23.3 C
Dar es Salaam
Sunday, October 6, 2024

Contact us: [email protected]

CAG ahojiwa kwa saa tatu

Na RAMADHAN HASSAN – DODOMA

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, amefika mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ambayo ilitumia zaidi ya saa tatu kumhoji.

Kuhojiwa huko kumekuja kufuatia wito wa Spika Job Ndugai alioutoa Januari 7, mwaka huu akitaka kiongozi huyo afike kwenye kamati hiyo kutokana na kauli yake aliyosema kuwa ‘Bunge ni dhaifu’.

CAG alianza kuhojiwa saa 5:07 asubuhi na kutoka saa 8:47 mchana.

Katika mahojiano hayo, CAG alitoka nje ya ukumbi wa mkutano huo mara kadhaa na kisha kurudi ndani kutolea ufafanuzi baadhi ya hoja.

Mara ya kwanza alitoka nje saa 6:45 mchana na kurudi tena ndani saa 7:15. Alipumzika kwa nusu saa kabla ya kurudi tena.

Pia alitoka saa 7:58 mchana na kurudi saa 8:35 mchana hadi alipotoka tena na kuondoka saa 8:47 mchana.

KUTOTUMIA GARI YA CAG

Profesa Assad aliwasili katika viwanja vya Bunge saa 4:46 asubuhi akiwa katika gari jeupe lenye namba za usajili STL 6249 akiwa na dereva.

Alipitia katika geti ambalo linatumiwa na wafanyakazi na Waziri Mkuu ambako alikaguliwa katika mashine kama watu wengine wa kawaida.

Mara baada ya kufika katika mashine, aliamuriwa kuvua viatu, koti, saa na kutoa simu ili aweze kupita.

Utaratibu huo si wa kawaida kwa CAG kwani katika siku za nyuma, alikuwa akiingia viwanja vya Bunge akiwa katika gari lake lenye namba za CAG na alikuwa akaguliwi geti la nje.

Pia huambatana na walinzi pamoja na wasaidizi wake wengine.

Pamoja na mabadiliko ya utaratibu huo, jana huku akionesha kujiamini, alivua vyote alivyotakiwa akiwa getini na kisha kupita katika mashine ya kukagulia watu wanaoingia kwenye viwanja vya Bunge.

Profesa Assad mara baada ya kuingia getini akiwa amebeba begi jeupe, alipokewa na askari kanzu wa Bunge na kuambatana naye hadi lango la kuingilia jengo la utawala ambako aliketi katika viti vya mapokezi kusubiri maelekezo.

Baadae alisalimiana na Katibu wa Spika wa Bunge, Saidi Yakubu na alipatiwa kitabu cha kusaini.

Mara baada ya kusaini aliketi kwa muda akisubiri kuitwa kuingia ukumbini.

Wakati akiwa amekaa huku akisubiri muda ufike, Profesa Assad alitoa makaratasi katika begi lake na kuanza kuzisoma nyaraka mbalimbali kwa umakini.

Mara baada ya kusoma kwa muda karatasi hizo, alinyanyuka na kwenda katika mashine ya kutolea fedha (ATM) iliyopo ndani ya jengo la utawala na MTANZANIA ilimshuhudia akitoa kiasi fulani cha fedha.

Profesa Assad aliitwa kuingia ukumbini saa 5.05 asubuhi na kuingia rasmi ndani ya ukumbi dakika mbili baadaye ambako aliwasalimia wajumbe 17 wa kamati hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti Emmanuel Mwakasaka na kuwasha kompyuta mpakato yake aliyokuwa nayo.

Mwakasaka alimkaribisha Profesa Assad mbele ya kamati na kuwaomba waandishi wa habari watoke nje ya ukumbi kwa kuwa wameshashuhudia ujio wake.

 “Shahidi ameshafika mbele ya kamati, Profesa Assad karibu sana, tunawaomba waandishi mtupishe maadam ameshafika mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge tunashukuru sana,” alisema Mwakasaka ambaye pia ni mbunge wa Tabora Mjini.

KAMATI YATOKA NA MAJIBU

Mwenyekiti Mwakasaka akiwa na makamu wake Dk. Christina Ishengoma alisema kwamba Profesa Assad ametoa ushirikiano mkubwa kwao.

“Nithibitishe kwamba Profesa Assad ambaye ndiye CAG, leo ameitikia wito na baada ya kufika ametoa ushirikiano kwa masuala mbalimbali ambayo tumemuuliza na ambayo yalitokana na mwito.

“Na tumemuhoji na bado tunaendelea na shauri hili, lakini pia kamati imefanya kazi yake sio kwamba ndio tumemaliza, ukiishamsikiliza shahidi, sisi tunaita shahidi sehemu zingine anaitwa mtuhumiwa, lakini sisi kwa kanuni zetu tunaita shahidi,” alisema.

Alisema kuna uchambuzi wataendelea nao na mara baada ya kumaliza suala hilo watalipeleka kwa Spika Ndugai kupatiwa ufumbuzi.

“Na tukiishamsikiliza kuna uchambuzi tunaendelea nao, lakini tukikamilisha suala lake kwa mujibu wa kanuni zetu tukimaliza tutalipeleka kwa Spika,” alisema.

Alipoulizwa CAG amejitetea nini, Mwakasaka alisema; “Suala lolote unapoitwa mtu atakuja na vielelezo vyake, lakini vielelezo vile ambavyo alikuja navyo bado vinafanyiwa kazi, kwahiyo hatuwezi kuviongelea katika hatua ya sasa.

“Lakini pia nimewaambia kwa mujibu wa kanuni zetu tukiishakamilisha kazi tunapeleka kwa Mheshimiwa Spika ambaye sasa yeye kama kuna hatua inafuata atatujuza.

“Kwa hiyo kama umesikia habari ya vielelezo kwamba ameleta, sisi hatuwezi kulizungumzia hilo kwa sababu bado tunalifanyia kazi.”

Alipoulizwa kama kumekuwa na mgogoro kati ya CAG na Bunge, mwenyekiti huyo alikana huku akidai kwamba lazima watu wakumbuke kwamba Bunge ni mhimili unaojitegemea.

“Sasa hapa hakuna mgogoro labda kati ya Spika na CAG, huu ni mhimili, sasa kwa yale ambayo yalikuwa yametamkwa na nyinyi (waandishi wa habari) mmeyaandika sana, ndiyo yamemfikisha hapa.

“Kama tunavyosema, ile ‘body language’ ambayo amekuja nayo nimewaambia ‘from the beginning’ (tangu mwanzo) kwamba hakuonesha ukaidi wa aina yoyote, ametoa ushirikiano mkubwa kwa kamati, tumemuhoji kama ambavyo tulivyotarajia, naye amejibu kama ambavyo anatakiwa kujibu kwenye mahojiano yoyote,” alisema.

Kuhusiana na mapendekezo ya kamati hiyo juu ya suala hilo, mwenyekiti huyo alisema jambo hilo limebaki kuwa siri ya kamati.

“Sasa hilo ni suala la uchambuzi na kwa sasa hatuwezi kuzungumzia mapendezo kwa sababu nimewaambia imebaki ni siri ya kamati, hatuwezi kuzungumzia lolote kuhusiana na hilo,” alisema.

MDEE KUHOJIWA LEO

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) anatarajiwa kuhojiwa leo na kamati hiyo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mwakasaka alisema mbunge huyo anatarajiwa kuhojiwa leo saa tano asubuhi katika ukumbi wa Spika ndani ya Bunge.

“Ile ratiba ambayo mnayo ipo vilevile haijabadilika, kwahiyo atahojiwa muda ule ule ambao amehojiwa CAG, kwa maana saa tano kamili,” alisema.

ILIVYOKUWA

Januari 7 mwaka huu, Spika Ndugai alitoa wito kwa CAG kufika mbele ya kamati hiyo kwa madai ya kulidhalilisha Bunge vinginevyo atapelekwa akiwa amefungwa pingu.

Hivi karibuni, Profesa Assad alipokuwa akihojiwa na Mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, Arnold Kayanda, aliulizwa kuwa ofisi yake imekuwa ikijitahidi kila mwaka kufanya ukaguzi na kutoa ripoti zenye kuonyesha kuna ubadhirifu lakini baada ya hapo wananchi hawaoni kinachoendelea.

CAG alijibu; “Hilo ni jambo ambalo kimsingi ni kazi ya Bunge. Kama tunatoa ripoti zinazoonesha kuna ubadhirifu halafu hatua hazichukuliwi, huo kwangu ni udhaifu wa Bunge. Bunge linatakiwa kusimamia na kuhakikisha pale panapoonekana kuna matatizo basi hatua zinachukuliwa.

“Sisi kazi yetu ni kutoa ripoti. Na huu udhaifu nafikiri ni jambo lenye kusikitisha. Lakini ni jambo ambalo muda si mrefu huenda litarekebishika. Ni tatizo kubwa ambalo tunahisi Bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa.

“Sitaki kuwa labda nasema hili kwa sababu linahusisha watu fulani, lakini ninachotaka kusema ni kuwa Bunge likifanya kazi yake vizuri, hata huu udhaifu unaoonekana utapungua.”

Maagizo hayo ya Spika yaliibua sintofahamu katika mitandao ya kijamii huku wasomi na watu wa kada mbalimbali wakiwemo wabunge wakionesha kuyapinga.

Walioonesha kupinga hadharani ni pamoja na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT Wazalendo) ambaye alifungua kesi katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam kuzuia CAG asihojiwe na Bunge.

Lakini Mahakama Kuu Tanzania ilikataa kuipokea kesi hiyo na kuisajili ikieleza kuwa ina kasoro za kisheria kutokana na hati za viapo vya wadai wanne pamoja na hati ya wito wa Spika Ndugai na hati ya kiapo cha CAG kutokuambatanishwa kwenye hati ya maombi.

Katika kesi hiyo, Zitto na wenzake walikuwa wanaiomba mahakama itoe tafsiri ya kinga ya CAG iliyopo kikatiba na pia kutoa tafsiri ya sheria ya haki, kinga na madaraka ya Bunge katika kushtaki watu wanaosemekana kudharau Bunge.
Lakini Januari 17 mwaka huu, Profesa Assad aliibuka na kukubali wito wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kama alivyotakiwa na Spika Ndugai.

Pia alinukuliwa na vyombo vya habari akidai kwamba   majibu yake katika mahojiano yaliyozua mjadala hayakuwa na nia ya kulidhalilisha Bunge.

Mkaguzi huyo alibainisha kuwa neno udhaifu ni la kawaida kwa wakaguzi katika kutoa maoni ya utendaji wa mifumo ya taasisi mbalimbali.

“Maneno kama udhaifu na mapungufu ni lugha ya kawaida sana kwa wakaguzi katika kutoa maoni ya utendaji wa mifumo ya taasisi mbalimbali,” alisema Profesa Assad.

Alisema ni wazi kuwa watu wengine wanaweza kuchukua tafsiri tofauti ya maneno kama hayo ambayo yamesababisha malumbano makali na marefu katika nyanja zote za mawasiliano kuhusu rai na nafasi na maamuzi mbalimbali yaliyochukuliwa na viongozi mbalimbali na wanasiasa.
“Ni wazi kuwa watu wengine wanaweza kuchukua tafsiri tofauti ya maneno kama haya. Yametokea malumbano makali na marefu katika nyanja zote za mawasiliano kuhusu rai, nafasi na maamuzi mbalimbali yaliyochukuliwa na viongozi.

“Januari 15, nilipokea wito wa kisheria ulionitaka kutokea mbele ya Kamati ya Bunge tarehe 21 Januari mwaka huu, kwa mantiki ya kudumisha mahusiano mazuri kati ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali na Bunge, ninayo nia ya kuitikia wito huo hapo tarehe 21,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles