25.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 27, 2023

Contact us: [email protected]

Vifo ajali ya moto Morogoro sasa 89

Waandishi wetu – Dar/Morogoro

MAJERUHI saba kati 32 wa ajali ya lori la mafuta lililoanguka na kulipuka mkoani Morogoro, waliokuwa wakitibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), wamefariki dunia jana.

Kufariki dunia kwa majeruhi hao, kunafanya idadi ya waliopoteza maisha katika ajali hiyo iliyotokea Agosti 10, eneo la Msamvu mkoani Morogoro hadi sasa kufikia 89.

Katika hatua nyingine, hadi jana mchana katika Hospitali ya Rufaa ya Morogoro, kulikuwa na majeruhi 16 ambao walielezwa kuwa wanaendelea vizuri.

Jana asubuhi Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa MNH, Aminiel Aligaesha, alisema kwa sasa wamebaki majeruhi 25 kati ya 46 waliopokewa hospitalini hapo kutoka Hospitali ya Rufaa ya Morogoro.

Alisema kati ya majeruhi hao, 16 wapo katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU) huku wengine tisa wakiendelea kupatiwa matibabu katika wodi maalumu iliyotengwa.

Aligaesha alisema waliofariki dunia jana ni Shabani Maringanya (40), Ramadhani Mdoe (50), Shabani Ayubu  (34), Omary Abdalla Omary (26), Khalif Iddy (26) Aloyce Mponzi (36) na Omary Abdalla (24).

“Idadi ya vifo imeongezeka usiku wa kuamkia leo (jana), majeruhi saba wamefariki dunia. Idadi hiyo imefanya kupoteza majeruhi 21 kati ya 46 waliofikishwa hapa Muhimbili na sasa wamebaki majeruhi 25,” alisema Aligaesha.

Alisema majeruhi waliobaki wanaendelea kupatiwa matibabu na wataalamu wa afya ili kuhakikisha wanaokoa maisha yao na kuwataka Watanzania waendelee kuwaombea.

Aligaesha alisema waliofariki dunia wanasafirishwa kwa gharama za Serikali hadi Morogoro huku wale ambao wanasafirisha mikoa mingine wanatumia gharama zao.

“Utaratibu wa kusafirisha marehemu unafanywa na Serikali, na kama anasafirishwa kwenda Morogoro Serikali inagharamia kila kitu, lakini kama ni mikoa mingine kwa mfano kupeleka Moshi, unatumia gharama zako mwenyewe Serikali inakupa jeneza au sanda,” alisema Aligaesha.

Aliishukuru Serikali kwa kuhakikisha vifaa tiba na vitendea kazi vinapatikana, hasa katika kipindi hiki cha majeruhi wa ajali ya moto.

“Tunaishukuru Serikali kwa kuendelea kuleta vifaa tiba, hatujapungukiwa kabisa, hasa katika kipindi hiki cha majeruhi wa ajali ya moto,” alisema Aligaesha.

Tayari miili zaidi ya 60 imezikwa katika makaburi ya Kola mkoani Morogoro na kwamba yote imechukuliwa vipimo vya vinasaba (DNA) na ambaye anafikiria katika ajali hiyo kuna ndugu yake amefariki, anaweza kufika hospitalini kupimwa na kufananishwa kama vinafanana.

CHUPA ZA DAMU ZAFIKA 500

Katika hatua nyingine, chupa 500 za damu zimekusanywa Muhimbili, kwa lengo la kuwasaidia majeruhi wa moto na wagonjwa mbalimbali waliopo hospitalini hapo.

Ofisa Mhamasishaji Damu kutoka Muhimbili, Dk. John Daniel, alisema hospitali hiyo pekee yake inatumia chupa 120 kwa siku.

Alisema ukiongeza na wagonjwa wanaolazwa katika Hospitali ya Mloganzila, kwa siku chupa 120 hadi 180 zinahitajika.

“Mahitaji ya damu hapa nchini ni makubwa na benki yetu inakabiliwa na upungufu wa damu, hivyo ni vyema jamii ikaona haja ya kujenga mazoea ya kuchangia,” alisema.

Daniel alisema mgonjwa mmoja ambaye ni majeruhi wa moto kwa siku hutumia chupa 10, hivyo ipo haja ya wananchi kujitokeza kila kukicha.

Alisema hadi sasa mwitikio wa wananchi ni mkubwa tofauti na siku za nyuma walipokuwa wakisuasua kuchangia damu.

Daniel alisema wengi wanaofika kuchangia damu wanakosa vigezo kama uzito kilogram 50 na kuendelea pia umri kati ya miaka 18 hadi 65, na wenye magonjwa mbalimbali hawaruhusiwi kuchangia damu.

“Ukiwa huna vigezo unaweza kupata shida ya kiafya, ikiwamo shinikizo la damu na mengineyo,” alisema Daniel.

Alisema pia wamekuwa wakitoa damu kwa wachangiaji ambao wana akiba ya damu na ambao wamepoteza sifa huachwa ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Steven Kebwe alisema miili saba ya majeruhi waliokuwa Muhimbili, imesafirishwa kwenda mkoani humo kwa mazishi.

Alisema miili miwili imechukuliwa na familia zao na kwamba miili hiyo saba imepelekwa Morogoro kwa makubaliano ya familia zao na mawasiliano na Ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo cha Maafa pamoja na Wizara ya Ulinzi.

“Wale marehemu waliofia huko Muhimbili tunafanya taratibu wale watakaowatambua ndugu zao na wanakwenda mikoani watapita hukohuko,” alisema.

Dk. Kebwe akizungumzia suala la upimaji wa vinasaba (DNA), alisema unaendelea kwani wapo ndugu ambao bado wanaendelea licha ya ndugu kujitokeza mmoja mmoja.

Alisema matangazo bado yanaendelea kutolewa kwenye maeneo mbalimbali kwa ndugu ambao wamepotelewa ndugu zao kuendelea kujitokeza ili kufanyiwa vipimo.

Katika hatua nyingine, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) limetoa  Sh milioni 10 kusaidia majeruhi wa ajali hiyo.

Akizungumza jana kwenye Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro, kwa niaba ya Tanapa, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa, Donatus Bayona, alisema wameguswa na janga hilo lililowakumba Watanzania wenzao.

Alisema licha ya mahitaji ya hifadhi kuwa mengi, watawasilisha mahitaji yaliyopo katika hospitali hiyo, kufuatia hospitali hiyo kuwa katikati na njia ya kwenda mikoa mbalimbali na kuona wao kama shirika wanaweza kusaidia vipi kukabiliana na majanga yaliyopo na mengine.

Katika tukio hilo, pia Dk. Kebwe aliishukuru Tanapa  kwa msaada huo utakaoweza kusaidia majeruhi wa ajali hiyo.

Alisema wanakabiliwa na changamoto ya kukosekana vifaa mbalimbali kama monita za kuangalia hali ya mapigo ya moyo yanakwendaje, msukumo wa damu na hewa ya oxygen kwenye mwili na vifaa vingine vya kusaidia mgonjwa kupumua.

Aidha Dk. Kebwe aliongeza kuwa wanatarajia fedha hizo zinazotolewa na wadau mbalimbali kuzielekeza kwenye ununuzi wa vifaa hivyo vya kusaidia wagonjwa. Hata hivyo, Dk. Kebwe alisema wameanzisha akaunti katika Benki ya NMB tawi la NSSF Mkoa wa Morogoro ya kusaidia maafa inayoitwa Morogoro Maafa Akaunti yenye nambari 24910000541

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,211FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles