ANAYEDAIWA KUTOBOLEWA MACHO NA ‘SCORPION’ ATELEKEZA FAMILIA

0
549

Na FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM


UKISTAAJABU ya Mussa utayaona ya Firauni. Ndivyo unaweza kusema baada ya kuibuka madai kwamba Said Mrisho anayedaiwa kutobolewa macho na Salum Henjewele maarufu kama ‘Scorpion’ ametelekeza familia yake.

Inadaiwa kuwa mke wa Mrisho anayetambulika kwa jina la Wastara Sudi, hivi sasa hana maisha ya raha katika ndoa yake baada ya mumewe huyo   kumtelekeza na watoto wake pacha wenye umri wa mwezi mmoja sasa.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Wastara alidai kuwa mume wake   alimtelekeza siku chache zilizopita licha ya kujifungua watoto hao, kwa kile alichoeleza kuwa yeye na ndugu zake walimwibia Sh milioni mbili.

Alisema mume wake alimkana mbele ya Ofisa wa Ustawi wa Jamii, akidai kuwa alikuwa akimletea wanaume ndani ya nyumba na kwamba alikuwa akihitaji nyaraka zake tu na si vinginevyo.

“Mrisho amesema hahitaji tena kuendelea na mimi akidai kuwa mimi ni mwizi, nimemwibia Sh milioni mbili pamoja na nguo,  hivyo hataki kuendelea kuishi na mimi tena.

“Kuhusu watoto, alisema angenipangishia nyumba na kulipa kodi ambayo inatarajia kuisha Oktoba mwaka huu.

“Hivyo kasema hayuko tayari kuendelea na mimi na hivyo amenipa talaka kwa maneno.

“Amewavuruga watoto wa mwezi mmoja kwa kuwapiga kama watu wazima… tangu mwezi wa Ramadhani, Mrisho aliamua kuoa mke mwingine.

“Kwa namna nilivyomsaidia hakuwa mtu wa kunifanyia hivi, kwa sababu nimemlea, nimehangaika naye nikiwa na mama yangu. Tumejinyima kwa ajili yake ili tu yeye ale vizuri, lakini amebadilika ghafla,” alidai Wastara.

Alidai kuwa kwa sasa mume wake na mke wake mpya wanaishi Tabata Barakuda huku akiwa amechukua vitu vyote vya thamani na kumwacha na vitu vya zamani.

Wastara alisema mara baada ya tukio la mumewe kuumizwa na kutobolewa macho na ‘Scorpion’ walipewa Sh milioni 12,  pikipiki tano na bajaji mbili, vitu ambavyo amedai kuwa Mrisho amekuwa akitaka kubaki navyo vyote.

“Watoto nimewaacha tangu asubuhi na dada yangu Mabibo Hosteli na maziwa ya kopo kwa sababu tangu asubuhi nahangaika tu, hivyo nimeachana naye akiwa amefuatana na dereva wa bodaboda.

“Hadi sasa nimeripoti Kituo cha Polisi Tabata  kupitia dawati huru kisha twende mahakamani, lakini yeye anasema nilichokuwa nahitaji ni nyaraka za mali jambo ambalo nililipinga,” alisema Wastara.

Wastara alisema kutokana na hali hiyo aliwasiliana na mama mzazi wa mume wake na kumweleza tukio hilo jambo ambalo hakupendezwa nalo na akashangazwa na kitendo hicho cha mtoto wake.

Alisema kwa sasa mumewe anamtumia fedha za matumizi ya watoto kwa njia ya simu Sh 10,000, fedha ambazo  wakati mwingine huzitoa baada ya malumbano kati yao.

Gezeti hili lilipomtafuta    Mrisho kuzungumzia tuhuma hizo, alisema kuwa ni uongo ambao ulikuwa ukienezwa na mkewe huyo kupitia vyombo vya habari bila ya yeye kuhojiwa.

“Hizi tuhuma zote si za kweli, ila baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikirusha mahojiano bila kunihusisha ilhali mke wangu anaongea uongo.

“Ukweli ni kwamba mke wangu ameniambia kuwa amechoka kuishi na mimi kwenye nyumba tuliyopanga hapa Tabata Maji Chumvi na ametoka hapa sasa hivi na fedha za matumizi nimempatia.

“Jambo kubwa lililopo ni kwamba mke wangu anataka tugawane vitu na mali nilizopewa wakati wa matatizo, anataka bajaji, pikipiki ilhali nilipewa mimi,” alisema.

Kuhusu kuoa mwanamke mwingine, Mrisho alisema si kweli.

Alisema ana mke ambaye alizaa naye mtoto mkubwa kabla hata ya kukutana na Wastara.

“Huyu mwanamke ambaye yeye anadai kuwa naishi naye Tabata Barakuda nimezaa naye watoto wakubwa tu kuliko hawa ambao nimezaa naye, kwa maana ni kabla ya yeye.

“Tena cha kushangaza mke wangu alinilazimisha tufunge ndoa miezi minne iliyopita wakati ambao niliumia, ili aweze kupata haki ya kumiliki mali, hivyo nilifunga ndoa kwa shingo upande,” alisema Mrisho.

Alisema alipoumia alikwenda kuishi ukweni  maeneo ya Mabibo Hosteli ambako aliambiwa kuwa asingeweza kuondoka hapo bila ya kufunga ndoa na mkewe huyo.

“Mke wangu anasema mimi nimewatelekeza watoto, hiyo si kweli.  Mimi nimenunua vitu vya ndani nikampa, hata leo (jana) nimempatia fedha za matumizi Sh 10,000.

“Lakini yeye amekuwa akibadilisha maneno kuwa nawaumiza watoto.

“Kuhusu kung’ang’ania vitu, nafanya hivyo kwa kuwa ni halali yangu, mimi ndiye najua watoto wataisha vipi, lakini yeye hataki hilo na badala yake anataka tugawane, haya ni mambo ya kitoto,” alisema Mrisho.

Akizungumzia madai ya ndugu wa mke wake kusema kuwa anadai mkewe alimwibia Sh milioni mbili, alisema  jambo hilo kwa sasa liko polisi Tabata, hivyo asingeweza kulizungumzia.

Wakati huohuo, kesi ya Mrisho dhidi ya ‘Scorpion’ iliyoko Mahakama ya Wilaya ya Ilala, inatarajiwa kuendelea kusikilizwa kwa kutolewa ushahidi Julai 18, mwaka huu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here