28.6 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

UWEKEZAJI WA MATAJIRI UTAIBEBA SERENGETI BOYS 2019

Na Dina Ismail-TUDARCo


HIVI karibuni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilimtangaza Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, kuwa mlezi wa timu ya Taifa ya Vijana walio chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’.

TFF ilisema kwamba, imeamua kumpa Mengi wadhifa huo kutokana na kuwa mdau mkubwa wa soka la vijana nchini, pia amekuwa akiifuatilia kwa karibu timu hiyo kwenye mashindano mbalimbali.

“Mengi amekuwa ni mpenda maendeleo ya soka, hususan soka la vijana na pia amekuwa shabiki mkubwa wa Serengeti Boys,” alisema Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Ndimbo alisema kuwa Mengi ni  mwanamichezo ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kukuza na kuendeleza soka la vijana, hivyo wanaamini kwa ushirikiano naye kutakuwapo matunda mazuri katika ustawi wa soka hilo.

“Mara kadhaa amekuwa akiwasiliana na TFF kufuatilia maendeleo ya Serengeti Boys kwenye mashindano mbalimbali. Tunafarijika kukubali kuwa mlezi wa timu hii na tunaamini kwa pamoja tutaifanya timu hii kuwa msingi mzuri katika maendeleo ya ustawi wa soka la Vijana,” alisema Ndimbo.

Uteuzi wa Mengi katika timu hiyo ni hatua nzuri na hasa ikizingatiwa kuwa timu hiyo inahitaji sapoti kubwa kutoka kwa wadau ili kuiwezesha kufika mbali ama kuwa na mafanikio katika michuano itakayoshiriki.

Ikumbukwe kuwa, vijana hao wanatarajiwa kushiriki fainali za Afrika (AFCON) kwa vijana wenye umri huo zinazotarajiwa kufanyika nchini mwakani.

Serengeti Boys itashiriki fainali hizo kama timu mwenyeji, ilishika nafasi ya tatu katika fainali za kusaka mwakilishi wa AFCON katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), zilizomalizika mwezi uliopita jijini Dar es Salaam, ambapo Uganda ‘The Kobs’ walitwaa ubingwa.

Kupitia michuano hiyo, Serengeti ilionesha uwezo wa hali ya juu uwanjani kiasi cha kutabiriwa kuwa ingeweza kutwaa ubingwa, lakini bahati haikuwa yao na kuishia nafasi hiyo.

Umahiri, uwezo na vipaji vya hali ya juu walivyoonyesha vijana hao ilidhihirisha kwamba vipaji hivyo vikitunzwa na kuendelezwa vema vitakuwa hazina kubwa ya baadaye.

Tukirejea kwa Mengi, sina shaka na uteuzi wake huo, kwani naamini sasa tutafanikisha maendeleo ya soka nchini kwa kuanzia ngazi ya vijana.

Lakini muhimu ni kwa TFF kumpa ushirikiano wa kutosha Mengi pamoja na wadau wengine waliomo katika jopo la kuipa sapoti Serengeti Boys, ili iweze kufika mbali kama si kutwaa ubingwa katika michano itakayoshiriki.

Kwani kwa nyakati tofauti, TFF imekuwa ikilia hali mbaya ya kifedha na kuomba wadau kuisaidia kuokoa jahazi, si kwa timu hiyo tu, bali kwa timu zake zote kuanzia ile ya wakubwa ‘Taifa Stars’, ya wanawake ‘Twiga Stars’, soka la ufukweni na ile ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes’.

Hivyo Mengi kama mfanyabiashara mkubwa kwa mapenzi na moyo wa huruma kwa timu hiyo hatashindwa kutafuta wadau ambao atashirikiana nao katika kuisaidia timu hiyo.

Kwa karne ya sasa, kunahitajika uwekezaji mkubwa wa timu na hasa za vijana ili kuweza kuwa na Taifa lenye mafanikio katika siku za usoni, hivyo uwekezaji bila fedha hauwezi kuwa na manufaa.

Timu itahitaji kupiga kambi ya maandalizi iliyokamilika, yaani uwanja na makazi mazuri, mechi za kujipima ubavu ndani na nje ya nchi, fedha za kujikimu pamoja na mishahara ya viongozi wa benchi la ufundi, sasa bila fedha hayo hayawezi kutimia.

Na kwa kuiwekea misingi mizuri Serengeti Boys ni kwamba itakuwa mtambo wa kuzalisha wachezaji mahiri tutakaowategemea katika timu za Ligi Kuu na hata Timu za Taifa.

Tutapata wachezaji walioiva kiakili na kimichezo, tutapata wachezaji wenye nidhamu ndani na nje ya uwanja, hivyo Mengi amekubali kuwa sehemu salama, hekima na busara zake zitaheshimika zaidi pindi timu itakapoleta neema kwa simu za usoni.

Itakuwa faraja miaka michache ijayo kuona wachezaji wa Taifa Stars karibu wote ni zao la Serengeti Boys na hata wale nyota tunaowazoea kuwika katika timu za Ligi Kuu nao tunafurahi wakitokea huko.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles