28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 1, 2024

Contact us: [email protected]

Viongozi wa dini wahamasisha wananchi chanjo saratani ya kizazi

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Wakati kampeni ya kitaifa dhidi ya chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi ikitarajiwa kuanza, viongozi wa dini wamewataka wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao wenye umri kati ya miaka 9 hadi 14 waweze kukingwa na ugonjwa huo.

Tafiti zinaonyesha saratani ya mlango wa kizazi inaweza kudhibitiwa kwa wasichana kabla hawajapata maambukizi kwa kupatiwa dozi moja ya chanjo kabla hawajaanza vitendo vya kujamiiana vinavyoweza kusababisha maambukizi.

Akizungumza Aprili 20,2024 wakati wa mkutano kuhusu chanjo ya kuzuia saratani ya shingo ya kizazi Naibu Katibu Mkuu Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Chesco Msaga, amesema watoto wakiweza kuokolewa na kuepushwa na saratani hiyo jamii kubwa itaokolewa.

Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dk. Ntuli Kapologwe, akizungumza wakati wa mkutano kuhusu chanjo ya kuzuia saratani ya shingo ya kizazi, Dar es Salaam.

Mkutano huo uliandaliwa kwa ushirikiano wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na Shirika lisilo la kiserikali TIP linaloundwa na taasisi nne za kidini ambazo ni Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) na Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar (MoZ).

“Hili ni tatizo kubwa siyo tu hapa nchini bali ulimwengu mzima, viongozi wa dini tunakutana na watu wengi kwenye nyumba za ibada na sehemu nyingine tuliona tuwe na uelewa sahihi ili kuwasaidia waumini wetu kuhamasika zaidi kushiriki katika chanjo hii,” amesema Pardi Msaga.

Askofu wa KKKT Dayosisi ya Morogoro, Jacob Mameo, akizungumza wakati wa mkutano kuhusu chanjo ya kuzuia saratani ya shingo ya kizazi, Dar es Salaam.

Askofu wa KKKT Dayosisi ya Morogoro, Jacob Mameo, amesema wanaungana na Serikali kuhakikisha wanahamasisha watu wapate chanjo hiyo.

“Saratani hii inakuja kwa kasi na inatishia uhai wa watoto wetu, tunaungana pamoja kuhakikisha kila mmoja anaona umuhimu wa jambo hili. Watoto ndio taifa la leo hivyo, tunawashawishi Watanzania wote kila mmoja apeleke watoto kwenye chanjo,” amesema Askofu Mameo.

Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar, amesema elimu ya chanjo hiyo ikitolewa nchini kuhusu chanjo hiyo watapatikana watu wenye afya bora watakaosaidia kuleta maendeleo ya nchi.

“Ukikosa kujikinga utaharibikiwa, lazima ujikinge uwe salama zaidi hivyo, kinachotakiwa watu wahamasike na kujitokeza wapatikane watoto wenye afya watakaosaidia kuendesha gurudumu la taifa,” amesema Sheikh Omary.

Mkurugenzi wa Kinga, Dk. Ntuli Kapologwe, amesema wanatarajia kuchanja wasichana 4,841,298 wenye umri wa miaka 9 hadi 14 walioko shuleni na nyumbani.

“Serikali imechukua jitihada za makusudi kuhakikisha kuwa inawalinda wasichana kwa kuwapatia chanjo ya kudumu wakiwa katika umri mdogo, sote tuna wajibu wa kuhakikisha walengwa wote ambao hawajapata chanjo wanapata kulingana na ratiba,” amesema Dk. Kapologwe.

Kwa mujibu wa Dk. Kapologwe, chanjo hiyo ambayo sasa itatolewa dozi moja badala ya mbili ni salama imethibitishwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) na Wizara ya Afya kupitia Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) na Kamati ya Kitaalam ya masuala ya Chanjo (TAITAG).

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la TIP, Asina Shenduli, amesema watashirikiana na Serikali kuhakikisha elimu juu ya chanjo hiyo inatolewa na viongozi wa dini kupitia fursa mbalimbali ikiwemo nyumba za ibada.

“Sote tunatambua umuhimu wa viongozi wa dini, wana sauti na sauti zao zinasikika, zinaaminika na kuheshimika hivyo, tushirikiane na Serikali na Unicef kuhakikisha elimu inatolewa,” amesema Shenduli.

Takwimu zinaonyesha kuwa saratani ya mlango wa kizazi inaongoza kuliko saratani zingine nchini ambapo utafiti wa NIMR wa 2019/20 hadi 2021/22 ulionyesha watu 17,757 waliugua saratani na kati yao asilimia 22.5 walikuwa na saratani ya mlango wa kizazi huku mikoa iliyoongoza ikiwa ni Kilimanjaro, Dar es Salaam na Mwanza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles