30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 30, 2023

Contact us: [email protected]

Viongozi wa Dini waipongeza Serikali kwa kupunguza vifo vitokanavyo na UKIMWI

*Yashauri kuondolewa kwa dirisha maalum la WAVIU kwenye vituo vya afya kupunguza unyanyapaa

*Yataka elimu ya UKIMWI ifike kwa viongozi wa dini ngazi za chini 

Na Nadhifa Omary, Morogoro

Viongozi wa Dini nchini wameipongeza Serikali kwa jitihada inazochukua katika kutoa elimu ya matumizi sahihi na endelevu ya dawa za kufubaza makali ya Virusi Vya UKIMWI (ARV) kwa watu wanaoishi na maambukizi na kupunguza vifo vitokanavyo na UKIMWI nchini.

Wito huo umetolewa mjini Morogoro Ijumaa Juni 10, 2022 na Fr. Charles Kitime katika kikao cha Matibu Wakuu na Wataalam kutoka Jukwaa la Taasisi Miavuli ya Dini nchini ambapo ameipongeza serikali kupitia Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania(TACAIDS) kwa kazi kubwa ambayo imefanyika kwani imesaidia kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na UKIMWI.

⦁ Katibu Mkuu wa Baraza la Maasikofu Tanzania (TEC), Fr. Charles Kitime akielezea Mkakati wa utoaji elimu ya VVU kwa jamii kupitia Viongozi wa Dini kuanzia ngazi ya Taifa katika ngazi ya chini kwa kuwa viongozi wa dini wa ngazi ya chini ndio wanajamii kubwa na itasaidia kufikia watu wengi kwa wakati mfupi.

Fr. Kitime amesema hatua inayochukuliwa na TACAIDS hasa ya kushirikisha viongozi wa dini katika elimu ya Mwitikio wa UKIMWI nchini ni jambo la kupongezwa huku akihimiza elimu hiyo kutoishia kwa viongozi wa ngazi ya juu pekee.

“Elimu hii inayotolewa kwa viongozi wa dini wa kitaifa basi ifikishwe kwa viongozi wa dini wa ngazi ya chini walioko Mikoani, Wilayani kote nchini kwakuwa huko ndio kuna jamii kubwa ambayo pia inaumuhimu wa kupata elimu hii ya kujikinga na maambukizi ya VVU na viongozi hao wanajua lugha sahihi ya kutumia kwa jamii husika,” amesema Fr. Kitime.

Ameongeza kuwa kwa elimu waliyoipata tangu kuanzishwa kwa TACAIDS kupitia vikao mbalimbali vinavyoendelea kufanyika kwa kushirikiana na jukwaa la taasisi za miavuli ya dini wanauwezo mkubwa wa kutoa elimu hiyo kwa walengwa, huku wakiomba kupatiwa  fedha kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli hiyo kuanzia ngazi ya chini.

“Kazi inayofanyika ni nzuri, niishauri serikali kuangalia namna nyingine ya kubadilisha mfumo katika vituo vya afya hasa katika huduma za Mwitikio wa UKIMWI, pindi mtu anapokwenda kupata huduma kusiwe na dirisha maalum kwa ajili ya watu wanaoishi na VVU ili kupunguza unyanyapaa kwa WAVIU,” amesema Fr. Kitime.

Katibu Mkuu Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Sheikh Nuhu Mruma akijadili namna sahihi ya ushiriki wa viongozi wa Dini katika utoaji Elimu katika Mwitikio wa UKIMWI kwa jamii nchini.

Nae Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Sheikh Nuhu Mruma amesisitizia umuhimu wa mafunzo ya uelimishaji namna ya kujikinga na maambukizi ya VVU kuelekezwa kwa viongozi wa dini wa ngazi ya Mkoa ikiwa ni pamoja na kuwapatia machapisho ya habari,elimu na mawasiliano kwa kwa ajili ya kufundishia, viongozi wa dini ngazi ya chini ndio wanaoishi na watu wengi.

“Viongozi wa dini ngazi ya chini wapatiwe mafunzo ya uelishamishaji namna ya kujikinga na maambukizi ya VVU kisha wapatiwe vipeperushi pamoja na dhana za kufundishia ili elimu hiyo waweze kuitumia kuwafikisha kwa walengwa, kule ndiko jamii kubwa iliko,” amesema Sheikh Mruma.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu Jumuiya ya Makanisa ya Kipentekoste Tanzania(CPCT), Mch. Ezra Msanya akichangia katika mawasilisho ya maazimio yaliyofikiwa katika kikao chao cha awali likiwamo la Taasisi za Dini kupatiwa fedha za Mwitikio wa UKIMWI.

Aidha, amefafanua kuwa kuna umuhimu wa kendelea kutumia “Tanzania Interfaith Platform” ambacho ndio chombo kinachowaunganisha wote na tayari kuna mifumo sahihi ya uratibu, utekelezaji na ufuatiliaji wa majukumu hata fedha zikipatikana kuna kuwa hakuna ubabaishaji.

“Niishukuru TACAIDS kwa kuendelea kushirikisha viongozi wa dini katika kila hatua, kuanzia mafunzo na kutujengea uelewa ambao kwa sasa ni hatua kubwa imefanyika kwani hata viongozi wa dini walifanikiwa kupata mafunzo ya mwitikio wa UKIMWI kila wakikutana na waumini hawaachi kutoa elimu hiyo.

“Katika mpango mkakati wa nchi unaoandaliwa sasa hakikisheni inaangalia namna ya kufikia jamii kubwa ikiwa ni pamoja na jumbe ambazo miavuli ya dini imeshiriki kuziandaa pia hata usambazaji wake ziwafikie walengwa, zisiishie katika ngazi za juu.

“Mwisho wa siku tunahitaji kuwa na Tanzania isiyokuwa na maambukizi mapya ya VVU, unyanyapaa na vifo vitokanavyo na UKIMWI,” amesema Sheikh Mruma.

Asna Shendui Mtendaji Mkuu Tanzania Iterfaith Platform akiwasilisha maazimio yaliyofikiwa na kikao cha wataalamu kwa Makatibu wakuu katika kikao kilichofanyika Mkoani Morogoro Juni 10, 2022.

Awali, akiwasilisha maazimio Umoja Mtendaji Mkuu wa Interfaith Platform(TIP), Asna Shendui amesema imefika wakati sasa wadau wanaofadhili shughuli za UKIMWI nchini kama vile CDC, USAID kuziamini Taasisi za dini kuwa na uwezo wa kusimamia fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kuwa taasisi hizo zina mifumo imara kuanzia ngazi ya chini hadi Taifa, miongozo, taratibu na watalaam wanaoweza kutekeleza afua za VVU zinazotekelezwa katika taasisi husika ikiwa ni pamoja na kukaguliwa.

Mratibu wa Asasi za Kiraia kutoka TACAIDS, Mary Manzawa akizungumza na wadau wa kikao hicho kilichofanyika Juni 10, 2022 mkoani Morogoro.

Upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Jumanne Issango amewashukuru viongozi wa dini kwa mchango wao wanaoendelea kuutoa katika jamii kupitia waumini na wataalam kwa ushirikiano wao ambao wamekuwa wakiutoa kwa TACAIDS.

Amesema ni jambo jema kwa wataalam ambao wameweza kukaa kwa siku mbili na kuweza kupata mapendekezo ambayo ni mazuri na yenye mwelekeo wa kutatua changamoto katika Mwitikio wa UKIMWI pamoja na kuleta mwelekeo mzuri wa serikali kushirikiana na taasisi za dini katika Mapambano dhidi ya VVU na kwamba tume itanedeleza ushirikiano huo

“TACAIDS itaendelea kushirikiana na majukwaa haya kuendelea kuangalia ni namna gani tuwaweza kushirikiana ikiwa ni pamoja na kuzingatia maazimio yenu, tukikaa na wadau wa maendeleo tutayajadili haya pia hata kwenye mkakati wa tano wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI hatuwezi kuacha hatua hizi nzuri ambazo tumeshazianza,” amesema Isango.

Picha ya pamoja ya Katibu wakuu kutoka Taasisi za Dini nchini za Baraza la Maaskaofu Tanzania (TEC), Baraza la Waislamu Tanzania BAKWATA,Jumuiya ya Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT), Jumuiya ya Makanisa ya Kisabato Seventh Day Adventist (SDA),Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) wataalam kutoka Taasisi za Dini na Wawakilishi kutoka TACAIDS.
- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles