27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Wahifadhi wastaafu waagwa, waliobaki waaswa kupendana

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Prisca Lwangili amewaasa wahifadhi wa misitu nchini kujenga umoja, mshikamano na kupendana kazini ili waje kuwa na mwisho uliotukuka.

Lwangili ameyasema hayo Ijumaa Juni 10, 2022 kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Francis Michael (mgeni rasmi) wakati wa hafla ya kuwaaga wahifadhi misitu wastaafu 61 wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – TFS katika Jengo la Mkuki, Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, Lwangili amesema, ni heshima kubwa kuwaaga wenzao hao ambao wamefikia kikomo cha utumishi wao TFS baada ya kuitumikia kwa miaka mingi huku wakiacha alama ya utumishi uliotukuka unaoifanya TFS kuonekana inavyoonekana hivi leo.

“Nikiwatazama wastafu hawa naona bado wana nguvu na afya njema, hawa watu wana ujuzi na wamefanya TFS kwa miaka 11 ya uhai wake na tunaona matokeo mazuri walioacha, naamini kuna kanzu data yao watumieni watu hawa.

“Mimi kabla ya kuwa Wizara hii nilikuwa utumishi, TFS ni moja kati ya wakala zinazofanya vizuri sana, tuna Wakala 27 zilizoanzishwa kufanya Serikali iongeze mapato, kuna nyingine zinasuasua lakini TFS mko vizuri sana hii maana yake kila mmoja wenu ameshiriki kuifanya TFS hii, na si Kamishna wa Uhifadhi pekee, hongereni kwa hili,” anasema Lwangili.

Aidha, Lwangili ametoa wito kwa wastaafu hao wakirudi uraiani kuendelea kuwa mabarozi wazuri wa uhifadhi na kuendelea kushirikiana na jamii huku akiwaasa wahifadhi wanaobaki kutambua kuwa kuanza ajira maana yake kuna hitimisho la ajira, na hivyo wajipange.

Lwangili anawaasa watumishi waliopo makazini kufanya kazi kwa umoja, mshikamano na upendo kwa kile alichosema; “Ukimpenda mwenzako huwezi kumpiga majungu, huwezi kumuonea wivu zaidi utajenga ukaribu naye ili kile unachokiona kwake halafu kinakupa wivu ujifunze na wewe kikusaidie, na kila mmoja anapokuwa yuko vizuri kwenye eneo fulani, tunatengeneza taasisi yenye mshikamano na upendo na hivyo manung’uniko yatapungua,” amesema.

Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi – TFS, Prof. Dos Santos Silayo amewahakikishia wahifadhi wastaafu hao kuwa TFS itaendelea kushirikiana nao katika masuala mbalimbali pale itakapobidi licha ya kuwa wamemaliza muda wao wa kazi.

“Napenda kuwapongeza kwa utumishi wenu uliotukuka hadi kufikia siku ya leo, nipende kuwahakikishia kuwa sisi mnaotuacha kazini tunaamani, mmetuachia misingi mizuri na tutaendelea kuhakikisha taasisi hii inafikia malengo iliyokusudia,” amesema Prof. Dos Santos Silayo.

Mhifadhi misitu mkuu mstaafu, Valentino Msusa anasema ni mstaafu aliyestaafu kwa heshima pekee ndio hufanyiwa sherehe za kuagwa kiheshima na kuwataka wahifadhi waliobaki kuzingatia sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ya Serikali na kumuomba Mungu ili wawe na mwisho mwema.

Wahifadhi misitu wastaafu walioagwa ni wale waliostaafu mwaka huu wa fedha 2021/2022.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles