23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

VIGOGO 12 NSSF WAACHISHWA KAZI

*Ni wale waliosimamishwa kwa ubadhirifu

*Nafasi zao kutangazwa upya, bodi kufuatilia


Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM

BODI ya Wadhamini ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), imetangaza kuwaachisha kazi vigogo 12 wa shirika hilo.

Vigogo hao walisimamishwa kazi Julai, mwaka jana ili kupisha uchunguzi kuhusu tuhuma za ubadhirifu, matumizi mabaya ya ofisi na kutofuata kanuni, sheria na taratibu katika uwekezaji, usimamizi wa miradi, manunuzi ya ardhi na ajira.

Taarifa ya NSSF iliyotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu, Profesa Godius Kahyarara, ilieleza kuwa hatua ya kuwachisha kazi vigogo hao, imefikiwa na Bodi ya Wadhamini wa NSSF iliyoketi katika kikao chake cha 72 cha kawaida kilichofanyika Juni 30, mwaka huu.

Walioachishwa kazi ni Yacob Kidula (Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Miradi), Ludovick Mrosso (Mkurugenzi wa Fedha), Chiku Matessa (Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala) na Sadi Shemliwa (Mkurugenzi wa Udhibiti, Hadhara na Majanga).

Wengine ni Pauline Mtunda (Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Mahesabu ya Ndani), Crescentius Magori (Mkurugenzi wa Uendeshaji), Amina Abdallah (Meneja Utawala), Abdallah Mseli (Meneja wa Uwekezaji), Mhandisi John Msemo (Meneja wa Miradi).

Mbali na hao pia wapo Wakili Chedrick Komba (Meneja Kiongozi – Mkoa wa Temeke),  Mhandisi John Ndazi (Meneja Miradi) na Ramadhani Nasibu  (Meneja Mkuu Usalama).

 

MATOKEO YA UCHUNGUZI

Taarifa hiyo ya NSSF ilieleza kuwa kutokana na uchunguzi uliofanywa, bodi ilibaini watumishi hao kwa namna moja au nyingine ama kwa uzembe uliopindukia au makusudi, walishiriki kufanya ubadhirifu, matumizi mabaya ya ofisi na kutofuata kanuni, sheria na taratibu katika uwekezaji, usimamizi wa miradi, manunuzi ya ardhi na ajira.

“Watumishi hao wameliingiza shirika katika hasara, madeni na upotevu fedha. Kwa mfano, uchunguzi umebaini kuwa jumla ya Sh bilioni 12 zilikuwa zimetumika katika miradi ambayo bado haijaanza.

“Matumizi ya jumla ya Sh bilioni 43 katika mradi ambao ulikwishaanza na baadae kusitishwa; shirika kuingia mikataba mibovu ambayo inawanufaisha zaidi wabia pamoja na kuwa na gharama kubwa ambazo haziendani na uwezo wa mtiririko wa fedha wa shirika na kusababisha tatizo la ukwasi; shirika kushindwa kukusanya zaidi ya Sh bilioni 20 kutokana na utoaji wa mikopo isiyofuata taratibu.

“Shirika kufanya manunuzi ya viwanja bila kufuata utaratibu na kuna ambavyo vimevamiwa na ujumla wa viwanja vyenye matatizo vyenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 18, shirika kutekeleza miradi bila kufanya upembuzi yakinifu wa uhakika au kutokufanya kabisa na kusababisha shirika kutekeleza miradi ambayo gharama zake huongezeka zaidi ya mara tatu wakati wa utekelezaji na mwingine kuongeza gharama za miradi bila kupata idhini ya mamlaka husika,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo ya uchunguzi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, bodi bado inaendelea kufuatilia urejeshwaji wa fedha hizo kwa kuzingatia taratibu stahiki na kusitisha miradi yote yenye mikataba mibovu.

Pamoja na hali hiyo, bodi hiyo ya wadhamini ya NSSF imeuhakikishia umma kwamba hali ya mfuko kwa sasa ipo salama kwa maana ya kuweza kutimiza majukumu yake kwa wanachama na wafanyakazi wote.

“Mwenendo wa ukwasi wa shirika umeimarika sana kutoka Sh bilioni 12 Aprili, 2016 na kufikia Sh bilioni 354 Juni, 2017, hali ambayo imeliwezesha shirika kulipa malimbikizo ya madeni mbalimbali. Pia makusanyo ya michango ya wanachama yameongezeka kufikia wastani wa Sh bilioni 60 kwa mwezi kutoka Sh bilioni 42 kwa mwezi,” imeeleza taarifa hiyo.

Ilieleza kuwa itaendelea kusimamia majukumu yake ipasavyo ikiwa ni pamoja na kusimamia nidhamu kwa watumishi, udhibiti matumizi mabaya ya fedha, kufuata kanuni, sheria na taratibu katika uwekezaji, usimamizi wa miradi na ajira.

Aidha, kutokana na kuachishwa kazi wafanyakazi hao, bodi imeamua kutangazwa kwa nafasi zote za ajira zilizoachwa wazi.

 

RIPOTI YA CAG

Vigogo hao waliosimamishwa kazi Julai 20, mwaka jana, inaelezwa kuwa walihusishwa na ubadhirifu huo uliofanywa kupitia miradi ya usimamizi wa nyumba za kuuza zilizopo Mtoni Kijichi, Dar es Salaam, unaokadiriwa kufikia Sh bilioni 137.7.

Katika ripoti ya mwaka 2015/16 ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuhusu ukaguzi wa mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha 2014/2015, imebainika kuwa ulikuwapo ukiukwaji mkubwa wa taratibu katika miradi hiyo.

Taarifa hiyo ya CAG inaeleza katika ukurasa wa 165 na 166 kuwa Juni 30 mwaka 2015, Sh bilioni 79 za shirika hilo  zilitumika katika ujenzi wa nyumba hizo ambazo ziliamuriwa kuuzwa ndani.

Uamuzi huo ulitolewa badala ya kufuata maelekezo ya wasimamizi kwa kutumia benki au makampuni ya mikopo kama ilivyoelekezwa katika kanuni namba 13 ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) na mwongozo wa uwekezaji wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Katika maoni yake kuhusu mradi huo, ofisi ya CAG iliishauri menejimenti ya NSSF kuzingatia sheria, kanuni na maelekezo yanayotolewa na wasimamizi wake.

“Kitendo chochote cha kutofuata maagizo kinatakiwa kuwasilishwa kwa maandishi kwa mdhibiti wa sekta na kukubaliana muda uliopangwa kwa ajili ya kufuatwa,” ilisema sehemu ya ripoti hiyo.

Ukiukwaji mwingine wa sheria na taratibu unaotajwa kufanywa na vigogo hao, ni ununuzi wa ardhi bila ushindani kutoka kwa muuzaji mmoja, kwa gharama ya Sh bilioni 15.16.

Taarifa hiyo ya CAG inaeleza kuwa NSSF ilipanga bajeti ya Sh bilioni 1.6 kwa ununuzi wa kiwanja kupitia zabuni za ushindani.

“Hata hivyo, ilitumia chanzo kimoja katika ununuzi wa kiwanja kilichogharimu Sh bilioni 15.16. Nimegundua kwamba Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma haikujulishwa, kinyume cha kanuni namba 87 ya mwaka 2013 ya mamlaka hiyo inayohitaji kuwasilishwa taarifa za mkataba wa tuzo kwake, ndani ya siku saba kuhusu mchakato wa ununuzi endapo chanzo kimoja kilitumika,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo ya CAG.

CAG aliishauri menejimenti ya NSSF kuzingatia mpango wake wa bajeti na kanuni za ununuzi wa umma za mwaka 2013, kuhakikisha ununuzi unafanyika katika ushindani ili kupata huduma kwa bei nafuu.

Ripoti hiyo ya ukaguzi ya CAG alieleza namna NSSF lilivyoingia ubia na Kampuni ya Azimio Housing Estate kuanzisha kampuni maalumu kwa jina la Hifadhi Builders Ltd.

Katika mkataba huo, Azimio Housing Estates inatatakiwa kuendeleza ekari 20,000 za ardhi zilizopo Kigamboni ambako kwa hatua ya awamu itaaanza na ekari 300.

“Katika ubia huu, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii linamiliki asilimia 45 ya hisa wakati Azimio Housing Estate inamiliki asilimia 55. Jumla ya gharama za mradi ni Dola za Marekani milioni 653.3.44.

“Ukaguzi wa hatimiliki umeonyesha kuwa Azimio Housing Estate inamiliki viwanja viwili, kiwanja chenye hatimiliki namba 81828 chenye ukubwa wa hekta 1.98 na chenye hatimiliki namba 105091 chenye ukubwa wa hekta 114.11 ambavyo vyote vinapatikana katika eneo la Rasi Dege,” ilieleza taarifa ya CAG.

Pamoja na hali hiyo, alisema kuwa hajaweza kupatiwa hatimiliki za ardhi ambayo Azimio aliahidi kutoa kama uchangiaji wa mtaji hali ambayo NSSF ililipa asilimia 20 ya fedha kama mtaji ambazo zilikuwa kwenye hatari ya kupotea.

 

DENI LA BIL. 723.22/-

Katika taarifa hiyo ya CAG, ilielezwa kwamba NSSF lilikopesha Serikali katika miradi yake mbalimbali. Hata hivyo Serikali imekuwa hailipi madeni yake kwa muda mrefu.

Hali hiyo imekuwa ikisababisha kuongezeka kwa limbikizo la riba na adhabu hadi kufikia asilimia 39 ya salio la Sh bilioni 729.22 hadi kufikia Juni 2014.

 

WAFANYAKAZI NA MADENI

Shirika hilo lina utaratibu wa ndani wa kutoa mikopo kwa wafanyakazi wake. Ukaguzi wa mikopo ya wafanyakazi hao umeonyesha kiasi cha Sh milioni 827.98 bado kinadaiwa kwa wafanyakazi ambao si waajiriwa tena wa NSSF.

Kutokana na hali hiyo, mwanzoni mwa mwaka 2016 Rais Dk. John Magufuli alitengua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhani Dau na kumteua kuwa balozi na baadye kumpangia kituo cha kazi nchini Malaysia.

Hata mwanzoni mwa Machi mwaka jana, mrithi wa Dk. Dau, Dk. Carine Wangwe ambaye aliteuliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, uteuzi wake ulitenguliwa na Ofisi ya Rais Ikulu katika kile kilichoelezwa kuwa ulikiuka taratibu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles