24.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

TAHARIRI: VIONGOZI TFF FUNGUENI FIKRA MPYA ZA MAENDELEO

HATIMAYE Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), umefanyika juzi mkoani Dodoma na Wallace Karia kutawazwa kuwa rais huku Michael Wambura naye akishinda wadhifa wa Makamu wa Rais wa Shirikisho hilo watakaoongoza kwa kipindi cha miaka minne.

Karia katika utawala uliopita chini ya Rais Jamal Malinzi alikuwa Makamu wa rais wa TFF na sasa amepanda juu kwa kuwa Rais wa Shirikisho hilo.

Hii ni ishara kuwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, wameonyesha kuwa na imani naye na kumwamini kwa kumchagua kuwa bosi mkuu katika shirikisho hilo kwa masilahi ya maendeleo ya soka la Tanzania.

Si kwa Karia na Wambura pekee, bali wajumbe ambao wana dhima kubwa ya kuchagua viongozi wa soka la Tanzania, waliwachagua Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ambao ni Salum Chama, Vedastus Rufano, Mbasha Matutu, Sara Chao, Issa Mrisho, Kennedy Pesambili, Elius Mwanjala, James Mhagama, Dustan Ditopile, Mohamed Adei, Francis Kumba, Khalid Mohamed na Lameck Nyambaya.

Sasa ni wakati wa viongozi wa TFF kufungua fikra mpya na kufanya kazi kwa bidii zaidi ili kulifikisha soka la Tanzania katika maendeleo bora ambayo Watanzania wengi wanapenda kuona timu yao ya Taifa ‘Taifa Stars’ ikifanya vema katika mashindano ya Afrika (Afcon) na Kombe la Dunia.

Sisi MTANZANIA tunawatakia kila la kheri viongozi wote wa TFF waliochaguliwa katika uchaguzi huo na wafanye kazi kwa masilahi ya Taifa na kwa ushirikiano wa pamoja ili wailetee Tanzania fikra mpya za maendeleo.

Tunafahamu kuwa Watanzania wana kiu kubwa ya kuona soka la Tanzania linapiga hatua ya maendeleo, hivyo viongozi wa TFF wakiongozwa na Karia wana jukumu zito la kuhakikisha maendeleo hayo yanapatikana ili iwe faraja kwao.

Bado fursa ya kufikia maendeleo ipo iwapo viongozi hao wa TFF watakuwa na umoja na ushirikiano na kufanya maamuzi bora na yenye manufaa kwa Taifa bila kuangalia masilahi yao binafsi ambayo yatadhohofisha soka la Tanzania na kuwa chanzo cha migogoro ndani ya shirikisho hilo.

Sisi MTANZANIA tunawaasa pia viongozi wa TFF watengeneze fursa za kuwavutia wadhamini ili waone taasisi hiyo ni sehemu salama ya kuwekeza, pia kusimamia misingi ya utawala bora na kujikita zaidi katika kuwekeza vipaji vya vijana kwa ajili ya maendeleo ya baadaye ya Taifa Stars.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles