23.3 C
Dar es Salaam
Sunday, June 16, 2024

Contact us: [email protected]

Mkapa: Rasilimali za SADC bado ziko mikononi mwa wageni

ANDREW MSECHU na NORA DAMIAN

Rais mstaafu Benjamin Mkapa, amesema nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), zinatakiwa kukabiliana na ukiritimba wa mataifa ya magharibi ambayo yamekuwa yakifanya jitihada za kuhodhi rasilimali na masoko ya nchi hizo.

Akizungumza katika mjadala wa umma kuhusu kuboresha ushirikiano Sadc: mafanikio, changamoto na fursa uliofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam jana, Mkapa alisema ni wazi nchi 16 wanachama wa Sadc bado zinakandamizwa na mataifa yaliyozitawala wakati wa ukoloni, ambayo yanaona bado yana haki ya kuhodhi rasilimali na masoko.

“Bado kuna ukandamizaji wa hali ya juu, inaonekana wazi kwamba hata katika hazina ya rasilimali zetu, bado inamilikiwa na mataifa yaliyokuwa makoloni na mataifa yetu bado yanaendelea kuruhusu.

“Iwapo tutaelewa kuwa rasilimali hizi ni ufunguo wa maendeleo kwa siku zijazo, tutahakikisha mataifa yetu yanamiliki rasilimali hizi na tunazibadilisha kwa ajili ya kusaidia kubadilisha maisha ya watu wetu.

“Hii itasaidia kuwaweka watu wetu karibu zaidi, ninajua haitakuwa kama wakati ule wa mapambano ya ukombozi, lakini itakuwa karibu kwa namna tutakavyousimamia ukaribu huu kwa sasa,” alisema.

Alisema katika kusimamia hilo, uongozi wa juu unatakiwa kuimarisha usimamizi na kuweka mikakati maalumu ya kumiliki rasilimali katika kila nchi kwa kuwa kuna soko la zaidi ya watu milioni 300 katika ukanda huo wa Sadc.

Mkapa alisema japokuwa yeye amestaafu na yuko nje ya ofisi kwa miaka 14 sasa, amekuwa akisoma na kufuatilia mambo.

“Naona iwapo tunataka kuendelea hatuwezi kuendelea kuruhusu nchi zilizoendelea kumiliki rasilimali zetu na kubadilisha soko letu kuwa soko lao na kuzuia juhudi za kuanzisha masoko yetu na kumiliki rasilimali zetu.

“Mimi ninaona hii bado ni changamoto. Ukiniuliza kuwa ningefanya nini, kwa kweli niko nje na nina umri wa miaka 14 zaidi tofauti na nilivyokuwa madarakani, lakini ni suala ambalo nililipigania pia,” alisema.

Mkapa alisema katika kusimamia ujenzi wa Sadc iliyo imara, ni lazima kuwe na mipango, utekelezaji na kufanya tathmini ya utekelezaji.

Alisema kwa sasa inaonekana hakuna mpango mkakati unaosimamiwa kikamilifu, ndiyo maana Sekretarieti ya Sadc imekuwa ikihimiza nchi wanachama zijitoe kikamilifu.

“Tumekuwa wazuri wa kuweka mikakati, lakini suala la nini cha kufanya, nani afanye, ufadhili utakuwaje, nani atafanya tathmini, nani ataweka nguvu kubwa zaidi  hakuna, ndiyo maana tumekuwa na vikao vingi kila wakati na tumeongeza vikao hadi viwili kwa mwaka kutoka kimoja,” alisema.

Aliongeza kuwa imefikia hatua viongozi wa Sadc wanafikiria wakiiga na kuweka mambo kama zilivyo nchi zilizoendelea, hata kuiga mfumo na muundo wa Jumuiya ya Ulaya (EU) watakuwa wamefanikiwa.

Alisema ni vyema kukubali kuwa nchi hizi ni tofauti kwa mambo mengi, lakini zinaunganishwa na uhitaji kila mmoja kutokana na rasilimali inayokosekana kwake na kupatikana kwingine.

Mkapa alisema anakumbuka aliwahi kuwa Katibu binafsi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na wakati huo, hasa wakati wa harakati za ukombozi, alijitoa kweli kweli.

Alisema kuwa wakati huo alikuwa akiona jambo haliendi sawa alikuwa akiitisha mkutano hata ndani ya saa 24 na alihakikisha mambo yote yanakwenda.

Mkapa alisema kwa sasa bado inaonekana mwamko wa wananchi kuhusu Sadc uko chini, hivyo ni vyema kuhakikisha kunakuwa na mkakati wa kuifanya iwe ya watu, kwa kutoa elimu kwa umma na kuuelewesha kuhusu umuhimu wa uwepo wake na faida zake kwa wananchi kwenye nchi wanachama.

VIJANA

Akizungumzia kuhusu mchango wa vijana, Mkapa alisema anaona wengi hawaelewi uhalisia wa mapambano ya ukombozi na hawajapata taarifa za kutosha kuhusu mapambano hayo, kwa hiyo bado wengi hawajajua umuhimu wa Sadc na namna vijana wa wakati huo wa mapambano walivyochangia kuleta ukombozi.

Alisema ni wazi idadi kubwa ya watu katika Sadc kwa sasa ni vijana ambao wanatakiwa kueleweshwa namna wanavyoweza kutumia jumuiya hii na kutumia teknolojia kwa manufaa, kuliko kukubali kuzubaishwa na mitandao ya kijamii.

“Ni lazima tuhakikishe vijana wanatambua fursa zilizopo Sadc, tuwajengee uwezo na kuhakikisha kuwa wanaajirika au wanaweza kujiajiri. Katika hili, tuhakikishe mfumo wetu wa elimu unawaandaa na kuwapa stadi ambazo zitawanufaisha na kuwafanya kuwa watu muhimu katika kusimamia rasilimali na kuziendeleza,” alisema.

Mkapa alisema iwapo hakutakuwa na kipaumbele maalumu cha kuwafanya vijana wachangamkie fursa katika uchumi wa kidigitali, itakuwa kikwazo katika kufikia malengo ya kikanda.

Alisema hayo hayawezi kutokea hivi hivi, bali kwa kuwa na Serikali zinazoipa fursa ya kuzalisha ajira, kwa kuweka sera na sheria zinazosimamia eneo hilo, kwa kufanya tathmini ya kina kuhusu aina ya ajira zinazotakiwa kuzalishwa.

Mkapa alisema ni wazi kwamba kwa sasa teknolojia imeathiri maisha ya watu wengi na anaona ipo haja ya kuangalia namna ya kuwa na teknolojia ya digitali  ambayo inawafanya vijana kuwa wazalishaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles