutembea kwa siku mbili.

Kambole alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi, Janeth Mtega wakati kesi hiyo ilipokuwa ikitajwa mbele yake kwa sababu Hakimu Augustine Rwizile anayesikiliza kesi hiyo kuwa na udhuru.

Akiiwakilisha Jamhuri, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika wanaomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Kabla ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, Wakili Jebra alidai ana hoja mbili za kuwasilisha mahakamani kuhusu mteja wake.

Alidai hoja ya kwanza anaomba upelelezi ukamilike haraka na hoja ya pili kuhusu afya ya mteja wake.

“Mheshimiwa Agosti 21 mteja wetu aliumwa ghafla akiwa gerezani, mpaka leo anapata shida ya kupumua ukifika muda wa usiku.

“Agosti 21 hiyo hiyo mteja wetu alipooza miguu yote miwili akashindwa kutembea kwa siku mbili, akaishiwa nguvu, kama mawakili na ndugu zake hatujui anachoumwa.

” Tunaomba mahakama ilielekeze Jeshi la Magereza ili akapimwe sababu hajapata matibabu, tunaomba apelekwe Muhimbili sababu atapimwa kuna vifaa vyote,”alidai.

Akijibu Wakili Wankyo alidai mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa amri yoyote kutokana na mazingira ya kesi isipokuwa atawahimiza Askari Magereza wafuate taratibu zao ili mshtakiwa apate matibabu.

Alidai Magereza wanao utaratibu wao, wako mahakamani wanasikia hoja za wakili wa mshtakiwa hivyo watayafanyia kazi.

Hakimu Mtega alisema mahakama imesikia hoja za pande zote mbili, Hakimu anayesikiliza kesi hiyo atapitia na kutoa uamuzi, aliahirisha kesi hadi Septemba 12.

Kabendera alifikishwa  mahakamani kwa mara ya kwanza, Agosti 5, 2019 akikabiliwa na mashtaka matatu, ambayo ni kuongoza genge la uhalifu, kukwepa kodi na kutakatisha zaidi ya Sh173.2 milioni.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, shtaka la kwanza linalomkabili ni kwamba kati ya Januari mwaka 2015 na Julai 2019 maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam Kabendera na wengine ambao hawapo mahakamani anadaiwa alitoa msaada kwenye genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia fedha.

Katika shtaka la pili, anadaiwa kukwepa kodi, ambapo kati ya Januari, 2015 na Julai 2019 maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam bila sababu za msingi alikwepa kulipa kodi Sh 173,247,047.02 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Katika shtaka la tatu la kutakatisha fedha, inadaiwa katika tarehe hizo mshtakiwa alitakatisha kiasi hicho cha fedha huku akijua zimetokana na zao la kusaidia genge la uhalifu na kukwepa kodi.

Kabendera alifikishwa  mahakamani kwa mara ya kwanza, Agosti 5, 2019 akikabiliwa na mashtaka matatu, ambayo ni kuongoza genge la uhalifu, kukwepa kodi na kutakatisha zaidi ya Sh173.2 milioni.

Mshtakiwa alisomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Augustine Rwizile.

Hata hivyo, mshtakiwa Kabendera hakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo isipokuwa kwa kupata kibali kutoka kwa DPP.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,750FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles