27.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

UWT kuwezesha wanawake nchini kupata nishati safi ya kupikia

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) umedhamiria kwa vitendo kutekeleza dhamira ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha inamtua kuni mwanamke kichwani kwa kuhakikisha inazalisha nishati mbadala ya kupikia.

Hayo yameelezwa leo Machi 28, 2024 jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa UWT, Jokate Mwegelo baada ya kufanya mazungumzo na wawekezaji kutoka jimbo la Changzho nchini China walioletwa nchini na kampuni ya Amec Group kwa kushirikiana na Canopus Energy Solution kuona namna gani wanaweza kusaidia uwekezaji hasa sekta ya nishati.

“Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilitoa maelekezo kwa Jumuiya zake kuweza kujitegemea, hivyo sisi kama UWT tumekuwa tukikimbizana ili kuhakikisha tunapata wawekezaji ili kuendeleza maeneo yetu nchi nzima,” amesema Jokate.

Amesema UWT wanampango wa kuzalisha mkaa mbadala unaotokana na vumbi la makaa ya mawe hivyo kutokana na wawekezaji huo kujikita zaidi kwenye teknolojia itawasaidia kurahisisha uzalishaji.

Jokate amesisitiza kuwa katika miradi yote watahakikisha wanajielekeza katika kumuwezesha mwanamke hivyo chochote watakachoanzisha kitamgusa mwanamke moja kwa moja ili kuhakikisha wanamuinua kiuchumi.

“Tunajivunia kuwa na kundi kubwa la wanawake, hivyo tunauwezo wa kuwafikia wanawake wote nchini, hii ina maana kwamba tukijua hawa wawekezaji watakuja kuwekeza kwenye maeneo gani tutahakikisha tunawafikia wanawake husika,” amesema.

Pia Jokate ametoa rai kwa wanawake nchini kuungana, kuwezeshana na kujengana kiuchumi na kwamba kwa kufanya hivyo wanaweza kufanya mambo makubwa katika uchumi wao na Taifa kwa jumla.

Ameongeza kuwa kwa sasa wapo kwenye usajili wa wanawake kote nchini kwenye mfumo wao hivyo hiyo itawasaidia kuendelea kuwaunganisha wanawake ili hata sera za nchi zilizowekwa ziwasaidie.

Kwa upande wake, Mhandisi Anna Nyangasiwa kutoka Kampuni ya Canopus Energy Solutions amesema wawekezaji hao wamevutiwa na mpango wa UWT wa matumizi ya nishati mbadala hivyo watakapo kuja kwa ajili ya uwekezaji watajikita katika matumizi ya nishati mbadala kwa kutumia teknolojia ili kusaidia jitihada za Rais Samia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles