26.2 C
Dar es Salaam
Friday, December 3, 2021

VAT umeme wa Zanzibar yafutwa

Na Mwandishi Wetu -Dar es Salaam

BARAZA la Mawaziri limeridhia kufuta Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa umeme unaouzwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwenda Shirika la Umeme la Zanzibar (Zeco) na kufuta malimbikizo ya deni la kodi hiyo lililokuwa limefika Sh bilioni 22.9.

 Taarifa iliyotumwa kwa umma jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, ilisema Baraza la Mawaziri limefanya uamuzi huo jana Ikulu Dar es Salaam katika kikao kilichoongozwa na Rais Dk. John Magufuli.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Rais Magufuli alisema baada ya kufanya uamuzi huo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango atawasilisha marekebisho madogo ya sheria ya VAT, sura ya 148 kupitia sheria ya fedha ya mwaka 2019 ili umeme unaouzwa Tanzania Zanzibar utozwe VAT kwa kiwango cha asilimia sifuri.

“Kwahiyo madeni yatakayokuwa yanadaiwa kwa Zanzibar ni yale madeni ya kulipia umeme, umeme wametumia kiasi fulani wanalipa kama wanavyolipa wa maeneo mengine kwa mfano wanavyolipa Dar es Salaam, suala la kutoza VAT sasa halipo.

“Na katika hilo kwa sababu kulikuwa na deni ambalo lilikuwa limefika Sh bilioni 22.9, sisi Baraza la Mawaziri tutapeleka mapendekezo bungeni kwamba lisamehewe kwa sababu lipo ndani ya bajeti ya mwaka huu wa 2018/19, kwa hivyo litapunguza mapato yatakayotakiwa kukusanywa na Serikali,” alisema Rais Magufuli.

Kwa upande wake, na Dk. Shein alisema pamoja kuridhia utozaji wa VAT kwa kiwango cha asilimia sifuri, Baraza la Mawaziri pia limekubaliana kuwa Makamu wa Rais, Samia ataitisha vikao vya kuzungumzia masuala ya Muungano kila mara kunapokuwa na hoja ili kujadili na kutoa uamuzi. “Tungependa sana mambo haya yafanyike vizuri kwa sababu pande mbili za Muungano zinatuhusu wote, hili ni muhimu kwa sababu mambo yakikusanyika mengi wananchi wanahisi hatusaidii jitihada zao. “Kwa hivyo tumeridhia kuwa masuala ya Muungano ambayo yapo chini ya Makamu wa Rais, wakae pamoja wayajadili ili yapate uamuzi wa pande zote mbili,” alisema  Dk. Shein. Wakati huo huo, Rais Magufuli amemwapisha Anjellah Kairuki kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji. Kairuki aliyekuwa Waziri wa Madini, ameapishwa kabla ya kuanza kwa kikao cha Baraza la Mawaziri kufuatia mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais Magufuli Januari 8.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,875FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles