30.4 C
Dar es Salaam
Saturday, December 2, 2023

Contact us: [email protected]

UTALII Z’BAR: WAZIRI CASTICO ABEBESHWA ZIGO MPASUKO WA UTALII

 

*Wafanyakazi 150 wa hoteli kubwa wapoteza ajira

Na MWANDISHI WETU -ZANZIBAR

GIZA limetanda ndani ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), baada ya uamuzi wa Waziri wa Kazi, Uwezeshaji Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto,  Maudline Cyrus Castico, kutangaza mabadiliko ya kima cha chini cha mshahara bila kushirikisha wawekezaji wa sekta ya utalii visiwani hapa.

Kutokana na uamuzi huo ambao sasa umeanza kuathiri ajira kwa Wazanzibari wengi, zaidi ya watu 150 wamepoteza ajira kwenye sekta ya utalii hasa kwenye hoteli kubwa za kitalii.

Hatua hiyo inatokana na wawekezaji wa sekta ya utalii hasa mahoteli kuanza kupunguza wafanyakazi baada ya kushindwa kuwalipa kima hicho cha mshahara wafanyakazi wao.

Ingawa utekelezaji wa suala hilo bado haujaanza kufanyika baada ya Waziri Castico kushindwa kutoa ufafanuzi wa kina kwa wawekezaji hao ambapo mara kadhaa amekuwa akikacha vikao vya pamoja licha ya kuagizwa na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd.

Mabadiliko hayo ni wazi yameonekana kuitikisa sekta hiyo huku wamiliki wa hoteli hizo za kitalii wakijikuta wakishindwa kulipa kima kipya cha chini cha mishahara ambacho kimepandishwa kwa asilimia 109 na Waziri Castico.

Kutokana na hali hiyo, MTANZANIA lilizungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Abood, ambapo alisema kwa sasa Serikali inasubiri taarifa ya Waziri Castico ili iweze kujadili na kufanya uamuzi ambao utaleta utulivu kwenye sekta ya utalii visiwani hapa.

“Sisi bado tunasubiri taarifa ya Waziri mwenye dhamana (Castico) maana ofisi ya Makamu wa Pili ilimwandikia barua ya kumtaka akutane na wadau na kisha taarifa yake ailete iweze kujadili uamuzi huo kwa uwazi zaidi.

“Waziri aliambiwa afanye kikao na wadau ili asikilize mawazo yao sasa kama hakutokea kwenye kikao ni vizuri atafutwe mwenyewe aweze kuzungumzia hilo. Nasi katika ofisi yetu pia tulipokea maoni ya wadau na kuyashusha kwake kwa ufuatiliaji na utekelezaji ikiwemo kusikia maoni yao kutokana na hali hii.

“…na lengo la Serikali yetu hatuhitaji Wazanzibari wapoteze ajira, Serikali inataka sekta ya utalii itulie mambo yaende na uchumi wa Zanzibar uzidi kukua ila kwa sasa nashindwa kusema mambo mengi kwa kuwa bado hatujapata ripoti ya Waziri mwenye dhamana,” alisema Waziri Abood.

Tangazo hilo la Waziri Castico kwa sasa limeanza kuleta athari ikiwemo kuibuka kwa mgomo wa wafanyakazi wa Kiwanda cha Maji cha Drop cha Zanzibar ambao wafanyakazi waligoma hivi karibuni wakishinikiza kulipwa kiwango kipya cha mishahara.

Wafanyakazi hao waliogoma ni pamoja na walinzi, wanaoosha chupa za maji na kutengeneza vizibo jambo ambalo limetishia kufungwa kwa baadhi ya viwanda baada ya wamiliki kushindwa kulipa kiwango hicho kipya cha Sh 300,000 hadi 500,000 kwa mwezi kama wanavyotakiwa na Serikali.

MTANZANIA lilipomtafuta Waziri Castico ili kupata ufafanuzi wa kile kinachodaiwa kuwa alikacha kikao na wadau kilichofanyika hivi karibuni, alisema yupo kwenye vikao na hawezi kuzungumza jambo lolote kwa sasa.

“Bahati mbaya nipo kwenye kikao na sijui namaliza muda gani, hivyo siwezi kusema lolote kwa sasa,” alijibu Waziri Castico.

Hata hivyo, gazeti hili lilishuhudia kazi mbalimbali hasa kwa vibarua ambao walikuwa wakifanyakazi na kulipwa kwa siku kwenye hoteli mbalimbali kisiwani hapa wakiwa wachache ambapo kwa sasa kazi ya kufanywa na watu watatu hadi wanne wamiliki wa hoteli hulazimika kumtumia mtu mmoja.

Wakati wa Uchaguzi Mkuu Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, aliahidi kupitia ilani ya CCM kupandisha kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa Serikali kutoka shilingi 150,000 hadi 300,000 huku sekta binafsi ikijikuta ikikwama baada ya kutoshirikishwa katika mchakato huo kwa mujibu wa Sheria ya Zanzibar.

Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa za Serikali ya Zanzibar, kiwango cha ajira kimeshuka kutoka ajira 1,597 mwaka 2015 hadi 1,071 mwaka 2016 ambapo kwa sasa hali inaweza kuwa mbaya zaidi huku wengi watakaoathirika ni wananchi wa visiwa vya Zanzibar.

Mabadiliko hayo yamefanyika kwa mujibu wa kifungu cha 97 (1) cha sheria ya Ajira nambari 11 ya mwaka 2005 ambapo kima cha chini kwa wafanyakazi  wenye mikataba ya maandishi kwa taasisi ndogo zitakazoainishwa kwenye kanuni kimeongezeka kutoka Sh 145,000  hadi 180,000.

Kwa wafanyakazi wenye mikataba ikiongezwa kutoka kiwango cha sasa cha Sh 145,000 hadi 300,000.

Huku kwa vibarua wa kutwa wenye ujuzi, kimeongezwa kutoka Sh 10,000  hadi 30,000  kwa siku na kwa vibarua wa kutwa wasio na ujuzi, kimeongezwa kutoka Sh 7,000 na kufikia 25,000.

Kwa mujibu wa takwimu mbalimbali ikiwemo za Serikali, zinaonyesha kwamba kati ya asilimia 100 kuna watalii zaidi ya asilimia 40 ambao huingia Zanzibar moja kwa moja na hununua likizo zao kwenye makampuni yanayouza mapumziko katika visiwa tofauti duniani huko Ulaya

Wengi kati ya hawa ni pamoja na raia kutoka Italia, Hispania, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza na nchi nyinginezo za mataifa ya Ulaya.

Pakage hiyo ya utalii huwa ni bei rahisi lakini mara nyingi ndege hujazwa kwa wingi wa watu.

Watalii huja Zanzibar kwa wiki moja na bei wanayolipa huwa moja kwa moja na usafiri wa ndege, chakula, vinywaji pamoja na usafiri wa kutoka uwanja wa ndege kwenda hoteli na kurudi tena uwanjani kwa ajili ya safari ya kurudi nchi walizotoka.

Kutokana na aina hiyo ya wageni hao, Zanzibar hushindana na nchi kama Thailand, Tunisia, Morocco, Hispania, visiwa vya Ugiriki kama Crete, Mexico, Cuba, St. Lucia pamoja na visiwa vingine.

 

Hata kwa wanaouza Zanzibar huko Ulaya tayari wanasema Zanzibar ni bei ghali sasa ikiwa mishahara itapanda kupindukia na hao itawafanya wapandishe bei ina maana katika mapumziko ya mwaka 2018 wataiondoa Zanzibar katika mabango ya kuitangaza hasa kwenye mitandao ya kununua likizo za mapumziko.

Kwenye kundi la kuuza kuna hatari ya kuweza kusababisha pigo katika hilo kwa asilimia 45 ya wageni hasa Waitaliano  wanaokuja Zanzibar moja kwa moja.

‘Msione Wazungu hawa Waitalia mkaona ni matajiri, hawa wengi ni watumishi wa umma na mafundi, ni watu wa kawaida na hujipanga miezi nyuma kununua hizo likizo,” alisema Nassor Khalfan Ally ambaye ni mmoja wa wawekezaji wa utalii visiwani hapa.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Hii ndiyo hali halisi kiuchumi Tanzania. Msimtafute mchawi, Upinzani. Ukweli ndio huu. Uhalisia ndio huu. Inabidi serikali iwaunganishe Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama kuinusuru nchi bila kutumia visingizio. Kuna Wapinzani wengi sana wenye uwezo wangehusishwa na kupewa madaraka kikazi kwenye secta mbalimbali badala ya kuteua Wanaccm tuu na wengi wao ni mizigo mitupu.Kiongozi mzuri angeunganisha vyama vyote kimatendo na kuamua kufanya kazi na wenye elimu, utaalamu, na uzalendo kwa manufaa ya Taifa. Badala yake, tumejichagua kichama, kujaribu kujisafisha yale maovu yetu, bila kuubadili mfumo wa kupendelea, kubebana, na kudanganyana. Ukitaka kutumbua? tumbua anzia wale wahusika wakuu wote waliosababisha nchi iteteleke. Rudisha Katiba na nchi iendeshwe kwa uwazi na kufuata sheria safi za nchi na si uoga unaojionyesha waziwazi kwa sasa. Watu wanaogopa kutumbuliwa, kupoteza kazi, na kuwa mahabusi. Na huu ni ukweli. Unapotumia nguvu, utendaji unayumba , na ni wachache waoga watakuwa mbele kama wapiga debe au madili. Bado kazi kubwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles